Yoshua Mwana wa Sira 51

Yoshua Mwana wa Sira 51

NYONGEZA

Sala ya Yoshua Mwana wa Sira

1Ee BWANA, Mfalme wangu, nitakushukuru; Ee Mungu wa wokovu wangu, nitakuhimidi.

2Nami nitalitangaza jina lako Wewe uliye nguvu za uhai wangu. Kwa maana umeikomboa roho yangu na mauti, ukauzuia mwili wangu usishuke shimoni, ukaiokoa miguu yangu na uwezo wa kuzimu. Ukaniponya na masingizio ya watu katika mapigo ya ulimi usengenyao, na midomo yao wanaogeukia uongo.

3Ulikuwa upande wangu juu yao walioniondokea. Ukaniokoa, kwa kadiri ya wingi wa rehema zako, katika mtego wao waliokutazamia kuanguka kwangu, katika mikono yao waliotafuta maisha yangu; na katika mateso mengi umeniponya.

4Ukaniokoa na moto ulionisonga pande zote, yaani, katikati ya moto nisiouwasha mimi.

5Ukaniokoa katika vilindi vya kuzimu, na midomo itungayo madhara na kuzua maneno ya uongo, mishale ya ulimi wenye hila.

6Nami, roho yangu ilikaribia mauti, na maisha yangu yakawa karibu na kuzimu.

7Nikageukia pande zote, wala hakuna wa kunisaidia. Nilikuwa nikimtazamia mtu atakayenitegemeza, wala hakuna.

8Ndipo nilipozikumbuka fadhili za BWANA na rehema zake, na matendo yake yaliyokuwapo tangu milele; ambaye huwaokoa wamngojao, na kuwaponya katika mabaya yote.

9Hivyo nikaiinua dua yangu kutoka nchi, nikamlilia kutoka malangoni mwa kuzimu.

10Nilimwita BWANA, Wewe, Baba yangu,

Mwenye amri ya wokovu wangu,

Usiniache siku ya msiba wangu,

Katika siku ya uharibifu na ukiwa.

Nami nitalihimidi Jina lako daima,

Na kukukumbuka kwa shukrani.

11Ndipo BWANA alipoisikia sauti yangu, akaisikiliza dua yangu; akanikomboa katika mabaya yote, akaniokoa katika siku ya taabu.

12Kwa hiyo nitamshukuru na kumsifu, na kulihimidi Jina la BWANA.

Mashairi juu ya kuitafuta hekima

13Mimi nilipokuwa kijana, kabla sijasafiri bado, niliitafuta hekima kwa bidii katika sala yangu,

14na mbele ya hekalu nikaomba, nami hata mwisho nitazidi kuitafuta.

15Ikachanua kama zabibu inavyoiva, na moyo wangu ukapendezwa, na mguu wangu ukaenda katika njia iliyo sawa. Tangu ujana wangu nikafanya kuaua,

16nikaliinamisha sikio kidogo, nikaipokea, nikajipatia mafundisho tele.

17Kwangu nira yake ikawa utukufu, nami nitamshukuru Yeye aliyenifundisha.

18Kwa maana nilikusudia kujizoeza nayo, nikajitahidi katika yaliyo mema, wala sitatahayarishwa.

19Roho yangu imeshindana kwa nguvu ndani yake, na kuhusu kutenda kwangu nilikuwa mwangalifu; nikainyosha mikono yangu juu mbinguni, nikaulalamikia ujinga wangu.

20Nikaielekeza roho yangu moja kwa moja kwake, na katika unyofu nikaiona; tangu mwanzo nikajipatia ufahamu, na kwa hiyo sitakataliwa milele.

21Nao mtima wangu ukatamani kuitazama, kwa hiyo nimeipata kama tunu.

22Naye BWANA akanipa thawabu ya usemaji, basi kwa midomo yangu nitamhimidi.

23Enyi wajinga, mnikaribie, na kutua katika nyumba yangu ya mafundisho.

24Ya nini kupungukiwa na hayo, na roho zenu kuona kiu?

25Nimefumbua kinywa changu kusema, Jipatieni hekima pasipo fedha,

26jitieni shingo zenu chini ya nira yake, roho zenu ziuchukue mzigo wake; mradi ni karibu nao waitafutao.

27Tazameni kwa macho yenu kwamba mimi nilifanya kazi kitambo, na kujipatia wingi wa raha.

28Sikilizeni mafundisho yangu ingawa ni machache, na kwa hayo mtapata thawabu kama dhahabu.

29Roho zenu na ziifurahie rehema ya Mungu, wala hamtatahayarika katika kumsifu.

30Fanyeni kazi zenu kabla haujaja muhula, na wakati wake BWANA atawajazi.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya