Warumi 9

Warumi 9

Mungu na Wayahudi

1Nazungumza nayi sasa kama mmojawapo niliye wa Kristo. Hivyo mnaweza kuwa na uhakika kuwa sisemi uongo. Dhamiri yangu, inayotawaliwa na Roho Mtakatifu, inakubali kwamba ninayowaambia sasa ni kweli.

2Nimejawa na huzuni na maumivu ya moyoni yasiyokwisha

3kwa ajili ya watu wangu. Wao ni kaka na dada zangu katika mwili. Natamani ningeweza kuwasaidia. Ningekuwa tayari pia kuomba kupokea laana ya kutengwa na Kristo kama hiyo itaweza kuwasaidia.

4Ni Waisraeli, watoto waliochaguliwa na Mungu. Wameushuhudia utukufu wa Mungu na wanashiriki maagano aliyofanya Mungu na watu wake. Mungu aliwapa Sheria ya Musa, ibada ya Hekalu, na ahadi zake.

5Ni wazaliwa wa mababa zetu wakuu, na ni familia ya kidunia ya Masihi, ambaye ni Mungu aliye juu ya vyote. Yeye asifiwe milele! Amina.[#9:5 Kwa maana ya kawaida, “Kristo”, tafsiri ya Kiyunani kwa neno “Masihi”. Tazama na katika Orodha ya Maneno.; #9:5 Au “Masihi. Mungu, anayevitawala vitu vyote, asifiwe milele!”]

6Sina maana kuwa Mungu alishindwa kutimiza ahadi yake kwa Wayahudi. Lakini kwa hakika ni baadhi tu ya Waisraeli ndiyo watu wa Mungu.[#9:6 Kwa maana ya kawaida, “Israeli”, watu aliowachagua Mungu ili kuleta baraka ulimwenguni.]

7Na hivyo ni baadhi tu ya watoto wa Abrahamu ndiyo wazaliwa wake halisi. Hivi ndivyo Mungu alimwambia Abrahamu: “Wazaliwa wako halisi watakuwa wale waliotoka kwa Isaka.”[#Mwa 21:12]

8Hii ina maana kuwa si watoto wote wa Abrahamu walio watoto halisi wa Mungu. Wazaliwa halisi wa Ibrahamu ni wale wanaofanyika watoto wa Mungu kwa sababu ya agano ambalo Mungu alililiweka na Ibrahamu.

9Hivi ndivyo Mungu alivyosema katika agano hilo: “Wakati kama huu mwaka ujao nitakujia tena, na Sara mke wako atazaa mwana.”[#Mwa 18:10,14]

10Na si hivyo tu. Kitu kama hicho kilimtokea Rebeka ambaye baada ya kupata mimba ya wana wawili mapacha waliotokana na baba mmoja, baba yetu Isaka.

11-12Ndiyo, kabla ya kuzaliwa wana hao mapacha, Mungu alimwambia Rebeka, “Mwana mkubwa atamtumikia mdogo.” Hii ilikuwa kabla wavulana hawa hawajatenda jambo lolote jema au baya. Mungu alisema hivi kabla hawajazaliwa ili kwamba mvulana ambaye Mungu alimtaka atachaguliwa kutokana na mpango wa Mungu mwenyewe. Mvulana huyu alichaguliwa kwa sababu ndiye ambaye Mungu alitaka kumwita, si kwa sababu ya jambo lolote walilofanya wavulana hao.[#Mwa 25:23]

13Kama Maandiko yanavyosema, “Nilimpenda Yakobo lakini nilimchukia Esau.”[#Mal 1:2-3]

14Namsikia mtu akiuliza, “Hivyo hii ina maana gani? Je! Mungu si mwenye haki?” Hapana!

15Mungu alimwambia Musa, “Nitampa rehema yeyote ninayetaka kumpa rehema. Nitamhurumia yeyote ninayemchagua.”[#Kut 33:19]

16Hivyo Mungu atamchagua yeyote anayeamua kumpa rehema pasipo kujali watu wanataka nini ama kwa jinsi gani wanapiga mbio.

17Katika Maandiko Mungu anamwambia Farao: “Nilikuweka uwe mfalme kwa kusudi hili hasa: kuonesha nguvu zangu kupitia kwako. Nilitaka jina langu litangazwe ulimwenguni kote”[#Kut 9:16]

18Hivyo Mungu huwarehemu wale anaotaka kuwarehemu na huwafanya jeuri wale anaotaka wawe jeuri.

19Hivyo utaniuliza, “Ikiwa unayosema ni kweli, kwa nini Mungu amlaumu mtu yeyote kwa kufanya makosa? Hayupo anayeweza kukataa kufanya yale anayotaka Mungu, Je! yupo?”

20Hilo si la kuuliza. Wewe ni mwanadamu tu na huna haki ya kumhoji Mungu. Chungu hakiwezi kumhoji aliyekifinyanga. Hakiwezi kusema, “Kwa nini ulinifinyanga hivi?”

21Yeye aliyefinyanga chungu anaweza kufinyanga kitu chochote anachotaka. Anautumia udongo ule ule wa mfinyanzi kufinyanga vitu mbalimbali. Anaweza kufinyanga kitu kimoja kwa makusudi maalumu na kingine kwa matumizi ya kila siku.

22Ni kwa jinsi hiyo hiyo Mungu amefanya. Alitaka kuionesha hasira yake na kuwafanya watu waone nguvu zake. Lakini kwa uvumilivu wake aliwastahimili wale waliomuudhi, watu waliokuwa tayari kuangamizwa.

23Alingoja kwa uvumilivu ili aweze kuutangaza utajiri wa utukufu wake kwa watu aliowachagua wapokee rehema zake. Mungu alikwishawaandaa kuushiriki utukufu wake.

24Sisi ndiyo watu hao, ambao Mungu alituchagua si tu kutoka kwa Wayahudi lakini pia kutoka kwa wale wasio Wayahudi.

25Kama Mungu anavyosema katika kitabu cha Hosea,

“Watu wasiokuwa wangu,

nitasema ni watu wangu.

Na watu ambao sikuwapenda,

nitasema ni watu ninaowapenda.

26Na pale Mungu aliposema zamani:

‘Ninyi si watu wangu’;

hapo wataitwa watoto wa Mungu aliye hai.”

27Na Isaya huililia Israeli:

“Wako watu wengi sana wa Israeli,

kuliko mchanga ulio pwani ya baharini.

Lakini wachache wao watakaookolewa.

28Ndiyo, Bwana atakamilisha kwa haraka

aliyosema atayafanya duniani.”

29Ni kama vile alivyosema Isaya:

“Ikiwa Bwana Mwenye Uweza wote

asingewaruhusu watu wachache wakaishi,

tungekuwa tumeangamizwa kabisa,

kama vile miji miovu ya Sodoma, na Gomora.”

30Hivyo haya yote yanamaanisha nini? Je! tunasema kwamba watu wasio Wayahudi walifanikiwa kukipata kibali cha Mungu, hata kama hawakuwa wakijaribu kukipata kibali hicho? Ndiyo. Walipata kibali hicho kwa sababu ya imani kwa Mungu.

31Na vipi kuhusu watu wa Israeli? Wao walitaka kujipatia kibali cha Mungu kwa kuifuata sheria. Je! tunasema kuwa hawakufanikiwa?

32Ndiyo, na sababu yake ni hii: Walijitahidi kukipata kwa kufanya kwa usahihi mambo yote yaliyoamriwa katika sheria badala ya kumtumaini Mungu. Walijikwaa kwenye jiwe linalowafanya watu waanguke.

33Maandiko yanazungumza kuhusu jiwe hilo:

“Tazama, ninaweka jiwe katika Sayuni litakalowafanya watu wajikwae.

Ni mwamba utakaowaangusha watu.

Lakini yeyote atakayemtumaini yeye

hataaibika kamwe.”

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi Toleo la Awali © 2017 Bible League International
Published by: Bible League International