Filemoni 1

Filemoni 1

1Kutoka kwa Paulo mfungwa kwa kusudi la Kristo Yesu, na kutoka kwa Timotheo ndugu yetu. Kwa Filemoni rafiki yetu mpendwa na mtenda kazi pamoja nasi;[#1:1 Au “Mfalme Yesu”. Neno “Kristo” ni tafsiri ya Kiyunani ya neno la Kiebrania “Masihi”, ambao ni wadhifa wa kifalme. Tazama Mk 15:32; Lk 23:2. Tazama pia na katika Orodha ya Maneno.]

2kwa Afia dada yetu, Arkipo askari mwenzetu na kwa kanisa linalokutania nyumbani mwako.

3Neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na Bwana Yesu Kristo ziwe pamoja nawe.

Upendo na Imani ya Filemoni

4Namshukuru Mungu wangu siku zote kila ninapokukumbuka katika maombi yangu,

5kwa sababu nasikia juu ya upendo na uaminifu ulionao katika Bwana Yesu na unaouonesha kwa watu wa Mungu.

6Ninaomba kwamba ile imani unayoishiriki pamoja nasi ikusaidie wewe kuelewa kila fursa tulio nayo ya kutenda mema kama wale tunaomwamini Kristo.

7Nimepokea furaha kubwa na faraja kutokana na upendo wako, kwa sababu mioyo ya watu wa Mungu imepata nguvu mpya kwa juhudi zako ndugu yangu.

Mpokee Onesimo Kama Kaka

8Hivyo hiyo ndiyo sababu nakuagiza wewe kufanya jambo unalopaswa kulifanya. Kwa mamlaka niliyo nayo katika Kristo naweza kukuamuru kufanya hilo.

9Lakini sikuamuru; bali kwa sababu ya upendo nakusihi ufanye hivyo. Mimi Paulo, niliye mzee wa umri sasa, na sasa mfungwa kwa ajili ya Kristo Yesu.

10Ninakusihi kuhusu mwanangu Onesimo niliyemleta katika maisha mapya tulio nayo katika Bwana nilipokuwa gerezani.[#1:10 Paulo alimzaa Onesimo katika imani ya Yesu Kristo.]

11Huyo ambaye siku za nyuma hakuwa wa manufaa kwako, lakini sasa anafaa sio kwako tu bali hata kwangu mimi.[#1:11 Hapa Paulo anachezea maneno katika jina la Onesimo, lenye maana “anayefaa”. Aidha ni jina lilitumika zaidi kwa watumwa maana waliwafaa mabwana zao.]

12Ninamrudisha kwako, kitu ambacho kimekuwa kigumu sawa na kuupoteza moyo wangu.[#1:12 Kwa maana ya kawaida, “Ninamrudisha kwako, kitu ambacho kimekuwa kigumu sawa na kuupoteza moyo wangu.” Hii ni kama njia ya kusema kwamba kumtuma Onesimo ilikuwa kwa Paulo kana kwamba anapoteza kitu muhimu sana kwake kinachotoka ndani mwake.]

13Ningetamani kuendelea kuwa naye hapa, ili aendelee kunihudumia kwa niaba yako nitakapokuwa bado gerezani kwa ajili ya Habari Njema.

14Lakini sikuwa tayari kufanya jambo lo lote bila ruhusa yako, ili kila jambo lako zuri litendeke bila lazima bali kwa hiari yako mwenyewe.

15Labda sababu ya Onesimo kutenganishwa nawe kwa kipindi kifupi ni kuwezesha muwe pamoja siku zote,

16si mtumwa tena, bali ni zaidi ya mtumwa; kama ndugu mpendwa. Nampenda sana lakini wewe utampenda zaidi, sio tu kama kaka katika familia yenu, bali pia kama mmoja wa walio katika familia ya Bwana.

17Ikiwa unanitambua mimi kama niliye mwenye imani moja nawe, basi mpokee Onesimo na umkubali kama vile ambavyo ungenikubali.

18Endapo amekukosea jambo lo lote au unamdai kitu cho chote, unidai mimi badala yake.

19Mimi Paulo naandika kwa mkono wangu mwenyewe ya kwamba nitakulipa. Tena sina sababu ya kukumbusha kuwa una deni kwangu juu ya maisha yako.

20Kwa hiyo kaka yangu, kama mfuasi wa Bwana, tafadhali nipe upendeleo katika hili. Ndipo itakuwa faraja kuu kwangu kama kaka yako katika Kristo.[#1:20 Paulo hapa anachezea maneno tena katika jina la Onesimo, akitumia kitenzi kinachofanana na jina.]

21Ninapokuandikia barua hii nina ujasiri mkubwa kwamba utakubaliana nami na najua kwamba utafanya zaidi ya haya ninayokuomba.

22Pamoja na hayo naomba uniandalie chumba cha kufikia, kwa sababu nina matumaini kwamba kwa maombi yenu nitaachiliwa na kuletwa kwenu.

Salamu za Mwisho

23Epafra mfungwa pamoja nami katika Kristo Yesu anakusalimu.

24Marko, Aristarko, Dema, na Luka watendakazi pamoja nami nao wanakusalimu.

25Neema ya Bwana Yesu Kristo iwe pamoja nanyi.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi Toleo la Awali © 2017 Bible League International
Published by: Bible League International