The chat will start when you send the first message.
1Mimi ni ua la Sharoni,
ni yungiyungi ya bondeni.
2Kama yungiyungi kati ya michongoma,
ndivyo alivyo mpenzi wangu kati ya wasichana.
3Kama mtofaa kati ya miti ya msituni,
ndivyo alivyo mpenzi wangu kati ya wavulana.
Nafurahia kuketi chini ya kivuli chake,
na tunda lake tamu sana kwangu.
4Alinichukua hadi ukumbi wa karamu,
akatweka bendera ya mapenzi juu yangu.
5Nishibishe na zabibu kavu,
niburudishe kwa matofaa,
maana naugua kwa mapenzi!
6Mkono wake wa kushoto chini ya kichwa changu,
mkono wake wa kulia wanikumbatia.
7Nawasihi enyi wanawake wa Yerusalemu,
kama walivyo paa au swala wa porini,
msiyachochee wala kuyaamsha mapenzi,
hadi hapo wakati wake utakapofika.
8Hiyo ni sauti ya mpenzi wangu,
yuaja mbio,
anaruka milima,
vilima anavipita kasi!
9Mpenzi wangu ni kama paa,
ni kama swala mchanga.
Amesimama karibu na ukuta wetu,
achungulia dirishani,
atazama kimiani.
10Mpenzi wangu aniambia:
“Inuka basi, ewe mpenzi wangu, unipendezaye,
njoo twende zetu.
11Tazama, majira ya baridi yamepita,
nazo mvua zimekwisha koma;
12maua yamechanua kila mahali.
Wakati wa kuimba umefika;
sauti ya hua yasikika mashambani mwetu.
13Mitini imeanza kuzaa;
na mizabibu imechanua;
inatoa harufu nzuri.
Njoo, basi, ewe mpenzi wangu unipendezaye,
njoo twende.
14Ee hua wangu, uliyejificha miambani.
Hebu niuone uso wako,
hebu niisikie sauti yako,
maana sauti yako yapendeza na uso wako wavutia.
15“Tukamatieni mbweha,
wale mbweha wadogowadogo,
wanaoiharibu mizabibu yetu inayochanua.”
16Mpenzi wangu ni wangu, nami ni wake.
Yeye hulisha kondoo wake penye yungiyungi,
17hadi hapo jua linapochomoza
na vivuli kutoweka.
Rudi kama paa mpenzi wangu,
kama swala mdogo juu ya milima ya Betheri.