Yeremia 27

Yeremia 27

Yeremia anawaonya, wasikatae kumtumikia mfalme wa Babeli.

1Katika mwanzo wa ufalme wa Yoyakimu, mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda, neno hili likamjia Yeremia likitoka kwake Bwana kwamba:

2Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Jitengenezee kamba na kongwa, uzitie shingoni pako![#Yer. 13:1.]

3Kisha uzitume kwa mfalme wa Edomu na kwa mfalme wa Moabu na kwa Mfalme wa wana wa Amoni na kwa mfalme wa Tiro na kwa mfalme wa Sidoni, ukizitia mikononi mwa wajumbe wanaokuja Yerusalemu kwa Sedekia, mfalme wa Yuda![#Yer. 25:21-22.]

4Uwaagize, wawaambie mabwana wao kwamba: Hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi, Mungu wa Isiraeli, anavyosema, navyo ndivyo, mtakavyowaambia mabwana wenu:

5Mimi nilizifanya nchi na watu na nyama wa porini walioko katika nchi kwa nguvu yangu iliyo kuu na kwa mkono wangu uliokunjuka, nikampa anyokaye machoni pangu.

6Sasa mimi nimezitia nchi hizi zote mkononi mwa Nebukadinesari, mfalme wa Babeli, aliye mtumishi wangu; hata nyama wa porini nimempa, wamtumikie.[#Yer. 25:9.]

7Mataifa yote yatamtumikia yeye na mwanawe na mjukuu wake, mpaka zitakapotimia siku za nchi yake; ndipo, mataifa yenye watu wengi na wafalme wakuu watakapomtumikisha naye.[#Yer. 25:12.]

8Itakuwa, taifa au ufalme utakaokataa kumtumikia Nebukadinesari, mfalme wa Babeli, na kuzitia shingo zao katika makongwa ya mfalme wa Babeli, watu wa taifa hilo nitawapatiliza kwa panga na kwa njaa na kwa magonjwa mabaya.

9Kwa hiyo ninyi msiwasikie wafumbuaji wenu wala waaguaji wenu wala ndoto zenu wala waganga wenu wala watazamaji wenu wanaowaambia kwamba: Hamtamtumikia mfalme wa Babeli![#Yer. 14:13-14.]

10Kwani huwafumbulia yenye uwongo, kusudi wawatoe katika nchi yenu na kuwapeleka katika nchi ya mbali, nami niwatupe ninyi, mwangamie.

11Lakini watu wa taifa litakalotia shingo zao katika makongwa ya mfalme wa Babeli, wamtumikie, nitawatuliza katika nchi yao, wailime wakikaa kwao; ndivyo, asemavyo Bwana.

12Kisha nikamwambia Sedekia, mfalme wa Yuda, maneno haya yote ya kwamba: Zitieni shingo zenu katika makongwa ya mfalme wa Babeli, mmtumikie yeye na watu wake wote, mpate kukaa!

13Kwa sababu gani mnataka kufa, wewe nao walio ukoo wako, kwa panga na kwa njaa na kwa magonjwa mabaya, kama Bwana alivyosema kwa ajili ya taifa litakalokataa kumtumikia mfalme wa Babeli?

14Msiyasikie maneno ya wafumbuaji wanaowaambia kwamba: Msimtumikie mfalme wa Babeli! Kwani hao huwafumbulia yenye uwongo.[#Yer. 27:9.]

15Ndivyo, asemavyo Bwana: Sikuwatuma, nao hufumbua katika Jina langu yenye uwongo, kusudi niwatupe ninyi, mwangamie ninyi na wafumbuaji waliowafumbulia ninyi.

16Nao watambikaji na watu wote wa ukoo huu nikawaambia kwamba: Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Msiyasikie maneno ya wafumbuaji wenu wanaowafumbulia kwamba: Mtaona, vyombo vya Nyumba ya Bwana vikirudishwa toka Babeli sasa bado kidogo tu! Kwani hao huwafumbulia yenye uwongo.[#Yer. 28:3; 2 Mambo 36:10.]

17Msiwasikie! Ila mtumikieni mfalme wa Babeli, mpate kukaa! Kwa nini mji huu ugeuke kuwa mavunjiko?

18Kama ndio wafumbuaji, kama Neno la Bwana liko kwao, na wamwombe Bwana Mwenye vikosi, vyombo vilivyosalia katika Nyumba ya Bwana namo nyumbani mwa mfalme wa Yuda namo Yerusalemu visiende Babeli!

19Kwani hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema kwa ajili yao: Zile nguzo na bahari na vilingo na vyombo vyote vilivyosalia humu mjini,[#Yer. 52:17.]

20kweli Nebukadinesari, mfalme wa Babeli, hakuvichukua alipomhamisha Yekonia, mwana wa Yoyakimu, mfalme wa Yuda, toka Yerusalemu kwenda Babeli pamoja na wakuu wote wa Yuda na wa Yerusalemu;[#2 Fal. 24:14-15.]

21lakini hivi ndivyo, Bwana Mwenye vikosi, Mungu wa Isiraeli, anavyosema kwa ajili ya vyombo vilivyosalia Nyumbani mwa Bwana namo nyumbani mwa mfalme wa Yuda namo Yerusalemu:

22Vitapelekwa Babeli; ndiko, vitakakokuwa mpaka siku ile, nitakapowapatiliza; ndivyo, asemavyo Bwana. Ndipo, mtakapovileta huku na kuvirudisha mahali hapa.[#2 Mambo 36:22; Ezr. 1:7-11.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania