Mathayo 5

Mathayo 5

Sifa na heri

1Naye alipowaona makundi ya watu, alipanda mlimani; na alipokwisha kuketi, wanafunzi wake walimjia;[#Lk 6:20-49]

2akafumbua kinywa chake, akawafundisha, akisema,

3Heri walio maskini wa roho;[#Isa 57:15]

Maana ufalme wa mbinguni ni wao.

4Heri wenye huzuni;[#Isa 61:2; Zab 126:5; Ufu 7:17]

Maana hao watafarijika.

5Heri wenye upole;[#Zab 37:11]

Maana hao watairithi nchi.

6Heri wenye njaa na kiu ya haki;[#Isa 55:1-2]

Maana hao watashibishwa.

7Heri wenye rehema;[#Yak 2:13]

Maana hao watapata rehema.

8Heri wenye moyo safi;[#Zab 24:3-4; 51:10; 73:1; 1 Yoh 3:2,3]

Maana hao watamwona Mungu.

9Heri wapatanishi;[#Ebr 12:4]

Maana hao wataitwa wana wa Mungu.

10Heri wenye kuudhiwa kwa ajili ya haki;[#1 Pet 3:14]

Maana ufalme wa mbinguni ni wao.

11Heri ninyi watakapowashutumu na kuwaudhi na kuwanenea kila neno baya kwa uongo, kwa ajili yangu.[#1 Pet 4:14]

12Furahini, na kushangilia; kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa mbinguni; kwa maana ndivyo walivyowaudhi manabii waliokuwa kabla yenu.[#2 Nya 36:16; Mdo 7:52; Yak 5:10; Ebr 11:33-38]

Chumvi na nuru

13Ninyi ni chumvi ya dunia; lakini chumvi ikipoteza ladha yake, ladha hiyo itarudishwa vipi? Haifai tena kabisa, ila kutupwa nje na kukanyagwa na watu.[#Mk 9:50; Lk 14:34-35]

14Ninyi ni nuru ya ulimwengu. Mji ukiwa juu ya mlima hauwezi kusitirika.[#Yn 8:12; 9:5]

15Wala watu hawawashi taa na kuiweka chini ya pishi, bali juu ya kiango; nayo yawaangaza wote waliomo nyumbani.[#Mk 4:21; Lk 8:16; 11:33]

16Vivyo hivyo nuru yenu na iangaze mbele ya watu, wapate kuyaona matendo yenu mema, wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni.[#1 Pet 2:12; Efe 5:8,9]

Sheria na Manabii

17Msidhani ya kuwa nilikuja kuitangua Torati au Manabii; la, sikuja kutangua, bali kutimiliza.[#Mt 3:15; Rum 3:31; 10:4]

18Kwa maana, amin, nawaambia, Mpaka mbingu na nchi zitakapoondoka, yodi moja wala nukta moja ya torati haitaondoka, hata yote yatimie.[#Lk 16:17; 21:33; #5:18 tazama 2 Kor 1:20 na Ufu 3:14. Maana yake ni Ni hakika, au Ni kweli hasa nisemayo. Hilo ni neno la Kiaramu lisilofasiriwa kwa Kigiriki. Ni neno lililotamkwa, kwa lugha iyo hiyo ya Kiaramu, na Yesu Kristo mwenyewe. Litumiwapo mwisho wa sala, maana yake ni Na iwe hivyo.]

19Basi mtu yeyote atakayevunja amri moja katika hizi zilizo ndogo, na kuwafundisha watu hivyo, ataitwa mdogo kabisa katika ufalme wa mbinguni; bali mtu atakayezitenda na kuzifundisha, huyo ataitwa mkubwa katika ufalme wa mbinguni.[#Yak 2:10; 1 Kor 15:9]

20Maana nawaambia ya kwamba, Haki yenu isipozidi hiyo haki ya Waandishi na Mafarisayo, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni.

Kuhusu hasira

21Mmesikia watu wa kale walivyoambiwa, Usiue, na mtu akiua, itampasa hukumu.[#Kut 20:13; 21:12; Law 24:17; Kum 5:17; 17:8]

22Bali mimi nawaambieni, Kila amkasirikiaye ndugu yake itampasa hukumu; na mtu akimtusi ndugu yake, anastahili kuhukumiwa na baraza; na mtu akimwambia nduguye, Ewe mpumbavu, anastahili kuingia katika moto wa Jehanamu.[#1 Yoh 3:15]

23Basi ukileta sadaka yako madhabahuni, ukikumbuka ya kuwa ndugu yako ana neno juu yako,[#Mk 11:25]

24iache sadaka yako mbele ya madhabahu, uende zako, upatane kwanza na ndugu yako, kisha urudi uitoe sadaka yako.

25Patana na mshitaki wako upesi, wakati uwapo pamoja naye njiani; yule mshitaki asije akakupeleka kwa hakimu, na hakimu akakupeleka kwa askari, ukatupwa gerezani.[#Mt 6:14,15; 18:35; Lk 12:58,59]

26Amin, nakuambia, Hutoki humo kamwe hadi utakapolipa senti ya mwisho.

Kuhusu uzinzi

27Mmesikia kwamba imenenwa, Usizini;[#Kut 20:14; Kum 5:18]

28lakini mimi nawaambia, Kila mtu atazamaye mwanamke kwa kumtamani, amekwisha kuzini naye moyoni mwake.[#Ayu 31:1; 2 Pet 2:14]

29Jicho lako la kulia likikukosesha, ling'oe ulitupe mbali nawe; kwa maana yakufaa kiungo chako kimoja kipotee kuliko mwili wako wote utupwe katika Jehanamu.[#Mt 18:8,9; Mk 9:42,47; Kol 3:5]

30Na mkono wako wa kulia ukikukosesha, ukate uutupe mbali nawe; kwa maana yakufaa kiungo chako kimoja kipotee kuliko mwili wako wote kutupwa katika Jehanamu.[#Mt 18:8; Mk 9:43]

Kuhusu talaka

31Imenenwa pia, Mtu akimwacha mkewe, na ampe hati ya talaka;[#Kum 24:1-4; Mt 19:7; Mk 10:4]

32lakini mimi nawaambia, Kila mtu amwachaye mkewe, isipokuwa kwa sababu ya uasherati, amfanya kuwa mzinzi; na mtu akimwoa yule aliyeachwa, azini.[#Mt 19:9; Mk 10:11-12; Lk 16:18; 1 Kor 7:10-11]

Kuhusu viapo

33Tena mmesikia watu wa kale walivyoambiwa, Usiape uongo, ila mtimizie Bwana viapo vyako;[#Law 19:12; Hes 30:2; Kum 23:21; Kut 20:7]

34lakini mimi nawaambia, Usiape kabisa; hata kwa mbingu, kwa maana ndicho kiti cha enzi cha Mungu;[#Yak 5:12; Isa 66:1; Mt 23:16-22; Mdo 7:49]

35wala kwa nchi, kwa maana ndipo pa kuwekea miguu yake; wala kwa Yerusalemu, kwa maana ndio mji wa Mfalme mkuu.[#Isa 66:1; Zab 48:2]

36Wala usiape kwa kichwa chako, maana huwezi kufanya unywele mmoja kuwa mweupe au mweusi.

37Bali maneno yenu yawe Ndiyo, ndiyo; Siyo, siyo; kwa kuwa yazidiyo hayo yatoka kwa yule mwovu.[#2 Kor 1:17; Yak 5:12]

Kuhusu kujilipiza kisasi

38Mmesikia kwamba imenenwa, Jicho kwa jicho, na jino kwa jino;[#Kut 21:24; Law 24:20; Kum 19:21]

39Lakini mimi nawaambia, Msishindane na mtu mwovu; lakini mtu akupigaye shavu la kulia, mgeuzie na la pili.[#Lk 6:27-36; #Yn 18:22,23; Law 19:18]

40Na mtu atakaye kukushitaki na kulichukua shati lako, mwachie na koti pia.[#1 Kor 6:7]

41Mtu yeyote akikulazimisha mwendo wa maili moja, nenda naye maili mbili.

42Akuombaye, mpe; naye atakaye kukopa kwako, usimpe kisogo.

Upendo kwa adui

43Mmesikia kwamba imenenwa, Umpende jirani yako, na, Umchukie adui yako;[#Law 19:18]

44lakini mimi nawaambia, Wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi,[#Kut 23:4,5; Rum 12:14,20; Lk 23:34; Mdo 7:59]

45ili mpate kuwa wana wa Baba yenu aliye mbinguni; maana yeye huwaangazia jua lake waovu na wema, huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki.[#Efe 5:1]

46Maana mkiwapenda wanaowapenda ninyi mnapata thawabu gani? Hata watoza ushuru, je! Nao hawafanyi yayo hayo?

47Tena mkiwaamkia ndugu zenu tu, mnatenda tendo gani la ziada? Hata watu wa mataifa, je! Nao hawafanyi sawa na hayo?

48Basi ninyi iweni wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu.[#Law 19:2; Kum 18:13]

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya