The chat will start when you send the first message.
1Nzi waliokufa hufanya manukato ya mwuza marashi kutoa uvundo;
Kadhalika upumbavu haba ni mzito kuliko hekima na heshima.
2Moyo wake mwenye hekima upo upande wa kulia;[#Mt 6:33; Kol 3:1]
Bali moyo wake mpumbavu upo mkono wa kushoto.
3Naam, huyo mpumbavu tena, aendapo njiani, hupungukiwa na fahamu zake; hata humwambia kila mtu ya kuwa yeye ni mpumbavu.[#Mit 13:16]
4Roho yake mtawala ikiinuka kinyume chako,[#Mhu 8:3; 1 Sam 25:24; Mit 25:15]
Usiondoke mara mahali pako ulipo;
Kwa maana roho ya upole hutuliza machukizo yaliyo makubwa.
5Liko baa nililoliona chini ya jua, nalo ni kama kosa litokalo kwake yeye atawalaye;
6ya kuwa upumbavu huwekwa mahali pa juu sana, nao wakwasi hukaa mahali pa chini.
7Mimi nimeona watumwa wamepanda farasi, na wakuu wakienda kwa miguu juu ya nchi kama watumwa.[#Mit 19:10]
8Mwenye kuchimba shimo atatumbukia ndani yake;[#Zab 7:15; Mit 26:27]
Na yeye abomoaye boma, nyoka atamwuma.
9Mwenye kuchonga mawe ataumizwa kwayo;
Naye apasuaye miti huona hatari katika hiyo.
10Iwapo chuma hakipati, wala mtu hakinoi;
Ndipo hana budi kutumia nguvu zaidi. Lakini yafaa kutumia hekima, na kufanikiwa.
11Nyoka akiuma kabla hajachezeshwa,[#Yer 8:17]
Basi hakuna faida ya mchezeshaji.
12Maneno ya kinywa chake mwenye hekima yana neema;
Bali midomo ya mpumbavu itammeza nafsi yake.
13Mwanzo wa maneno ya kinywa chake ni upuuzi; na mwisho wa usemi wake ni wazimu wenye hatari.
14Tena, upumbavu huongeza maneno; lakini mwanadamu hajui yatakayokuwako; nayo yatakayokuwa baada yake, ni nani awezaye kumweleza?[#Yak 4:14]
15Kazi yao wapumbavu huwachosha kila mmoja,
Maana hajui hata njia ya kuuendea mji.
16Ole wako, nchi, iwapo mfalme wako ni kijana,[#Isa 3:4]
Na wakuu wako hula asubuhi!
17Heri kwako, nchi, mfalme wako akiwa mtoto wa watu,[#Mit 31:4]
Na wakuu wako hula wakati ufaao, Ili makusudi wapate nguvu, wala si kwa ajili ya ulevi.
18Kwa sababu ya uvivu paa hunepa;
Na kwa ulegevu wa mikono nyumba huvuja.
19Karamu hufanywa kwa ajili ya kicheko,
Na divai huyafurahisha maisha; Na fedha huleta jawabu la mambo yote.
20Usimlaani mfalme, la, hata katika wazo lako;[#Kut 22:28]
Wala usiwalaani wakwasi chumbani mwako;
Kwa kuwa ndege wa anga ataichukua sauti,
Na mwenye mabawa ataitoa habari.