Malaki 2

Malaki 2

Watambikaji wanaonywa.

1Sasa ninyi watambikaji, agizo hili mnatolewa ninyi.[#5 Mose 28:15.]

2Ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema: Msiposikia, wala msipoyatia mioyoni mwenu, mlipe Jina langu macheo, ndipo, nitakapowaapiza ninyi, nazo mbaraka zenu nitazigeuza kuwa maapizo; hata sasa nimekwisha kuzigeuza kuwa maapizo, kwani ninyi hamyatii haya mioyoni mwenu.

3Mtaniona, nikiyakemea mazao yenu ninyi, nikiwatupia mavi usoni penu, na yale mavi ya ng'ombe za tambiko za sikukuu zenu, nao watu watawachukua ninyi, wawapeleke penye hayo mavi.

4Ndipo, mtakapojua, ya kuwa nimewatolea agizo hili, liwe agano langu, nitakalolifanya na Lawi; ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema.

5Agano langu, nililolifanya naye, lilikuwa la kumpatia uzima na utengemano; naye ndiye, niliyempa, aniogope; akaniogopa kweli, akajinyenyekeza mbele ya Jina langu.

6Maonyo ya kweli yalikuwa kinywani mwake, lakini uovu haukuonekana midomoni mwake, akendelea kufuatana na mimi kwa utengemano na kwa unyofu, akarudisha wengi, wasiufuate uovu.

7Kwani midomo ya mtambikaji sharti iangalie yaliyo yenye ujuzi, nayo Maonyo ndiyo, watu wanayoyatafuta kinywani mwake, kwani yeye ni mjumbe wa Bwana Mwenye vikosi.[#5 Mose 33:10; Hag. 1:13.]

8Lakini ninyi mmeiacha njia hiyo, mkakwaza wengi, wasiyashike Maonyo, mkalivunja agano, nililolifanya na Lawi; ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema.

9Kwa hiyo mimi nami nimewatoa ninyi, mbezwe nao wote walio wa ukoo huu na kunyenyekezwa vivyo hivyo, kama ninyi mlivyokataa kuzishika njia zangu, mkawapendelea watu mlipowafundisha Maonyo.

Kuoa wanawake wa kimizimu ni kubaya.

10Je? Sisi sote baba yetu si mmoja? Kumbe aliyetuumba si yeye Mungu mmoja? Mbona tunaendeana kwa udanganyifu kila mtu na ndugu yake, tulipatie uchafu agano la baba zetu?[#Mal. 1:6; Iy. 31:15.]

11Wayuda ni wadanganyifu, yafanyikayo kwao Waisiraeli namo Yerusalemu ni matendo yatapishayo, kwani Wayuda wamepachafua Patakatifu pa Bwana, anapopapenda, walipooa wanawake wa mungu mgeni.[#Ezr. 9:2.]

12Mtu afanyaye hayo Bwana na amwangamize mahemani mwa Yakobo, mfunzi na mwanafunzi naye ampelekeaye Bwana Mwenye vikosi vipaji vya tambiko!

13Tena hili ni la pili mnalolifanya: meza ya kumtambikia Bwana mnaifunika kwa machozi yao wamliliao na kupiga kite, asitazame tena kipaji cho chote cha tambiko, wala asipokee mikononi mwenu cho chote cha kumpendeza.[#Mal. 1:10.]

14Nanyi mnauliza: Kwa sababu gani? Ni kwa sababu Bwana ni shahidi wako na shahidi wa mkeo wa ujana wako, uliyemwacha wewe kwa kumdanganya, naye alikuwa mwenzako wa kabila na mke wako wa kuagana naye.

15Hakuna mtu hata mmoja anayeweza kufanya hayo akiwa analo bado sao la kiroho. Naye yule mmoja alifanya nini? Alitafuta mzao wa Mungu! Kwa hiyo jiangalieni rohoni mwenu, msiwadanganye wake zenu wa ujana wenu![#Yes. 51:2; Ez. 33:24; 1 Mose 15:5-6; 21:12.]

16Kwani Bwana Mungu wa Isiraeli anasema: Ninachukia kuachana, maana ni kuyafunika mavazi yao kwa ukorofi; ndivyo, anavyosema Bwana Mwenye vikosi; kwa hiyo jiangalieni rohoni mwenu, msidanganye![#5 Mose 24:1.]

17Mmemchokesha Bwana kwa maneno yenu, mkiuliza: Tumemchokesha kwa nini? Ni kwa kusema kwenu; kila afanyaye mabaya ni mwema machoni pa Bwana, nao walio hivyo ndio, anaopendezwa nao! Au mkiuliza: Yuko wapi Mungu anayepatiliza?[#Mal. 3:13-14.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania