The chat will start when you send the first message.
1Hekima alimlinda yule aliyeumbwa kwanza, baba wa ulimwengu,
aliyeumbwa peke yake kabla ya wengine.
Hekima alimwokoa kutoka kosa lake,
2akampa nguvu ya kutawala vitu vyote.
3Lakini mtu mmoja mkosefu alijitenga naye katika hasira yake,
akaangamia kwa kumuua ndugu yake kutokana na ghadhabu yake.
4Kwa sababu ya mtu huyo gharika ilifurika duniani,
lakini kwa mara nyingine Hekima aliiokoa.
Alimwongoza mtu mmoja mwadilifu juu ya gharika katika mtumbwi dhaifu.
5Tena, mataifa yalipoafikiana katika uovu wao,
Hekima alimtambua mtu mmoja mwadilifu,
akanihifadhi katika unyofu wake mbele ya Mungu.
Hekima alimpa mtu huyo moyo wa kufuata amri ya Mungu
hata ingawa alimpenda sana mwanawe.
6Wakati watu waovu walipokuwa wanaangamizwa,
Hekima ndiye aliyemsalimisha mtu mmoja mwadilifu;
alimwokoa katika moto ulioshuka mbinguni na kuteketeza Miji Mitano.
7Hata sasa, ushahidi wa uovu wao unaonekana:
Nchi ya mahala hapo ni kame na inafuka moshi;
mimea ya hapo huzaa matunda lakini hayakomai kamwe;
na jiwe la chumvi limesimama hapo, kumbukumbu la mtu asiyeamini.
8Watu wa miji hiyo walimpuuza Hekima,
wasiweze kubainisha kati ya jema na baya.
Zaidi ya hayo, waliacha kumbukumbu la upumbavu wao,
ili kushindwa kwao kusisahaulike kamwe.
9Lakini Hekima aliwasalimisha hatarini wale waliomngojea kwa saburi.
10Mtu mmoja mwadilifu alipoikimbia ghadhabu ya ndugu yake,
Hekima alimwongoza katika njia sawa.
Alimwonesha ufalme wa Mungu
na kumjulisha mambo matakatifu.
Hekima alimfanikisha katika kazi zake;
alimzidishia mazao ya kazi zake.
11Wadhalimu walipotaka kunyakua mali yake kwa wivu,
Hekima alikaa upande wake na kumtajirisha.
12Hekima alimlinda na maadui zake
na kumwokoa na wale waliomvizia.
Katika mapigano makali Hekima alimpa ushindi,
apate kutambua kwamba wema una nguvu kupita chochote.
13Tena mtu mmoja mwadilifu alipouzwa utumwani, Hekima hakumwacha,
ila alimweka salama mbali na dhambi.
Hekima aliandamana naye gerezani,
14wala humo gerezani hakumwacha,
mpaka alipompa madaraka juu ya ufalme
na kumfanya mtawala juu ya mabwana zake.
Wale waliomshtaki akawadhihirisha kuwa waongo,
akamjalia heshima ya milele.
15Hekima aliwaokoa watu watakatifu wasio na hatia
makuchani mwa taifa lililowadhulumu.
16Aliingia ndani ya roho ya mtumishi mmoja wa Bwana,
naye kwa maajabu na ishara akawapinga wafalme wenye kutisha.
17Hekima aliwapa watu wa Mungu tuzo la jasho lao;
aliwaongoza katika njia ya ajabu
akawa kwao kivuli mchana
na mwanga wa nyota usiku.
18Hekima aliwavusha Bahari ya Shamu,
akawaongoza katikati ya maji mengi,
19lakini akawazamisha maadui zao
akaitosa miili yao ufuoni kutoka vilindini.
20Hivyo waadilifu wakawapokonya watu waovu,
wakaimba kulisifu jina lako takatifu, ee Bwana,
wote pamoja wakakutukuza kwa vile uliwapigania.
21Hekima aliwafumbua bubu vinywa wakaongea,
na kufanya ndimi za watoto wachanga kuongea waziwazi.