The chat will start when you send the first message.
1Usitende uovu, na uovu usikupate;
2Ukae mbali na dhambi, ikae mbali nawe.
3Mwanangu, usipande mifuoni mwa udhalimu,
usije ukavuna mara saba.
4Usitake ukubwa kwa BWANA,
Wala kiti cha mbele kwa mfalme.
5Usijifanye una haki mbele za BWANA; wala usijifanye una hekima mbele ya mfalme.
6Wala usitake kuwa hakimu, usije ukashindwa usiweze kuondoa udhalimu; pia na usije ukamjali mtu mwenye cheo, au kuiharibu adili yako kwa kutwaa rushwa.
7Usiwe mkosefu kwa wenyeji wa mjini,
Wala kutupa heshima yako mbele ya watu.
8Usikubali kutenda dhambi mara mbili,
Hata dhambi moja haikosi adhabu.
9Usiseme, Atatazama wingi wa sadaka zangu,
Nikimtolea Aliye Juu kafara ataikubali.
10Usiwe mlegevu wa kusali,
Wala usikawie kutoa sadaka.
11Usimdhihaki aonaye uchungu,
Yuko mwenye kudhili na kukweza.
12Usitunge uongo juu ya ndugu yako,
Wala juu ya rafiki usifanye hivi.
13Usipende kusema uongo wowote,
Hakuna tumaini jema katika huo.
14Usifanye kubabaika katika mkutano wa wakuu,
Wala usipayukepayuke wakati unaposali.
15Usiikirihi kazi ya mikono,
Wala ukulima ulioagizwa na BWANA.
16Usihesabike pamoja na wakosaji,
Kumbuka ghadhabu haikawii.
17Ujinyenyekeshe sana roho yako,
Adhabu ya wakosaji ni moto na funza.
18Usimbadili rafiki yako hata kwa kitu tunu,
Wala ndugu amini hata kwa dhahabu ya Ofiri.
19Usijinyime mke aliye mwema mwenye akili, kwa maana neema yake hupita dhahabu.
20Mtumishi atendaye kazi yake vizuri usimtende mabaya, wala mtu wa mshahara akupaye maisha yake.
21Umpende mtumishi mwenye akili kama nafsi yako, wala usimnyime uhuru wake.[#Kut 21:2; Kum 15:12-15]
22Ikiwa una ng'ombe, uwaangalie, na wakiwa wanakufaa wakae kwako.
23Ikiwa una watoto uwarudi, bali uwapatie wake zao wakati wa ujana wao.
24Ikiwa una binti, uwalinde miili yao, bali usiwaangazie uso wako.
25Umwoze binti yako, nawe utakuwa umemaliza jambo kubwa; tena umpe mtu mwenye ufahamu.
26Iwapo una mke akupendezaye usimchukie; lakini usijitie nafsi yako katika mikono ya mke akuchukizaye.
27Baba yako umtukuze kwa moyo wako wote, wala usisahau uchungu wa mama yako;[#Kut 20:12]
28ukumbuke ya kuwa ulizaliwa nao, nawe utawezaje kuwalipa kwa hayo waliokutendea?
29Mche BWANA kwa roho yako yote; tena uwaheshimu makuhani wake.
30Kwa nguvu zako zote umpende Yeye aliyekuumba, wala usiwaache wahudumu wake.
31Umtukuze BWANA, na kumheshimu kuhani, ukampe sehemu yake kama ulivyoamriwa; chakula cha sadaka ya dhambi, na toleo la bega, na kafara ya utakaso, na malimbuko ya vitu vilivyo vitakatifu.
32Aidha, umnyoshee maskini mkono wako, ili baraka upewayo ikamilike.
33Kipawa kina neema machoni pa kila mtu aliye hai; yeye naye aliyefariki usimzuilie neema yako.
34Usikose kuwapo pamoja nao waliao, tena omboleza pamoja nao wanaoomboleza.
35Wala usisahau kwenda kumtazama mgonjwa, mradi ukifanya hivi utapata kupendwa na watu.
36Na katika mambo yako yote uukumbuke mwisho wako, hivyo hutakosa kamwe hata hatima.