Yosua 7

Yosua 7

Wizi wa Akani unavumbuliwa.

1Wana wa Isiraeli wakakora manza kwa kuuvunja ule mwiko, kwani Akani, mwana wa Karmi, mwana wa Zabudi, mwana wa Zera wa shina la Yuda, akachukua vitu vyenye mwiko; ndipo, makali ya Bwana yalipowawakia wana wa Isiraeli.

2Kisha Yosua akatuma watu kutoka Yeriko kwenda Ai ulioko karibu ya Beti-Aweni, upande wa maawioni kwa jua wa Beteli, akawaambia kwamba: Pandeni kuipeleleza nchi hiyo! Nao wale watu wakapanda kupeleleza Ai.

3Waliporudi kwa Yosua wakamwambia: Wasiende watu wote kupanda huko! Watu kama 2000 au 3000 watatosha, waupige Ai. Usiwasumbue watu wote pia! Kwani wao ni wachache.

4Kisha walipopanda kama watu 3000 kwenda huko, wakawakimbia watu wa Ai,

5nao watu wa Ai wakaua kwao kama 36, wakawakimbiza kuanzia kwenye lango la mji mpaka kufika Sebarimu, wakawaua huko penye mtelemko; ndipo, mioyo ya watu ilipoyeyuka kuwa kama maji.

6Naye Yosua akazirarua nguo zake, akajiangusha chini kifudifudi mbele ya Sanduku la Bwana mpaka jioni, yeye na wazee wa Waisiraeli, wakitia mavumbi vichwani pao.

7Kisha Yosua akaomba: Wewe Bwana Mungu, kwa nini umewavukisha watu hawa Yordani, ukitutia mikononi mwa Waamori, watuangamize? Ingetufaa sana kukaa ng'ambo ya huko ya Yordani!

8E Bwana! Nisemeje, kwa kuwa Waisiraeli wamewapa adui zao visogo?

9Wakanaani na wenyeji wote wa nchi hii watakapovisikia, watatuzunguka, walitoweshe jina letu katika nchi hii. Nawe utafanya nini kwa ajili ya Jina lako kuu?[#2 Mose 32:12.]

10Ndipo, Bwana alipomwambia Yosua; Inuka! Ni kwa sababu gani, ukianguka usoni pako?

11Waisiraeli wamekosa wasipolishika agano langu, nililowaagiza, kwa maana wamechukua vitu vyenye mwiko kwa kuviiba, wakavificha na kuvitia katika vyombo vyao.

12Kwa hiyo wana wa Isiraeli hawakuweza kusimama machoni pa adui zao, hawakuwa na budi kuwapa hao adui zao visogo, kwani wamejipatia kiapizo. Mimi sitaendelea kuwa nanyi, msipokitowesha hicho kiapizo katikati yenu.

13Inuka, uwaeue hawa watu na kuwaambia: Jieulieni siku ya kesho! Kwani hivyo ndivyo, Bwana Mungu wa Isiraeli anavyosema: Kiko kiapizo kilichoko katikati yenu, Waisiraeli; kwa hiyo hamtaweza kusimama machoni pa adui zenu, mpaka mkiondoe hicho kiapizo katikati yenu.[#Yos. 3:5.]

14Kesho asubuhi sharti mjilete hapa shina kwa shina, nalo shina, Bwana atakalolikamata, litajileta ukoo kwa ukoo, nao ukoo, Bwana atakaoukamata, utajileta mlango kwa mlango, nao mlango, Bwana atakaokamata, watu wake watajileta mmoja mmoja.

15Naye atakayekamatwa kuwa mwenye kiapizo atateketezwa kwa moto pamoja navyo vyote, alivyo navyo, kwa kuwa hakulishika agano la Bwana na kuwafanyizia Waisiraeli upumbavu.

16Kesho yake Yosua akaamka na mapema; naye alipowaleta Waisiraeli shina kwa shina, likakamatwa shina la Yuda.[#1 Sam. 10:20-21; 14:41-42.]

17Alipozileta koo za Yuda, akaukamata ukoo wa Wazera; alipouleta ukoo wa Wazera mmoja mmoja, Zabudi akakamatwa.[#4 Mose 26:20.]

18Alipouleta mlango wake mmoja mmoja, akakamatwa Akani, mwana wa Karmi, mwana wa Zabudi, mwana wa Zera wa shina la Yuda.

19Ndipo, Yosua alipomwambia Akani: Manangu, mche Bwana Mungu wa Isiraeli na kumtukuza, ukimwungamia waziwazi! Nielezee uliyoyafanya, usiyafiche!

20Akani akamjibu Yosua na kumwambia: Kweli, mimi nimemkosea Bwana Mungu wa Isiraeli nikifanya hivi na hivi.

21Nilipoona katika nyara vazi zuri la Babeli na fedha 200 na ulimi mmoja wa dhahabu wenye uzito wa sekeli 50, ndio ratli mbili, nikaingiwa na tamaa navyo, nikavichukua, viko hemani mwangu, vimefukiwa mchangani, nazo fedha ziko chini yao.

22Yosua akatuma wajumbe, wakapiga mbio kwenda hemani, wakaviona, vimefichwa hemani mwake, nazo fedha zilikuwa chini yao.

23Wakavichukua mle hemani, wakavipeleka kwa Yosua, wana wote wa Isiraeli walikokuwa, wakaviweka huko mbele yake Bwana.

Akani anauawa.

24Kisha Yosua akamchukua Akani, mwana ma Zera, pamoja na zile fedha na lile vazi na ule ulimi wa dhahabu, hata wanawe wa kiume na wa kike, na ng'ombe wake na punda wake na mbuzi na kondoo wake na hema lake navyo vyote vilivyokuwa vyake, nao Waisiraeli wote wakaenda naye, wakawapeleka wote katikati ya bonde la Akori.

25Huko Yosua akasema: Kama ulivyotupatia mabaya, ndivyo Bwana akupatie mabaya nawe siku hii ya leo! Ndipo, Waisiraeli wote walipompiga mawe, navyo vile vitu wakavichoma moto, nao wale watu wakawaua kwa kuwapiga mawe.

26Kisha wakakusanya juu yake chungu kubwa la mawe lililoko mpaka siku hii ya leo. Ndipo, Bwana alipoyaacha makali yake yenye moto. Kwa hiyo wakaliita jina lake mahali pale Bonde la Akori (Bonde la Mabaya) mpaka siku hii ya leo.[#Yes. 65:10; Hos. 2:15.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania