The chat will start when you send the first message.
1Na baada ya siku sita Yesu akawatwaa Petro, na Yakobo, na Yohana nduguye, akawaleta juu ya mlima mrefu faraghani;[#2 Pet 1:17-18]
2akageuka sura yake mbele yao; uso wake ukang'aa kama jua, mavazi yake yakawa meupe kama nuru.[#2 Pet 1:16-18]
3Na tazama, wakatokewa na Musa na Eliya, wakizungumza naye.
4Petro akajibu akamwambia Yesu, Bwana, ni vizuri sisi kuwapo hapa; ukitaka, nitafanya hapa vibanda vitatu, kimoja chako wewe, na kimoja cha Musa, na kimoja cha Eliya.
5Alipokuwa bado akisema, tazama, wingu jeupe likawatia uvuli; na tazama, sauti ikatoka katika lile wingu, ikasema, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye; msikieni yeye.[#Mwa 22:2; Kum 18:15; Zab 2:7; Isa 42:1; Mt 3:17; 12:18; Mk 1:11; Lk 3:22]
6Na wale wanafunzi waliposikia, walianguka kifudifudi na kuogopa sana.
7Yesu akaja, akawagusa, akasema, Inukeni, wala msiogope.
8Wakainua macho yao, wasione mtu ila Yesu peke yake.
9Na walipokuwa wakishuka mlimani, Yesu aliwaagiza, akasema, Msimwambie mtu yeyote habari ya maono hayo, hadi Mwana wa Adamu atakapofufuka katika wafu.[#Mt 16:20]
10Wanafunzi wake wakamwuliza, wakisema, Basi kwa nini waandishi hunena ya kwamba imempasa Eliya kuja kwanza?[#Mal 4:5; Mt 11:14]
11Naye akajibu, akawaambia, Kweli Eliya yuaja kwanza, naye atatengeneza yote,
12ila nawaambia, ya kwamba Eliya amekwisha kuja, wasimtambue, lakini wakamtenda yote waliyotaka. Vivyo hivyo Mwana wa Adamu naye yuaenda kuteswa kwao.[#Mt 11:14; 14:9,10]
13Ndipo wale wanafunzi walipofahamu ya kuwa amesema nao habari za Yohana Mbatizaji.[#Lk 1:17]
14Nao walipoufikia mkutano, mtu mmoja akamjia, akampigia magoti, akisema,[#Mk 9:14-29; Lk 9:37-42]
15Bwana, umrehemu mwanangu, kwa kuwa ana kifafa, na kuteswa vibaya; maana mara nyingi huanguka motoni, na mara nyingi majini.
16Nilimleta kwa wanafunzi wako, wasiweze kumponya.
17Yesu akajibu, akasema, Enyi kizazi kisichoamini, kilichopotoka, nitakaa pamoja nanyi hadi lini? Nitachukuliana nanyi hadi lini? Mleteni huku kwangu.[#Kum 32:5; Yn 14:9]
18Yesu akamkemea pepo, naye akamtoka; yule mvulana akapona tangu saa ile.
19Kisha wale wanafunzi wakamwendea Yesu kwa faragha wakasema Mbona sisi hatukuweza kumtoa?[#Mt 10:1]
20Yesu akawaambia, Kwa sababu ya upungufu wa imani yenu. Kwa maana, amin, nawaambia, Mkiwa na imani kiasi cha punje ya haradali mtauambia mlima huu, Ondoka hapa uende kule; nao utaondoka; wala halitakuwako neno lisilowezekana kwenu. [[#Mt 21:21; Mk 11:23; 1 Kor 13:2; Lk 17:6]
21Lakini namna hii haitoki ila kwa kusali na kufunga.]
22Nao walipokuwa wakikaa Galilaya, Yesu akawaambia, Mwana wa Adamu anakwenda kutiwa katika mikono ya watu, nao watamwua, na siku ya tatu atafufuka.[#Mk 9:30-32; Lk 9:43-45; #Mt 16:21]
23Wakasikitika sana.
24Na walipofika Kapernaumu, wale watozao nusu-shekeli walimwendea Petro, wakasema, Je! Mwalimu wenu hatoi ushuru wa hekalu? Akasema, Hutoa.[#Kut 30:13; 38:26; #17:24 yaani nusu shekeli.]
25Naye alipoingia nyumbani, Yesu alitangulia kumwuliza, akisema, Waonaje, Simoni? Wafalme wa dunia hutwaa kodi ama ushuru kwa watu gani? Kwa wana wao au kwa wageni?
26Naye aliposema, Kwa wageni, Yesu alimwambia, Basi, kama ni hivyo, wana wako huru.
27Lakini tusije tukawakwaza, nenda baharini ukatupe ndoana, ukatwae samaki yule azukaye kwanza; na ukifumbua mdomo wake utaona shekeli; ichukue hiyo ukawape kwa ajili yangu na kwa ajili yako.[#17:27 Shekeli moja ni kama shilingi 3.]