The chat will start when you send the first message.
1Salamu kutoka kwa Paulo, mtumishi wa Kristo Yesu.[#1:1 Au “Mfalme Yesu”. Neno “Kristo” ni tafsiri ya Kiyunani ya neno la Kiebrania “Masihi”, ambao ni wadhifa wa kifalme. Tazama Mk 15:32; Lk 23:2. Tazama pia na katika Orodha ya Maneno.]
Mungu alinichagua niwe mtume na akanipa kazi ya kuhubiri Habari Njema yake.
2Tangu zamani, kwa vinywa vya manabii katika Maandiko Matakatifu, Mungu aliahidi kwamba angewaletea Habari Njema watu wake.
3Habari Njema hii inahusu Mwana wa Mungu, ambaye kama mwanadamu, alizaliwa katika ukoo wa Mfalme Daudi.
4Na alipofufuliwa na Roho Matakatifu kutoka kwa wafu, alipewa mamlaka kamili ya kutawala kama Mwana wa Mungu. Ni Yesu Kristo, Bwana wetu.[#1:4 Kwa maana ya kawaida, “Roho wa Utakatifu”.]
5Kupitia kwa Yesu, Mungu amenionyesha wema wake. Na amenipa mamlaka ya kuwaendea watu wa mataifa yote na kuwaongoza kumwamini na kumtii yeye. Kazi yote hii ni kwa ajili yake.
6Nanyi pia ni miongoni mwa waliochaguliwa na Mungu ili mmilikiwe na Yesu Kristo.
7Waraka huu ni kwa ajili yenu ninyi nyote mlio huko Rumi. Kwani Mungu anawapenda na amewachagua kuwa watu wake watakatifu.
Ninamwomba Mungu Baba yetu na Bwana wetu Yesu Kristo, wawape ninyi neema na amani.
8Kwanza, ninamshukuru Mungu wangu kupitia Yesu Kristo kwa ajili yenu ninyi nyote. Ninamshukuru yeye kwa sababu kila mahali ulimwenguni watu wanazungumza kuhusu imani yenu kuu.
9-10Kila wakati ninapoomba, ninawakumbuka ninyi daima. Mungu anajua kuwa hii ni kweli. Yeye ndiye ninayemtumikia kwa moyo wangu wote nikiwaambia watu Habari Njema kuhusu Mwanaye. Hivyo ninaendelea kuomba kwamba mwishowe Mungu atanifungulia njia ili niweze kuja kwenu.
11Ninataka sana niwaone na niwape zawadi ya kiroho ili kuimarisha imani yenu.
12Ninamaanisha kuwa ninataka tusaidiane sisi kwa sisi katika imani tuliyo nayo. Imani yenu itanisaidia mimi, na imani yangu itawasaidia ninyi.
13Kaka zangu na dada zangu, ninataka mjue kwamba nimepanga mara nyingi kuja kwenu, lakini jambo fulani hutokea na kubadili mipango yangu kila ninapopanga kuja. Juu ya kazi yangu miongoni mwenu, ningependa kuona matokeo yale yale mazuri yakitokea ya kazi yangu miongoni mwa watu wengine wasio Wayahudi.
14Imenilazimu kuwatumikia watu wote; waliostaarabika na wasiostaarabika, walioelimika na wasio na elimu.[#1:14 Kwa maana ya kawaida, “Wayunani na wasio Wayunani”. Tazama katika Orodha ya Maneno.]
15Ndiyo sababu ninataka sana kuzihubiri Habari Njema kwenu ninyi pia mlio huko Rumi.
16Kwa mimi hakuna haya katika kuhubiri Habari Njema. Ninayo furaha kwa sababu Habari Njema ni nguvu ya Mungu inayomwokoa kila anayeamini, yaani inawaokoa Wayahudi kwanza, na sasa inawaokoa Mataifa.[#1:16 Paulo anazungumzia suala la kuona haya kwa kuihubiri Habari Njema (injili) kwa sababu, nyakati zake, Habari Njema zilileta mshtuko na fadhaa kwa watu wengi. Kama anavyoandika katika barua zake nyingine, msingi wa ujumbe wake ulikuwa “Kristo (Mfalme toka kwa Mungu) aliuawa msalabani.” Anaongeza, “Ujumbe huu ni kikwazo kwa Wayahudi, na kwa watu wengine ni upuuzi.” Tazama 1 Kor 1:22-25.; #1:16 Yaani watu wasio Wayahudi.]
17Ndiyo, wema wa uaminifu wa Mungu umedhihirishwa katika Habari Njema kwa uaminifu wa mmoja, ambao huongoza imani ya wengi. Kama Maandiko yanavyosema, “Aliye na haki mbele za Mungu ataishi kwa imani.”[#1:17 Au “Mwenye haki”, mara nyingi hutumika kama cheo cha Masihi, Mfalme Mteule wa Mungu aliyeahidiwa katika Agano la Kale. Tazama Isa 53:11; Hab 2:4; Zek 9:9; Mdo 3:14; 7:52; 22:14.; #1:17 Katika Hab 2:4, ambayo pia, inaweza kutafsiriwa kuwa, “Mwenye haki ataishi kwa uaminifu.”]
18Mungu huonesha hasira yake kutokea mbinguni dhidi ya mambo mabaya ambayo waovu hutenda. Hawamheshimu na wanatendeana mabaya. Maisha yao maovu yanasababisha ukweli kuhusu Mungu usijulikane.
19Hili humkasirisha Mungu kwa sababu wamekwisha oneshwa Mungu alivyo. Ndiyo, Mungu ameliweka wazi kwao.
20Yapo mambo yanayoonekana kuhusu Mungu, kama vile nguvu zake za milele na yale yote yanayomfanya awe Mungu. Lakini tangu kuumbwa kwa ulimwengu, mambo haya yamekuwa rahisi kwa watu kuyaona. Maana yake ni kuwa, watu wanaweza kumwelewa Mungu kwa kuangalia yale aliyoumba. Hivyo watu hawana udhuru kwa uovu wanaotenda.
21Watu walimjua Mungu, lakini hawakumheshimu kama Mungu. Na hawakumpa shukrani. Badala yake waliyageukia mambo ya hovyo yasiyo na manufaa. Akili zao zilichochanganyikiwa zilijaa giza.
22Walisema kuwa wana hekima, lakini wakawa wajinga.
23Hawakuuheshimu ukuu wa Mungu, anayeishi milele. Wakaacha kumwabudu Mungu wakaanza kuabudu sanamu, vitu vilivyotengenezwa vikaonekana kama wanadamu, ambao wote mwisho hufa, au kwa mfano wa ndege na wanyama wanaotembea na wanaotambaa.
24Hivyo Mungu akawaacha wazifuate tamaa zao chafu. Wakawa najisi na wakaivunjia heshima miili yao kwa njia za uovu walizotumia.
25Waliibadili kweli kuhusu Mungu kwa uongo. Wakasujudu na kuabudu vitu alivyoviumba Mungu badala ya kumwabudu Mungu aliyeviumba vitu hivyo. Yeye ndiye anayepaswa kusifiwa milele yote. Amina.
26Hivyo, kwa kuwa watu hawakumheshimu Mungu, Mungu akawaacha wafuate tamaa zao za aibu. Wanawake wao wakabadili namna ya kujamiiana na wakawatamani wanawake wenzao na wakajamiiana wao kwa wao.
27Wanaume wakafanya vivyo hivyo. Wakaacha kujamiiana na wanawake kwa mfumo wa asili, wakaanza kuwawakia tamaa wanaume wenzao. Wakafanya mambo ya aibu na wanaume na wavulana. Wakajiletea aibu hii juu yao wenyewe, wakapata yale waliyostahili kwa kutelekeza kweli.
28Watu hawa waliona kuwa haikuwa muhimu kwao kumkubali Mungu katika fikra zao. Hivyo Mungu akawaacha wayafuate mawazo yao mabaya. Hivyo hufanya mambo ambayo mtu yeyote hapaswi kufanya.
29Maisha yao yamejaa kila aina ya matendo mabaya, uovu, tamaa na chuki. Wamejaa wivu, uuaji, ugomvi, uongo na hamu ya kuwadhuru wengine. Wanasengenya
30na kusemana maovu wao wenyewe. Wanamchukia Mungu. Ni wakorofi, wana kiburi na hujivuna. Hubuni njia za kufanya maovu. Hawawatii wazazi wao.
31Ni wapumbavu, hawatimizi ahadi zao. Hawawaoneshi wema wala huruma wengine.
32Wanajua amri ya Mungu kuwa yeyote anayeishi kwa namna hiyo lazima afe. Lakini si tu kwamba wanaendelea kufanya mambo haya wenyewe, bali wanakubaliana na wengine wanaofanya mambo hayo.