The chat will start when you send the first message.
1Lakini Waisraeli walifanya dhambi katika kitu kilichowekwa wakfu; maana Akani, mwana wa Karmi, mwana wa Zabdi, mwana wa Zera, wa kabila la Yuda, alitwaa baadhi ya vitu vilivyowekwa wakfu; hasira ya BWANA ikawaka juu ya Waisraeli.[#Yos 22:20]
2Kisha Yoshua akatuma watu kutoka Yeriko mpaka mji wa Ai, ulio karibu na Beth-aveni, upande wa mashariki wa Betheli, akawaambia, akisema, Pandeni juu mkaipeleleze nchi, basi wakapanda juu wakaupeleleza Ai.
3Wakarejea kwa Yoshua wakamwambia, Wasiende watu wote, ila waende watu kama elfu mbili, tatu, wakaupige Ai; usiwataabishe watu wote kwenda huko maana watu hao ni wachache tu.
4Basi watu wakaenda huko wapata elfu tatu tu; nao wakakimbizwa na wakazi wa mji wa Ai.[#Law 26:17; Kum 28:25; 32:30; Isa 30:17; 59:2]
5Watu wa Ai wakawapiga watu kama thelathini na sita; wakawafuatia kutoka mbele ya mlango mpaka Shebarimu, wakawapiga huko kwenye materemko; mioyo ya watu ikayeyuka, ikawa kama maji.[#Yos 2:9,11; Law 26:36; Zab 22:14]
6Yoshua akayararua mavazi yake, akaanguka kifudifudi mbele ya sanduku la BWANA hadi jioni, yeye na wazee wa Israeli; wakatia mavumbi vichwani mwao.[#Mwa 37:29; Hes 14:5,6; 2 Sam 13:31; Ezr 9:3-5; Est 4:1; Ayu 1:20; Mdo 14:14; 1 Sam 4:12; 2 Sam 1:2; 13:19; Neh 9:1; Ayu 2:12]
7Yoshua akasema, Ee Bwana MUNGU, kwa nini umewavusha watu hawa mto wa Yordani, ili kututia katika mikono ya Waamori, na kutuangamiza? Laiti tu, tungaliridhika kukaa ng'ambo ya Yordani[#Kut 5:22; 2 Fal 3:10]
8Ee Bwana, niseme nini baada ya Israeli kuwapa visogo adui zao?
9Maana Wakanaani na wenyeji wote wa nchi hii watasikia habari hizi, nao watatuzingira, na kulifuta jina letu katika nchi. Nawe utafanya nini kwa ajili ya jina lako kuu?[#Zab 83:4; Kut 32:12; Hes 14:13]
10BWANA akamwambia Yoshua, Haya! Inuka, mbona umeanguka kifudifudi hivi?
11Israeli wamefanya dhambi, naam, wamelivunja agano langu nililowaagiza; naam, wametwaa baadhi ya vitu vilivyowekwa wakfu; tena wameiba, tena wamevificha na kuvitia pamoja na vitu vyao wenyewe.[#Yos 6:17; Mdo 5:1]
12Ndiposa wana wa Israeli hawawezi kusimama mbele ya adui zao; wakawapa visogo adui zao, kwa sababu wamelaaniwa; mimi sitakuwa pamoja nanyi tena, msipokiharibu kitu kile mlicho nacho kilichowekwa wakfu.[#Hes 14:45; Amu 2:14; Kum 7:26; Yos 6:18]
13Haya! Inuka, uwatakase watu, ukaseme, Jitakaseni, muwe tayari kesho; maana BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi; Kitu kilichowekwa wakfu kiko katikati yako, Ee Israeli; huwezi kusimama mbele ya adui zako, hata mtakapokiondoa kile mlicho nacho kilichowekwa wakfu.[#Kut 19:10; Yos 3:5]
14Basi asubuhi mtaletwa karibu nami kabila kwa kabila; kisha itakuwa ya kwamba kabila ile atakayoitwaa BWANA itakaribia jamaa kwa jamaa; na jamaa ile atakayoitwaa BWANA itakaribia nyumba kwa nyumba; na nyumba ile atakayoitwaa BWANA itakaribia mtu kwa mtu.[#1 Sam 10:19-21; 14:41,42; Mit 16:33; Yon 1:7; Mdo 1:24-26]
15Tena itakuwa ya kwamba yeye atakayetwaliwa, naye anacho kitu kile kilichowekwa wakfu, atateketezwa kwa moto, yeye na vitu vyote alivyo navyo; kwa sababu amelivunja agano la BWANA, na kwa sababu ametenda upumbavu katika Israeli.[#1 Sam 14:38,39; Mwa 34:7; Amu 20:6]
16Basi Yoshua akaondoka asubuhi na mapema, akawasongeza Israeli kabila kwa kabila; kabila la Yuda likatwaliwa.
17Akazisongeza jamaa za Yuda, akaitwaa jamaa ya Wazera; akaisongeza jamaa ya Wazera mtu kwa mtu; Zabdi akatwaliwa.
18Akawasongeza watu wa nyumba yake mmoja mmoja; na Akani, mwana wa Karmi, mwana wa Zabdi, mwana wa Zera, wa kabila la Yuda akatwaliwa.[#Mwa 4:7; Hes 32:23; Mit 13:21; Yer 2:26; Mdo 5:1-10]
19Yoshua akamwambia Akani, Mwanangu, nakusihi, umtukuze BWANA, Mungu wa Israeli, ukaungame kwake; uniambie sasa ulilolitenda; usinifiche.[#1 Sam 6:5; Yer 13:16; Yn 9:24; Hes 5:6,7; 2 Nya 30:22; Zab 51:3; Dan 9:4]
20Akani akamjibu Yoshua, akasema, Kweli nimefanya dhambi juu ya BWANA, Mungu wa Israeli, nami nimefanya mambo haya na haya.
21Nilipoona katika nyara joho zuri la Babeli, na shekeli mia mbili za fedha, na kabari ya dhahabu, uzani wake shekeli hamsini, basi nilivitamani nikavitwaa; tazama, vimefichwa mchangani katikati ya hema yangu, na ile fedha chini yake.[#Kut 20:17; 1 Fal 21:1; 2 Fal 5:20-27; Mit 15:27; Hab 2:9; Lk 12:15; Rum 7:7,8; Efe 5:5; 1 Tim 6:10]
22Basi Yoshua akatuma wajumbe wakapiga mbio mpaka hemani; na tazama, vile vitu vilikuwa vimefichwa hemani mwake, na ile fedha chini yake.
23Wakavitoa kutoka hapo katikati ya hema, wakavileta kwa Yoshua, na kwa wana wa Israeli wote, nao wakaviweka chini mbele za BWANA.
24Kisha Yoshua, na Israeli wote pamoja naye, wakamtwaa Akani, mwana wa Zera, na ile fedha, na lile joho, na ile kabari ya dhahabu, na wanawe, na binti zake, na ng'ombe wake, punda wake na kondoo wake, hema yake na vitu vyote alivyokuwa navyo, wakavileta juu hadi bonde la Akori.[#Yos 15:7]
25Yoshua akasema, Mbona umetufadhaisha hivi? BWANA atakufadhaisha wewe leo. Ndipo Israeli wote wakampiga kwa mawe, kisha wakawateketeza kwa moto, na kuwapiga kwa mawe.[#Yos 6:18; 1 Fal 18:17; 1 Nya 2:7; Gal 5:12; Kum 17:5]
26Kisha wakakusanya juu yake rundo kubwa la mawe hata leo; naye BWANA akauacha ukali wa hasira yake. Kwa sababu hiyo jina la mahali pale likaitwa, Bonde la Akori, hata leo.[#Yos 8:29; 2 Sam 18:17; Omb 3:53; Kum 13:17; 2 Sam 21:14; Isa 65:10; Hos 2:15; #7:26 maana yake ni ‘bonde la taabu’.]