The chat will start when you send the first message.
1Amasia alikuwa mwenye miaka 25 alipoupata ufalme, akawa mfalme miaka 29 mle Yerusalemu. Jina la mama yake ni Yoadani wa Yerusalemu.
2Akayafanya yanyokayo machoni pake Bwana, lakini hakuyafanya kwa moyo wote mzima.
3Ikawa, alipoushupaza ufalme wake, akawaua watumishi wake waliomwua baba yake mfalme.[#2 Mambo 24:25.]
4Lakini wana wao hakuwaua, kwa kuwa katika Maonyo katika kitabu cha Mose imeandikwa, ya kuwa Bwana ameagiza kwamba: Baba wasife kwa ajili ya wana, wala wana wasife kwa ajili ya baba, ila kila mtu sharti afe kwa kosa lake yeye.[#5 Mose 24:16.]
5Kisha Amasia akawakusanya Wayuda, akawapanga kwa milango na kwa wakuu wa maelfu na kwa wakuu wa mamia wote pia waliokuwa Wayuda na Wabenyamini. Alipowakagua walio wenye miaka ishirini na zaidi akapata watu 300000 waliochaguliwa kwenda vitani waliojua kushika mikuki na ngao.
6Akajipatia nako kwa Waisiraeli watu wa mshahara 100000 waliokuwa mafundi wa vita wenye nguvu, akawalipa vipande mia vya fedha, ndio shilingi milioni na 200000.
7Ndipo, mtu wa Mungu alipomjia, akamwambia: Mfalme, vikosi vya Waisiraeli visiende na wewe! Kwani Bwana hawi nao Waisiraeli, maana wote ni wana wa Efuraimu.
8Kama ni kwenda, vifanye wewe, ukijishupaza, upate kupigana! Kama sivyo, Mungu atakukwaza mbele ya adui, kwani Mungu anazo nguvu za kusaidia na za kukwaza.
9Amasia akamwuliza huyu mtu wa Mungu: Tena nivifanyeje vile vipande mia vya fedha, nilivyowapa wao wa kikosi cha Waisiraeli? Ndipo, huyu mtu wa Mungu alipomwambia: Bwana anaweza kukupa zaidi ya hivyo.
10Kisha Amasia akakitenga kile kikosi kilichokuja kwake toka nchi ya Efuraimu, waende kwao; nao wakawakasirikia sana Wayuda, wakarudi kwao wenye makali yaliyowaka moto.
11Kisha Amasia akajishupaza, akawaongoza watu wake kwenda katika Bonde la Chumvi, akawapiga wana wa Seiri 10000,
12wengine 10000 wana wa Yuda wakawateka, wa hai, wakawapeleka mwambani juu, wakawakumba toka hapo juu mwambani; ndipo, wote pia walipopondeka.
13Lakini watu wa kile kikosi, Amasia alichokirudisha, wasiende naye kupigana, waliingia miji ya Yuda toka Samaria hata Beti-Horoni, na kunyang'anya mali, wakapiga humo watu 3000, wakachukua mali nyingi, walizozinyang'anya.
14Amasia aliporudi akiisha kuwashinda Waedomu akaileta miungu ya wana wa Seiri, akaiweka kuwa miungu yake, akaiangukia na kuivukizia.
15Kwa hiyo Bwana akamkasirikia Amasia sana, akatuma mfumbuaji kwake, akamwambia: Mbona unaifuatafuata miungu ya watu hao, isiyowaponya watu wao mikononi mwako?
16Alipomwambia hayo, akamwuliza: Tumekuweka kula njama na mfalme? Yaache! Unatakiaje, wakupige? Ndipo, mfumbuaji alipoacha akisema: Ninajua sasa, ya kuwa Mungu anataka kukuangamiza, kwa sababu umefanya hivyo, usilisikie shauri langu.
17Kisha Amasia, mfalme wa Yuda, akapiga shauri, akatuma kwa Yoasi, mwana wa Yoahazi, mwana wa Yehu, mfalme wa Waisiraeli, kumwambia: Njoo, tuonane uso kwa uso!
18Naye Yoasi, mfalme wa Waisiraeli, akatuma kwa Amasia, mfalme wa Wayuda, kumwambia: Kingugi kilichoko Libanoni kilituma kwa mwangati ulioko Libanoni kwamba: Mpe mwanangu mtoto wako wa kike, awe mkewe! Ndipo, nyama wa porini wa huko Libanoni alipopita, akakikanyaga kile kingugi na kukiponda.[#Amu. 9:14.]
19Unasema, umewapiga Waedomu; kwa hiyo moyo wako unakukuza, ujitutumue. Sasa kaa nyumbani mwako! Mbona unataka kujitia katika vita vibaya, uanguke wewe na Wayuda pamoja na wewe?
20Lakini Amasia hakusikia, kwani jambo hilo limetoka kwa Mungu, awatie mikononi mwa wengine, kwa kuwa waliifuatafuata miungu ya Waedomu.
21Basi, Yoasi, mfalme wa Waisiraeli, akapanda, wakaonana uso kwa uso, yeye na Amasia, mfalme wa Wayuda, huko Beti-Semesi katika nchi ya Wayuda.
22Wayuda wakashindwa na Waisiraeli, wakakimbia kila mtu hemani kwake.
23Naye Yoasi, mfalme wa Waisiraeli, akamkamata Amasia, mfalme wa Yuda, aliyekuwa mwana wa Yoasi, mwana wa Yoahazi, kule Beti-Semesi, akampeleka Yerusalemu, akalivunja boma la Yerusalemu toka lango la Efuraimu hata lango la pembeni, ndio mikono 400.
24Akachukua dhahabu na fedha zote, navyo vyombo vyote vilivyopatikana Nyumbani mwa Mungu kwa Obedi-Edomu navyo vilimbiko vya nyumbani mwa mfalme nao watu, aliowataka kuwa kole, kisha akarudi Samaria.
25Ikawa, Yoasi, mwana wa Yoahazi, mfalme wa Isiraeli, alipokwisha kufa, Amasia, mwana wa Yoasi, mfalme wa Wayuda, akawapo tena miaka 15.
26Mambo mengine ya Amasia, ya mwanzo na ya mwisho, hatuyaoni, yameandikwa katika kitabu cha wafalme wa Wayuda na wa Waisiraeli?
27Tangu hapo, Amasia alipoacha kumfuata Bwana, walikuwako watu huko Yerusalemu waliomlia njama ya kumwua; kwa hiyo akakimbilia Lakisi, lakini wale wakatuma watu kumfuata lakisi, nao wakamwua huko.[#2 Mambo 24:25.]
28Wakamchukua kwa farasi, wakamzika kwa baba zake mjini mwa Yuda.