The chat will start when you send the first message.
1BWANA akamtokea Ibrahimu karibu na mialoni ya Mamre, alipokuwa ameketi mlangoni pa hema yake mchana wakati wa hari.[#Mwa 13:18; 14:13; Mdo 7:2]
2Akainua macho yake akaona, na tazama, watu watatu wamesimama mbele yake. Naye alipowaona alipiga mbio kuwalaki kutoka mlangoni pa hema, akainama mpaka nchi,[#Ebr 13:2; Mwa 18:22; 19:1; 1 Pet 4:9]
3akasema, Bwana wangu, kama nimeona fadhili machoni pako nakuomba usinipite sasa mimi mtumwa wako.
4Na yaletwe basi maji kidogo mkanawe miguu, mkapumzike chini ya mti huu.[#Mwa 24:32; 43:24]
5Nami nitaleta chakula kidogo, mkaburudishe moyo, baadaye mwendelee, iwapo mmemjia mtumwa wenu. Wakasema, Haya, fanya kama ulivyosema.
6Basi Ibrahimu akaenda hima hemani kwa Sara, akasema, Himiza vipimo vitatu vya unga safi, uukande, ufanye mikate.
7Ibrahimu akapiga mbio kwenda kundini, akaleta ndama wa ng’ombe aliye laini, mzuri, akampa mtumishi, naye akahimiza kuiandaa.
8Akatwaa siagi na maziwa, na ndama aliyoiandaa, akawaandikia mbele yao, akasimama karibu nao chini ya mti, nao wakala.
9Wakamwambia, Yu wapi Sara mkeo? Akasema, Yumo hemani.[#Mwa 24:67; Tit 2:5]
10Akamwambia, Hakika nitakurudia wakati huu huu mwakani, na tazama, Sara mkeo atapata mwana wa kiume. Sara akasikia mlangoni pa hema iliyokuwapo nyuma yake.[#Rum 9:9; Mwa 21:2; Lk 1:13]
11Basi Ibrahimu na Sara walikuwa wazee, na umri wao mkubwa, na Sara alikuwa amekoma katika desturi ya wanawake.[#Rum 4:19; Ebr 11:11]
12Kwa hiyo Sara akacheka moyoni mwake, akisema, Niwapo mkongwe, nitapata furaha, na bwana wangu mzee?[#1 Pet 3:6; Lk 1:18; Mwa 17:17]
13BWANA akamwambia Ibrahimu, Mbona Sara amecheka akisema, Mimi kweli nitazaa mwana, nami ni mzee?
14Kuna neno gani lililo gumu la kumshinda BWANA? Kwa muhula wake nitakurudia, wakati huu huu mwakani, na Sara atapata mwana wa kiume.[#Lk 1:37; Zab 115:3; Yer 32:17; Zek 8:6; Mt 3:9; 19:26; Rum 4:21; Ebr 11:19]
15Akakana Sara, akisema, Sikucheka, maana aliogopa. Naye akasema, Sivyo, umecheka.
16Kisha watu hao wakaondoka huko wakaelekeza nyuso zao Sodoma. Ibrahimu akaenda pamoja nao awasindikize.
17BWANA akanena, Je! Nimfiche Ibrahimu jambo nilifanyalo,[#Zab 25:14; Amo 3:7; Yn 15:15]
18akiwa Ibrahimu atakuwa taifa kuu, hodari, na katika yeye mataifa yote ya dunia watabarikiwa?[#Mwa 12:3; 22:18; Zab 72:17; Mdo 3:25; Gal 3:8,9,16,18]
19Kwa maana nimemjua ya kwamba atawaamuru wanawe, na nyumba yake baada yake waishike njia ya BWANA, wafanye haki na hukumu, ili kwamba BWANA naye akamtimizie Ibrahimu ahadi zake.[#Kum 6:6,7; Yos 24:15; Efe 6:4]
20BWANA akasema, Kwa kuwa kilio cha Sodoma na Gomora kimezidi, na dhambi zao zimeongezeka sana,[#Mwa 4:10; 19:13; Yak 5:4]
21basi, nitashuka sasa nione kama wanayotenda ni kiasi cha kilio kilichonijia; na kama sivyo, nitajua.[#Mwa 11:5; Kut 3:8; Zab 14:2; Ebr 4:13]
22Basi wale watu wakatoka huko wakaelekea Sodoma; lakini Ibrahimu alikuwa akali akisimama mbele za BWANA.[#Mwa 18:1,2]
23Ibrahimu akakaribia, akasema, Je! Utaharibu mwenye haki pamoja na mwovu?[#Hes 16:22; 2 Sam 24:17; Zab 11:4-7]
24Huenda wakawapo wenye haki hamsini katika mji, utaharibu, wala hutauacha mji kwa ajili ya hao hamsini wenye haki waliomo?[#Mt 7:13,14]
25Hasha usifanye hivyo, ukamwue mwenye haki pamoja na mwovu, mwenye haki awe kama mwovu. Hasha; Mhukumu ulimwengu wote asitende haki?[#Isa 3:10,11; Ayu 8:3,20; Zab 58:11; 94:2; Rum 3:5,6]
26BWANA akasema, Nikiona katika Sodoma wenye haki hamsini mjini, nitapaacha mahali pote kwa ajili yao.[#Yer 5:1; Eze 22:30; Mt 24:22]
27Ibrahimu akajibu, akasema, Basi, nimeshika kusema na Bwana, nami ni mavumbi na majivu tu.[#Lk 18:1; Zab 8:4]
28Huenda wakapunguka watano katika wale hamsini wenye haki, je! Utaharibu mji wote kwa kupungua watano? Akasema, Sitauharibu, nikiona humo arobaini na watano.
29Akazidi tena kusema naye, akinena, Huenda wakaonekana humo arobaini? Akasema, Sitafanya kwa ajili ya hao arobaini.[#1 The 5:17]
30Akasema, Bwana asiwe na hasira, nami nitasema, Huenda wakaonekana huko thelathini? Akasema, Sitafanya, nikiona humo thelathini.[#Isa 55:8,9]
31Akasema, Tazama, nimeshika kusema na Bwana, huenda wakaonekana huko ishirini? Akasema, Sitaharibu kwa ajili ya hao ishirini.[#Ebr 4:16]
32Akasema, Bwana asiwe na hasira, nami nitasema mara hii tu, Huenda wakaonekana huko kumi? Akasema, Sitaharibu kwa ajili ya hao kumi.[#Amu 6:39; Kut 34:6,7; Zab 34:15; Mit 15:29; 1 Yoh 3:22; Yak 5:16]
33Basi BWANA alipokwisha kuzungumza na Ibrahimu, akaenda zake; Ibrahimu naye akarudi mahali pake.