Waraka kwa Waebrania 2

Waraka kwa Waebrania 2

Onyo kuhusu kuwa makini

1Kwa hiyo imetupasa kuyaangalia zaidi hayo tuliyoyasikia tusije tukayakosa.

2Kwa maana, ikiwa lile neno lililonenwa na malaika lilikuwa imara, na kila kosa na uasi ulipata ujira wa haki,[#Mdo 7:38,53; Gal 3:19]

3sisi je! Tutapataje kupona, tukipuuza wokovu mkuu namna hii? Ambao kwanza ulinenwa na Bwana, kisha ukathibitika kwetu na wale waliomsikia;[#Ebr 10:29; 12:25]

4Mungu naye akishuhudia pamoja nao kwa ishara na ajabu na nguvu za namna nyingi, na kwa karama za Roho Mtakatifu, kama alivyopenda mwenyewe.[#Mk 16:20; 1 Kor 12:4,11]

Kutukuka kwa kujishusha

5Maana hakuuweka chini ya malaika ulimwengu ule ujao tunaounena, ila mtu mmoja ameshuhudia hivi mahali fulani, akisema,

6Mwanadamu ni nini hata umkumbuke,[#Zab 8:4-6]

Ama mwana wa binadamu, hata umwangalie?

7Umemfanya mdogo kwa muda kuliko malaika,

Umemvika taji la utukufu na heshima,

Umemtawaza juu ya kazi za mikono yako;

8Umeweka vitu vyote chini ya nyayo zake.[#1 Kor 15:27]

Kwa maana katika kuweka vitu vyote chini yake hakubakiza kitu kisichowekwa chini yake. Lakini sasa bado hamjaona vitu vyote kutiwa chini yake,

9ila twamwona yeye aliyefanywa mdogo kwa muda kuliko malaika, yaani, Yesu, kwa sababu ya maumivu ya mauti, amevikwa taji la utukufu na heshima, ili kwa neema ya Mungu aionje mauti kwa ajili ya kila mtu.[#Flp 2:8,9]

10Kwa kuwa ilimpasa yeye, ambaye kwa ajili yake na kwa njia yake vitu vyote vimekuwapo, akileta wana wengi waufikie utukufu, kumkamilisha kiongozi mkuu wa wokovu wao kwa njia ya mateso.[#Rum 11:36]

11Maana yeye atakasaye na hao wanaotakaswa wote pia watoka kwa mmoja. Kwa ajili hii haoni haya kuwaita ndugu zake;[#Mk 3:34,35; Mt 25:40; Yn 20:17]

12akisema,[#Zab 22:22]

Nitalihubiri jina lako kwa ndugu zangu;

Katikati ya kanisa nitakuimbia sifa.

13Na tena,[#Isa 8:17,18; 2 Sam 22:3]

Nitakuwa nimemtumaini yeye.

Na tena,

Tazama, mimi nipo hapa na watoto niliopewa na Mungu.

14Basi, kwa kuwa watoto wameshiriki damu na mwili, yeye naye vivyo hivyo alishiriki yayo hayo, ili kwa njia ya mauti amharibu yeye aliyekuwa na nguvu za mauti, yaani, Ibilisi,[#2 Tim 1:10; Yn 12:31; Ufu 12:10; 1 Kor 15:56]

15awaache huru wale ambao katika maisha yao yote kwa hofu ya mauti walikuwa katika hali ya utumwa.

16Maana ni hakika, hatwai asili ya malaika, ila atwaa asili ya mzao wa Abrahamu.[#Isa 41:8,9]

17Hivyo ilimpasa kufananishwa na ndugu zake katika mambo yote, apate kuwa kuhani mkuu mwenye rehema, mwaminifu katika mambo ya Mungu, ili afanye kafara ya suluhu kwa dhambi za watu wake.[#Zab 22:22; Flp 2:7]

18Na kwa kuwa mwenyewe aliteswa alipojaribiwa, aweza kuwasaidia wao wanaojaribiwa.[#Ebr 4:15]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya