Mathayo 18

Mathayo 18

Ukuu wa kweli

1Saa ile wanafunzi wakamwendea Yesu wakisema,[#Lk 22:24; #Mk 9:33-47; Lk 9:46-48]

2Ni nani basi aliye mkuu katika ufalme wa mbinguni? Akaita mtoto mmoja, akamweka katikati yao,

3akasema, Amin, nawaambia, Msipoongoka na kuwa kama watoto, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni.[#Mk 10:15; Lk 18:17; Mt 19:14; Yn 3:3-5]

Majaribu ya dhambi

4Basi, yeyote ajinyenyekezaye mwenyewe kama mtoto huyu, huyo ndiye aliye mkuu katika ufalme wa mbinguni.

5Na yeyote atakayempokea mtoto mmoja mfano wa huyu kwa jina langu, anipokea mimi;[#Mt 10:40; Yn 13:20]

6bali atakayemkosesha mmojawapo wa wadogo hawa waniaminio, yamfaa afungiwe shingoni jiwe kubwa la kusagia, na kutoswa katika kilindi cha bahari.[#Lk 17:1,2]

7Ole ni wa ulimwengu kwa sababu ya mambo ya kukosesha! Maana hayana budi kuja mambo ya kukosesha; lakini ole wake mtu yule aliletaye jambo la kukosesha!

8Basi mkono wako au mguu wako ukikukosesha, ukate ukautupe mbali nawe; ni afadhali kuingia katika uzima ukiwa umepungukiwa na mkono au mguu, kuliko kuwa na mikono miwili au miguu miwili, na kutupwa katika moto wa milele.[#Mt 5:29,30]

9Na jicho lako likikukosesha, ling'oe, ukalitupe mbali nawe; ni afadhali kuingia katika uzima ukiwa na chongo, kuliko kuwa na macho mawili, na kutupwa katika Jehanamu ya moto.[#Mt 5:29]

Mfano wa kondoo aliyepotea

10Angalieni msidharau mmojawapo wa wadogo hawa; kwa maana nawaambia ya kwamba malaika wao mbinguni siku zote huutazama uso wa Baba yangu aliye mbinguni. [[#Ebr 1:14]

11Kwa maana Mwana wa Adamu alikuja kukiokoa kilichopotea.][#Lk 19:10]

12Mwaonaje? Mtu akiwa na kondoo mia, mmoja akampotea, je! Hawaachi wale tisini na tisa, akaenda milimani, na kumtafuta yule aliyepotea?[#Lk 15:4-7]

13Hata akipata kumwona, amin, nawaambia, amfurahia huyo zaidi, kuliko wale tisini na tisa wasiopotea.

14Vivyo hivyo haipendezi mbele za Baba yenu aliye mbinguni kwamba mmoja wa wadogo hawa apotee.

Kumwonya anayekukosea

15Na ndugu yako akikukosea, nenda ukamwonye, wewe na yeye peke yenu; akikusikia, umempata nduguyo.[#Lk 17:3; Law 19:17; Gal 6:1]

16La, kama hasikii, chukua pamoja nawe tena mtu mmoja au wawili, ili kwa vinywa vya mashahidi wawili au watatu kila neno lithibitike.[#Kum 19:15]

17Na asipowasikiliza wao, liambie kanisa; na asipolisikiliza kanisa pia, na awe kwako kama mtu wa mataifa na mtoza ushuru.[#1 Kor 5:13]

18Amin, nawaambieni, yoyote mtakayoyafunga duniani yatakuwa yamefungwa mbinguni; na yoyote mtakayoyafungua duniani yatakuwa yamefunguliwa mbinguni.[#Mt 16:19; Yn 20:23]

19Tena nawaambia, ya kwamba wawili wenu watakapopatana duniani katika jambo lolote watakaloliomba, watafanyiwa na Baba yangu aliye mbinguni.[#Mk 11:24]

20Kwa kuwa walipo wawili watatu wamekusanyika kwa jina langu, nami nipo papo hapo katikati yao.[#Mt 28:20; Yn 14:23]

Kusameheana

21Kisha Petro akamwendea akamwambia, Bwana, ndugu yangu anikosee mara ngapi nami nimsamehe? Hata mara saba?[#Lk 17:3-4]

22Yesu akamwambia, Sikuambii hata mara saba, bali hata saba mara sabini.

Mfano wa mtumishi asiyesamehe

23Kwa sababu hii ufalme wa mbinguni umefanana na mfalme mmoja aliyetaka kufanya hesabu na watumwa wake.

24Alipoanza kuifanya, aliletewa mtu mmoja mwenye deni la talanta elfu kumi.[#18:24 Talanta moja ni kama shilingi 5,000.]

25Naye alipokosa cha kulipa, bwana wake akaamuru auzwe, yeye na mkewe na watoto wake, na vitu vyote alivyokuwa navyo, ikalipwe ile deni.

26Basi yule mtumwa akaanguka, akamsujudia akisema, Bwana, nivumilie, nami nitakulipa yote pia.

27Bwana wa mtumwa yule akamhurumia, akamfungua, akamsamehe ile deni.

28Mtumwa yule akatoka, akamwona mmoja wa watumishi wake, aliyemwia dinari mia; akamkamata, akamkaba koo, akisema, Nilipe unachodaiwa.[#18:28 Dinari moja ni kama senti 75.]

29Basi mtumwa mwenzake akaanguka miguuni pake, akamsihi, akisema, Nivumilie, nami nitakulipa yote pia.

30Lakini hakutaka, akaenda, akamtupa gerezani, hadi atakapoilipa ile deni.

31Basi watumwa wenzake walipoyaona yaliyotendeka, walisikitika sana, wakaenda wakamweleza bwana wao yote yaliyotendeka.

32Ndipo bwana wake akamwita, akamwambia, Ewe mtumwa mwovu, nilikusamehe wewe deni ile yote, uliponisihi;

33nawe, je! Haikukupasa kumrehemu mtumwa mwenzako, kama mimi nilivyokurehemu wewe?

34Bwana wake akaghadhibika, akampeleka kwa watesaji, hata atakapoilipa deni ile yote.[#Mt 5:26]

35Ndivyo na Baba yangu wa mbinguni atakavyowatenda ninyi, msiposamehe kwa mioyo yenu kila mtu ndugu yake.[#Mt 6:14,15]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya