The chat will start when you send the first message.
1PAOLO na Timotheo, watumwa wa Yesu Kristo, kwa watakatifu wote katika Kristo Yesu, walio katika Filipi, pamoja na maaskofu na wakhudumu;
2Neema iwe kwenu na amani zitokazo kwa Mungu Baba na kwa Bwana Yesu Kristo.
3Namshukuru Mungu wangu killa niwakumbukapo,
4siku zote killa niwaombeapo ninyi nyote nikisema sala zangu kwa furaha,
5kwa sababu ya ushirika wenu katika kuieneza Injili, tangu siku ya kwanza hatta leo hivi;
6niliaminilo ndilo hili, ya kwamba yeye aliyeanza kazi njema mioyoni mwenu ataimaliza hatta siku ya Yesu Kristo;
7kama ilivyo wajib wangu kufikiri haya juu yenu nyote; kwa sababu ninyi mmo moyoni mwangu; kwa kuwa katika kufungwa kwangu na katika kazi ya kuitetea Injili na kuithubutisha, ninyi nyote mmeshirikiana nami neema hii.
8Maana Mungu ni shahidi wangu, jinsi ninavyowaonea shauku katika moyo wake Kristo Yesu.
9Na hii ndiyo sala yangu, pendo lenu lizidi kuwa jingi sana, katika hekima na ufahamu wote;
10mpate kuyakubali yaliyo mema; illi mwe na mioyo safi, bila kosa, mpaka siku ya Kristo,
11mmejazwa matuuda ya haki, kwa njia ya Yesu Kristo, kwa utukufu na sifa ya Mungu.
12Lakini, ndugu zangu, nataka mjue ya kuwa mambo yote yaliyonipata yamekuja yakaieneza Injili;
13hatta vifungo vyaugu vimekuwa dhahiri katika Kristo, katika praitorio, na kwa wengine wote.
14Na walio wengi wa ndugu walio katika Bwana, wakipata kuthubutika kwa ajili ya kufungwa kwangu, wamezidi sana kuthubutu kulinena neno la Bwana pasipo khofu.
15Wengine wanakhubiri khabari za Kristo kwa sababu ya husuda na fitina: na wengine kwa nia njema.
16Hawa wanamkhubiri Kristo kwa fitina wala si kwa moyo mweupe, wakidhani kuongeza taabu za kufungwa kwangu;
17na hawa wengine kwa pendo, wakijua ya kuwa nimewekwa illi niitetee Injili.
18Yadhuru nini? bali kwa njia zote, ikiwa ni kwa hila, au ikiwa ni kwa kweli, Kristo anakhubiriwa; na kwa hiyo nafurahi, naam, nami nitafurahi.
19Maana najua ya kuwa haya yatanigeukia kuwa wokofu wangu, kwa sababu ya kuomba kwenu, na kuruzukiwa Roho ya Yesu Kristo,
20kama nilivyotazamia sana, na kutumaini, kwamba sitaaibika kabisa, bali kwa nthabiti wote, kama siku zote, na sasa tena Kristo atatukuzwa katika mwili wangu, ikiwa kwa maisha yangu, au kwa mauti yangu.
21Kwa maana kwangu mimi kuishi ni Kristo, na kufa ni faida.
22Illa ikiwa kuishi katika mwili, kwangu mimi ni matunda ya kazi; bassi nitakalolichagua sitambui.
23Ninasongwa kati kati ya mambo mawili; ninatamani kwenda zangu nikae na Kristo; maana ni vizuri zaidi;
24bali kudumu katika mwili kwuhitajiwa zaidi kwa ajili yenu.
25Nami nikitumaini haya, najua ya kuwa nitakaa na kudumu pamoja nanyi, illi muendelee mkapate kufurahi katika imani;
26kujisifu kwenu kupate kuzidi katika Kristo Yesu kwa ajili yangu kwa sababu ya kuwapo kwangu pamoja nanyi nyote tena.
27Lakini mwenendo wenu uwe kama inavyoipasa Injili ya Kristo, illi, nikija na kuwaona ninyi, au nisipokuwapo, niyasikie mambo yenu, kama mnasimama imara katika roho moja, kwa moyo mmoja mkiishindania imani ya Injili;
28wala hamwogopi adui zenu, katika neno lo lote; kwao hao ni ishara wazi ya kupotea, bali kwenu ninyi ni ishara ya wokofu, nao wa Mungu.
29Maana mmepewii kwa ajili ya Kristo, si kumwamini tu, illa na kuteswa kwa ajili yake,
30mkiwa na mashindano yale yale mliyoyaona kwangu, mkasikia kvvamba ninayo hatta sasa.