The chat will start when you send the first message.
1*Mtu huyatengeneza mambo ya moyo,
lakini Bwana huyapa, ulimi unayoyajibu.
2Njia zote za mtu hutakata machoni pake,
lakini Bwana huzijaribu roho.
3Mtupie Bwana yote utakayoyafanya!
Ndivyo, mawazo yako yatakavyotimia.
4Bwana aliyaumba yote kulitimiza neno, alitakalo,
hata yeye asiyemcha alimwumbia kuiona siku mbaya.
5Wote wajikuzao mioyoni mwao humtapisha Bwana,
ingawa wapeane mikono, hawana budi hupatilizwa.
6Manza huondolewa kwa huruma na kwa welekevu,
kwa kumcha Bwana mtu huepuka penye mabaya.
7Njia za mtu zikimpendeza Bwana,
hupatanisha naye hata wachukivu wake.
8Machache yapatikanayo kwa wongofu ni mema
kuliko mapato mengi yapatikanayo kwa njia zisizo sawa.
9Moyo wa mtu hujiwazia njia zake,
lakini Bwana ndiye anayeiendesha miguu yake.*
10Midomo ya mfalme inayoyasema ni fumbo,
kwa kukata shauri kinywa chake hakidanganyi.
11Mizani na vipimo vya kweli hujua Bwana,
vijiwe vyote vya kupimia vilivyomo mifukoni ni kazi zake.
12Kufanya maovu hutapisha wafalme,
kwani kiti cha kifalme hupata nguvu kwa wongofu.
13Midomo isemayo yaongokayo hupendeza wafalme,
nao wasemao yanyokayo huwapenda.
14Makali ya mfalme hufanana na wajumbe wa kifo,
lakini mtu mwerevu wa kweli huyatuliza.
15Uso wa mfalme ukiangaza hupatia watu uzima,
akipendezwa hufanana na wingu lenye mvua ya masika.
16Kupata werevu wa kweli ni kwema kuliko kupata dhahabu,
kupata utambuzi hufaa zaidi kukuchagua kuliko kupata fedha.
17Mwenendo wao wanyokao huepuka penye mabaya,
aiangaliaye roho yake huilinda njia yake.
18Majivuno hufuatwa na kuanguka,
nako kujikuza rohoni hufuatwa na kujikwaa.
19Kujinyenyekeza pamoja nao wanyonge ni kwema
kuliko kugawanya mapokonyo pamoja nao wajivunao.
20Aliangaliaye Neno huona mema,
naye amwegemeaye Bwana ni mwenye shangwe.
21Mwenye moyo uerevukao kweli huitwa mtambuzi,
midomo isemayo maneno matamu huendesha mafunzo.
22Kutumia akili humpatia mwenyewe kisima cha uzima,
lakini mapigo ya wajinga huwapatia ujinga tu.
23Moyo wa mwerevu wa kweli hukifundisha kinywa chake,
nayo midomo yake huendesha mafunzo.
24Maneno yapendezayo ni asali iliyo nzuri yenyewe,
roho huyaona kuwa matamu, nayo mifupa hupata uzima mumo humo.
25Ziko njia zinyokazo machoni pa mtu,
lakini mwisho hujulika kuwa njia za kwenda kufani.
26Roho ya msumbufu hujisumbukia,
kwani kinywa chake humlemea.
27Mtu asiyefaa kitu huchimbua mabaya,
nayo maneno ya midomo yake hufanana na moto uunguzao.
28Mtu mpotovu huzusha magomvi,
msingiziaji hutenganisha watu waliopendana.
29Mtu mkorofi humpoteza mwenziwe
akimwongoza katika njia isiyo njema.
30Ayafumbaye macho yake huwaza mapotovu,
akazaye kuifunga madomo yake amikwisha kutunga mabaya.
31Mvi ni kilemba chenye utukufu,
huonekana katika njia ya wongofu.
32Uvumilivu ni mwema kuliko ufundi wa vita,
ajitawalaye moyoni mwake ni mwema kuliko atekaye miji.
33Kura hupigwa katika mikunjo ya nguo,
lakini mashuri yote hukatwa na Bwana.