Zekaria 10

Matengenezo ya Yuda na Israeli

1Mwombeni BWANA mvua wakati wa masika, naam, BWANA aletaye mawingu ya mvua, naye atawapa manyunyu ya mvua, kila mtu atapewa nyasi shambani.[#Yer 14:22; Yoe 2:23]

2Kwa maana vinyago vimenena maneno ya ubatili, nao waaguzi wameona uongo; nao wameleta habari za ndoto za uongo, wafariji bure; kwa sababu hiyo watu wanatangatanga kama kondoo, wanateseka kwa kukosa mchungaji.[#Mt 9:36; Mk 6:34]

3Hasira yangu imewaka juu ya wachungaji, nami nitawaadhibu viongozi; kwa maana BWANA wa majeshi ameliangalia kundi lake, yaani, nyumba ya Yuda, naye atawafanya kuwa kama farasi wake mzuri vitani.[#Kut 4:31; Rut 1:6; Sef 2:7; Lk 1:68; 1 Pet 2:12; #10:3 Katika Kiebrania ni beberu.]

4Kwake yeye litatoka lile jiwe la pembeni, kwake yeye utatoka msumari, kwake yeye utatoka upinde wa vita, kwake yeye atatoka kila kamanda.[#Isa 22:23]

5Nao watakuwa kama mashujaa, wakanyagao adui zao katika matope ya njia vitani; nao watapiga vita, kwa sababu BWANA yu pamoja nao; na hao wapandao farasi watafadhaishwa.

6Nami nitaitia nguvu nyumba ya Yuda, nami nitaiokoa nyumba ya Yusufu, nami nitawarudisha, kwa maana nawaonea rehema; nao watakuwa kana kwamba sikuwatupa; kwa maana mimi ni BWANA, Mungu wao, nami nitawasikia.

7Na watu wa Efraimu watakuwa kama shujaa, na moyo wao utafurahi kana kwamba ni kwa divai; naam, watoto wao wataona mambo haya, na kufurahi; mioyo yao itamfurahia BWANA.

8Nitawapigia kelele, na kuwakusanya pamoja; kwa maana nimewakomboa; nao wataongezeka kama walivyokua hapo awali.[#Isa 5:26]

9Nami nitawapanda kama mbegu kati ya mataifa; nao watanikumbuka katika nchi zilizo mbali; nao watakaa pamoja na watoto wao; tena watarudi.

10Tena nitawarudisha toka nchi ya Misri, nitawakusanya na kuwatoa katika Ashuru; nami nitawaingiza katika nchi ya Gileadi na Lebanoni; hata pasiwe na nafasi ya kuwatosha.[#Rum 11:25; Kut 14:26,27; Isa 49:20]

11Naye atapita kati ya bahari ya mateso, na kuyapiga mawimbi ya bahari, na vilindi vyote vya mto Nile vitakauka; na kiburi cha Ashuru kitashushwa; na fimbo ya enzi ya Misri itatoweka.[#Eze 30:13]

12Nami nitawatia nguvu katika BWANA; nao watatembea huku na huko katika jina lake, asema BWANA.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya