Zaburi 10

Zaburi 10

Sala ya ukombozi kutoka kwa adui

1Ee BWANA, kwa nini wasimama mbali?

Kwani unajificha nyakati za shida?

2Kwa kiburi chake asiye haki mnyonge anafuatiwa kwa ukali;[#Mit 5:22]

Na wanaswe kwa hila zizo hizo walizoziwaza.

3Maana mdhalimu hujisifia tamaa ya nafsi yake,

Na mwenye choyo humkana BWANA na kumdharau.

4Mdhalimu kwa kiburi cha uso wake[#2 Fal 18:35; Ayu 21:15; Zab 12:3-5]

Asema, Mungu Hatapatiliza.

Mawazo yake yote ni, Hakuna Mungu;

5Njia zake ni thabiti kila wakati.

Hukumu zako ziko juu asizione,

Adui zake wote awakaripia.

6Asema moyoni mwake, Sitaondoshwa,

Kizazi baada ya kizazi sitakuwamo taabuni.

7Kinywa chake kimejaa laana,[#Rum 3:14]

Na hila na dhuluma.

Chini ya ulimi wake kuna madhara na uovu,

8Hujificha na kuotea vijijini.

Katika maficho humwua asiye na hatia,

Macho yake humtazama kisiri mtu duni.

9Huotea faraghani kama simba pangoni,

Huotea amkamate mtu mnyonge.

Naam, humkamata mtu mnyonge,

Na kumkokota akiwa wavuni mwake.

10Hujikunyata na kuinama;

Watu duni huanguka kwa nguvu zake.

11Asema moyoni mwake, Mungu amesahau,

Auficha uso wake, haoni kamwe.

12Inuka, Ee Mungu BWANA, uuinue mkono wako, Ee Mungu

Usiwasahau wanyonge.

13Kwa nini mdhalimu amdharau Mungu.

Akisema moyoni mwake, Hutapatiliza?

14Umeona, maana unaangalia matatizo na dhiki,

Uyatwae mkononi mwako.

Mtu duni hukuachia nafsi yake,

Maana umekuwa msaidizi wa yatima.

15Uuvunje mkono wa mdhalimu,

Na mwovu, uipatilize dhuluma yake, hadi usiione.

16BWANA ndiye Mfalme milele na milele;

Mataifa yataangamia kutoka nchi yake.

17BWANA, utayasikia matakwa ya wanyonge,

Uutaidhibiti mioyo yao, utalitega sikio lako.

18Ili kumhukumu yatima na aliyeonewa,

Binadamu aliye udongo asizidi kudhulumu.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya