Yudithi 15

Yudithi 15

Ushindi wa Israeli

1Wanajeshi waliposikia kilichotukia, waliogopa,

2wakaanza kutetemeka kwa hofu; hakuna aliyemngoja mwenzake; bali kwa nia moja walijaribu kukimbia kwa kupitia njia za milimani na mabondeni.

3Wanajeshi waliokuwa wamepiga kambi zao milimani kuuzunguka mji wa Bethulia, nao wakaanza kukimbia. Ndipo wanajeshi wote wa Israeli wakatoka wakawafuatia nyuma.

4Uzia akatuma wajumbe kwenye miji ya Betomesthaimu, Bebai, Koba, Kola na nchi nzima ya Israeli, kuwaambia Waisraeli yaliyotukia na kuwahimiza kuungana na wenzao kuwafuatia maadui na kuwaangamiza.

5Basi watu wa Israeli walipopata habari hizo, wote kwa pamoja wakawashambulia hao Waashuru na kuwafukuza hadi mji wa Koba huku wanawaua hao maadui. Hata watu wa mjini Yerusalemu na wengine waliokaa sehemu za milimani wakaungana na wenzao kuwashambulia (maana watu walikuwa wamewaambia mambo yaliyotokea katika kambi ya maadui zao), nao Wagileadi na Wagalilaya wakawazunguka na kuwashambulia Waashuru wanapokimbia, na wakawaua Waashuru wengi sana mpaka walipopita Damasko na mipaka yake.

6Wakati huo huo watu wengine waliobaki mjini Bethulia walikwenda kwenye kambi ya Waashuru, wakateka mali nyingi iliyowatajirisha sana.

7Wanajeshi wa Israeli waliporudi kutoka kuwaua maadui, walichukua chochote kilichosalia kambini. Kulikuwa na mali nyingi hata watu wa miji na vijiji vya karibu milimani na sehemu tambarare walipata nyara nyingi.

Waisraeli wanasherehekea ushindi

8Kuhani mkuu Yoakimu na halmashauri kuu ya Israeli wakaja kutoka Yerusalemu kujionea wenyewe mambo makubwa ambayo Bwana alikuwa amewafanyia watu wa Israeli na kukutana na Yudithi ili kumpongeza.

9Walipowasili, wote kwa pamoja wakamsifu Yudithi wakisema, “Wewe ni utukufu wa Yerusalemu! Wewe ni fahari ya taifa la Israeli na sifa kuu ya taifa letu.

10Maana kwa mkono wako mwenyewe umefaulu kufanya haya yote. Umelifanyia mema taifa la Israeli; Mungu amependezwa nayo. Ubarikiwe na Mungu Mwenye Nguvu katika siku zote zijazo.” Nao watu wote wakaitikia, “Amina.”

11Iliwachukua watu siku thelathini kubeba vitu vilivyokuwa katika kambi ya Waashuru. Yudithi akapewa hema ya Holoferne na vitu vyote vilivyokuwamo: Fedha, mabakuli, makochi na vitu vingine vyote. Akavichukua na kuvipakia juu ya nyumbu wake kadiri alivyoweza; kisha akaleta magari yake ya punda na kuyajaza vitu alivyochukua.

12Wanawake wote Waisraeli wakaja kumwona Yudithi; wakamwimbia nyimbo za kumsifu, baadhi yao wakamchezea ngoma. Naye Yudithi alichukua matawi mikononi mwake na kuwagawia wanawake waliofuatana naye.

13Walijivika taji za majani ya mizeituni; yeye na wale walioandamana naye. Halafu akiwa anawatangulia watu wote aliongoza wanawake wote wakicheza ngoma huku wanaume wote wa Israeli wakiwafuata wakiwa wamebeba silaha zao na wamevaa mashada ya maua vichwani mwao huku wakiimba nyimbo za sifa.

14Basi Yudithi akaimba wimbo wa shukrani mbele ya Waisraeli wote, na watu wakaimba pamoja naye wimbo huu wa sifa.

Swahili Common Language DC Bible: Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki © Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya, 1995, 2001. Haki zote zimehifadhiwa.  
Published by: Bible Society of Tanzania