Zaburi 8

Zaburi 8

Utukufu wa Mungu na hadhi ya utu

1Ee, MUNGU, Bwana wetu

Jinsi lilivyo tukufu jina lako duniani kote!

Wewe umeuweka utukufu wako mbinguni;

2Vinywani mwa watoto wachanga na wanyonyao[#Mt 21:16; 11:25; 1 Kor 1:27]

Umeiweka misingi ya nguvu;

Kwa sababu yao wanaoshindana nawe;

Uwakomeshe adui na mjilipiza kisasi.

3Nikiziangalia mbingu zako, kazi ya vidole vyako,[#Zab 44:16; 19:1; Ayu 22:12; Rum 1:20]

Mwezi na nyota ulizoziratibisha;

4Mtu ni kitu gani hata umkumbuke,[#Ayu 7:17-18; Zab 144:3; Ebr 2:6-8]

Na binadamu hata umwangalie?

5Umemfanya mdogo kuliko Mungu;

Umemvika taji la utukufu na heshima;

6Umemtawaza juu ya kazi za mikono yako;[#1 Kor 15:27; Efe 1:22; Ebr 2:8; Mwa 1:26]

Umevitia vitu vyote chini ya miguu yake.

7Kondoo, na ng'ombe wote pia;

Naam, na wanyama wa porini;

8Ndege wa angani, na samaki wa baharini;

Na kila kipitacho njia za baharini.

9Wewe, MUNGU, Bwana wetu,[#Ayu 11:7; Zab 35:10]

Jinsi lilivyo tukufu jina lako duniani kote!

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya