Yoshua Mwana wa Sira 34

Yoshua Mwana wa Sira 34

Ndoto Hazimaanishi kitu

1Mwenye kuufuata ubatili ataona udanganyifu; na ndoto huwapa wapumbavu mabawa.[#Kum 13:1-5; 18:9-14]

2Mithili ya yule akamataye kivuli, au kuufuata upepo, ndivyo alivyo mtu anayetumainia ndoto.

3Maono ya ndoto ni kama lila na fila; kama mlingano wa uso wako na uso wenyewe.

4Katika kitu kichafu kipande gani kitakuwa safi? Na katika uongo sehemu gani ni kweli?

5Maaguzi, na ndege, na ndoto, ni ubatili; na kwa hayo moyo wa mtu una mauzauza, kama mwanamke wakati wa uchungu.

6Zisipoletwa naye Aliye Juu katika majilio yake, usiziangalie moyoni.

7Kwa maana ndoto zimewadanganya wengi, nao wamebatilishwa matumaini yao.

8Pasipokuwapo uongo torati itatekelezwa;

Kinywani mwa mwaminifu hekima hukamilika.

Uzoefu kama Msafiri

9Mtu mwelekevu huyatafuta mambo yote, na yeye aliyeona mengi atauhubiri ufahamu wake.

10Asiye mwelekevu ajua machache; lakini aliyesafiri ataongeza werevu wake.

11Katika kusafiri kwangu mimi mwenyewe nimeona mambo mengi, hata ufahamu wangu unaweza kupita niwezavyo kusema.

12Tena mara nyingi nimeona hatari, hata ya kufa; lakini kwa sababu ya hayo nikapona.

13Roho zao wamchao BWANA wataishi;

Maana taraja lao lina Yeye awaokoaye.

Mcheni Bwana

14Amchaye BWANA haoni hofu wala hafanyi woga;

Maana Yeye ndiye aliye tumaini lake.

15Amebarikiwa roho yule amchaye BWANA;

Amtazamaye ni nani, na nguzo yake ni nini?

16Macho ya BWANA yawaelekea wampendao;

Ngao yenye nguvu na nguzo thabiti,

Kifuniko wakati wa joto na jua kichwani,

Huwalinda wasijikwae, huwasaidia wasianguke.

17Huihuisha roho, huyaangaza macho,

Hutoa afya, na uzima, na baraka.

Dhabihu na Matoleo

18Mtu atoaye sadaka kitu kilichopatikana kwa udhalimu, sadaka yake imetolewa kwa dhihaka, wala dhihaka za wasio haki hazipati kibali.

19Yeye Aliye Juu hapendezwi na sadaka za waovu, wala Yeye haridhii dhambi kwa ajili ya wingi wa kafara.

Dhabihu Zitolewazo

20Yeyote aletaye mali za maskini ziwe sadaka, mfano wake ni mtu amchinjaye mwana mbele ya macho ya babaye.

21Riziki ya wahitaji ndiyo uzima wake maskini, na mwenye kumnyima ni mtu wa damu.

22Amnyang'anyaye jirani yake riziki yake ni mmwaga damu, naye amnyimaye mtumishi mshahara wake ni mwuaji.

23Iwapo mtu mmoja anajenga, mwenzake akabomoa, je! Faida yao ni nini ila kazi bure tu?

24Iwapo mtu mmoja anaomba, na mwingine analaani, je! BWANA ataisikia sauti ya yupi?

25Mwenye kutawadha baada ya kugusa maiti akaigusa tena, kule kutawadha kwake kwafaa nini?

26Kadhalika mtu afungaye kwa sababu ya dhambi zake, akaenda akazifanya zizo hizo tena, ni nani atakayeisikiliza sala yake, ama kujinyenyekeza kwake kutamfaidia nini?

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya