The chat will start when you send the first message.
1Baada ya miaka 14 nilirudi tena Yerusalemu nikiwa na Barnaba na nilimchukua Tito pia.
2Nilikwenda kule maana Mungu alinionyesha kuwa ninapaswa kwenda. Niliwafafanulia Habari Njema kama nilivyoihubiri kwa watu wasio Wayahudi. Pia nilikutana faragha na wale waliokuwa wanatazamiwa kuwa viongozi. Nilitaka niwe na uhakika kuwa tulikuwa tunapatana ili kazi yangu ya nyuma na ile niliyokuwa naifanya sasa zisipotee bure.
3Tito, aliyekuwa pamoja nami ni Myunani. Hata hivyo viongozi hawa hawakulazimisha kumtahiri.
4Tulihitaji kuyazungumzia matatizo haya, kwa sababu wale waliojifanya kuwa ni ndugu zetu walikuja kwenye kundi letu kwa siri. Waliingia kama wapelelezi kutafiti kuhusu uhuru tuliokuwa nao ndani ya Kristo Yesu. Walitaka watufanye sisi watumwa,
5lakini hatukujiweka chini ya chochote ambacho hawa ndugu wa uongo walikitaka. Tulitaka ukweli wa Habari Njema ubaki ule ule na hatimaye uwafikie na ninyi.
6Na watu wale ambao walihesabiwa kuwa viongozi muhimu hawakuongeza lolote katika ujumbe wa Habari Njema niliyowahubiria watu. (Haijalishi kwangu kuwa walikuwa wa “muhimu” au la. Kwa Mungu binadamu wote ni sawa.)
7Lakini viongozi hawa waliona kuwa Mungu alinipa kazi maalumu ya kuhubiri Habari Njema kwa wasio Wayahudi, kama vile alivyomwagiza Petro kufanya kazi hiyo hiyo ya kuhubiri Habari Njema miongoni mwa Wayahudi.[#2:7 Jina la Kefa limetumika badala ya Petro katika nakala za kale za Kiyunani. Pia katika mstari wa 11.]
8Mungu alimpa Petro uwezo wa kufanya kazi kama mtume lakini kwa walio Wayahudi. Mungu akanipa mimi pia uwezo wa kufanya kazi kama mtume, lakini kwa wasiokuwa Wayahudi.
9Yakobo, Petro na Yohana walikuwa viongozi muhimu kanisani. Hawa wakaona kuwa Mungu alinipa kipaji hiki maalumu cha huduma, hivyo wakatupa mkono wa shirika mimi pamoja na Barnaba. Wakakubali kuwa sisi tutaendelea kufanya kazi miongoni mwao wasio Wayahudi, na wao wataendelea kufanya kazi miongoni mwao walio Wayahudi.
10Wakatuomba jambo moja tu, ya kwamba tukumbuke kuwahudumia waaminio walio maskini. Na kwa hakika hili lilikuwa jambo nililojitahidi kufanya.[#2:10 Maskini wanaozungumziwa hapa ni wale waliokuwemo miongoni mwa waamini katika kanisa la Yerusalemu.]
11Petro alipokuja Antiokia, alifanya kitu ambacho hakikuwa sahihi. Nami nikampinga, kwa sababu hakika alikuwa na hatia mbele za Mungu.
12Hivi ndivyo ilivyotokea: Petro alipokuja Antiokia, hapo awali kabla ya Wayahudi kufika, alikula na kujumuika na wasio Wayahudi. Lakini baada ya Wayahudi kufika kutoka kwa Yakobo, Petro akajitenga na wasio Wayahudi. Akaacha kula pamoja nao kwa sababu aliwaogopa Wayahudi.
13Hivyo Petro akafanya kama mnafiki, na waamini wengine pale Antiokia wakaungana naye katika unafiki huo. Wakamfanya hata Barnaba naye kuwa mnafiki kama wao.
14Hawakuwa wakiifuata kweli ya Habari Njema. Nilipoona hili, nilimweleza Petro mbele ya kila mtu. Nilisema, “Petro, wewe ni Myahudi, lakini huenendi kama Myahudi. Unaenenda kama mtu asiye Myahudi. Hivyo kwa nini unajaribu kuwalazimisha wale wasio Wayahudi kuenenda kama Wayahudi?
15Sisi ni Wayahudi kwa kuzaliwa. Hatukuzaliwa tukiwa ‘watenda dhambi’, kama vile Wayahudi wanavyowaita wale wasio Wayahudi.
16Lakini tunajua kuwa hakuna mtu anayehesabiwa haki mbele za Mungu kwa kuifuata sheria. Ni kwa kuamini katika Yesu Kristo ndiko kunamfanya mtu ahesabiwe haki mbele za Mungu. Hivyo hata nasi Wayahudi tumeiweka imani yetu katika Kristo Yesu, kwa sababu tulitaka kuhesabiwa haki mbele za Mungu. Na tumehesabiwa haki kwa imani ya Yesu Kristo, siyo kwa sababu tuliifuata sheria. Naweza kusema hili kwa sababu hakuna anayeweza kuhesabiwa haki kwa kuifuata Sheria ya Musa.[#2:16 Au “uaminifu wa”.; #2:16 Au “kupitia uaminifu wa”.]
17Kwa hiyo tunaamini uhusiano wetu kwa Kristo utatufanya tuhesabiwe haki mbele za Mungu. Ikiwa hiyo inatufanya tuonekane kama ‘watenda dhambi’ wasio Wayahudi, je itakuwa na maana kuwa Kristo anasababisha dhambi kuongezeka. Kwa hakika sivyo?
18Sheria ilijenga ukuta baina yetu Wayahudi na watu wengine wote, ukuta ambao nilijitahidi kuuvunja. Kweli nitakosea sana kuujenga tena ukuta huo.
19Sheria yenyewe iliyafikisha mwisho maisha yangu chini ya sheria. Nikafa katika sheria hiyo na kuwa huru ili niweze kuishi kwa ajili ya Mungu. Nimepigiliwa misumari msalabani pamoja na Kristo.
20Hivyo siyo mimi ninayeishi sasa; ni Kristo ndiye anayeishi ndani yangu. Bado naishi katika mwili wangu, lakini naishi kwa imani katika Mwana wa Mungu aliyenipenda na kujitoa mwenyewe kuniokoa mimi.
21Si mimi ninayeikataa neema ya Mungu kama vile haina manufaa yoyote. Kwa sababu ikiwa kwa kuifuata sheria ndivyo watu wanahesabiwa haki mbele za Mungu, basi Kristo alikufa pasipo faida!”