Wagalatia 1

Wagalatia 1

1Salamu kutoka kwa mtume Paulo. Sikutumwa na kundi lolote la watu au mtu yeyote hapa duniani niwe mtume. Sikupewa mamlaka yangu na mwanadamu yeyote. Nilipewa mamlaka haya moja kwa moja kutoka kwa Kristo Yesu na Mungu Baba, aliyemfufua Yesu kutoka kwa wafu.[#1:1 Au “Mfalme Yesu”. Neno “Kristo” ni tafsiri ya Kiyunani ya neno la Kiebrania “Masihi”, ambao ni wadhifa wa kifalme. Tazama Mk 15:32; Lk 23:2. Tazama pia na katika Orodha ya Maneno.]

2Salamu pia kutoka kwa wote walio familia ya Mungu, walio pamoja nami.

Kwa makanisa yaliyoko Galatia:

3Namwomba Mungu Baba yetu na Bwana wetu Yesu Kristo awe mwema kwenu na awape neema na amani.

4Yesu alijitoa mwenyewe kwa ajili ya dhambi zetu ili atuweke huru kutoka katika uovu wa ulimwengu huu tunamoishi. Hili ndilo Mungu Baba yetu alitaka.

5Mungu Baba yetu anastahili utukufu milele na milele! Amina.

Kuna Ujumbe Mmoja tu wa Habari Njema

6Wakati mfupi tu uliopita Mungu aliwaita mkamfuata. Aliwaita katika neema yake kwa njia ya Kristo. Lakini sasa nashangazwa kwamba kwa haraka hivi mmegeuka mbali na kuamini kitu kingine tofauti kabisa na Habari Njema tuliyowahubiri.

7Hakuna ujumbe mwingine wa Habari Njema, lakini baadhi ya watu wanawasumbua. Wanataka kuibadili Habari Njema ya Kristo.

8Tuliwahubiri ninyi ujumbe wa Habari Njema tu. Hivyo laana ya Mungu impate mtu yeyote yule anayewahubiri ninyi ujumbe ulio tofauti, hata ikiwa ni mmoja wetu au malaika kutoka mbinguni!

9Nitalisema tena lile nililolisema hapo mwanzo. Ninyi mmekwishaipokea Habari Njema. Yeyote atakayewahubiri kitu kingine tofauti na ile Habari Njema mliyoipokea, basi mjue kwamba Mungu atamlaani mtu huyo!

10Sasa mnafikiri ninajaribu kuwapendeza wanadamu? Hapana, ninataka kumpendeza Mungu siyo wanadamu. Kama ningekuwa najaribu kuwapendeza wanadamu, nisingekuwa mtumwa wa Kristo.

Mamlaka ya Paulo ni Kutoka kwa Mungu

11Ndugu zangu, ninawataka mjue kuwa ujumbe wa Habari Njema niliowaambia haukuandaliwa na mtu yeyote.

12Sikuupata ujumbe wangu kutoka kwa mwanadamu yeyote. Habari Njema siyo kitu nilichojifunza kutoka kwa watu. Yesu Kristo mwenyewe ndiye aliyenifunulia Habari Njema ninayowahubiri watu.

13Mmesikia juu ya mwenendo wangu hapo zamani nilipokuwa mfuasi hodari wa dini ya Kiyahudi. Nililitesa kwa nguvu kanisa la Mungu, nikiwa na shabaha ya kuliangamiza kabisa.

14Nilipata maendeleo makubwa katika dini ya Kiyahudi kwa kufanya kazi na kusoma kwa bidii kwa sababu nilikuwa mwaminifu kwa desturi za baba zetu.

15Lakini Mungu alikuwa na mpango maalumu kwa ajili yangu hata kabla sijazaliwa. Hivyo aliniita kwa neema yake. Na ilimpendeza[#1:15 Tazama Isa 49:1; Yer 1:5.]

16kumfunua Mwanaye ili niweze kuwahubiri Habari Njema watu wasio Wayahudi. Hicho ndicho nilichofanya baada ya hapo. Sikuomba ushauri ama msaada wowote kutoka kwa mtu yeyote.

17Sikwenda Yerusalemu kuwaona wale waliokuwa mitume kabla mimi sijawa mtume. Badala yake, kwanza nilienda moja kwa moja Arabia. Kisha baadaye, nikarudi katika mji wa Dameski.

18Miaka mitatu baadaye nilikwenda Yerusalemu kumwona Petro. Nilikaa naye kwa siku 15.[#1:18 Kwa maana ya kawaida, “Kefa”, jina la Kiaramu la Petro, mmoja wa mitume kumi na wawili wa Yesu. Majina yote mawili yanamaanisha “mwamba”. Pia katika 2:9,11,14.]

19Sikuonana na mtume mwingine yeyote, isipokuwa Yakobo mdogo wake Bwana peke yake.

20Mungu anajua kuwa hakuna ninachowaandikia kisicho cha kweli.

21Baadaye, nilielekea katika majimbo ya Shamu na Kilikia.

22Lakini kwa wakati ule, makanisa ya Kristo yaliyokuwa Uyahudi yalikuwa bado hayajanifahamu mimi binafsi.

23Walikuwa wamesikia tu juu yangu: “Mtu huyu alikuwa anatutesa. Lakini sasa anawaambia watu juu ya imani ile ile aliyojaribu kuiangamiza huko nyuma.”

24Waamini hawa walimsifu Mungu kwa sababu yangu.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi Toleo la Awali © 2017 Bible League International
Published by: Bible League International