Danieli 12

Danieli 12

Wakati wa mwisho

1“ ‘Wakati huo, Mikaeli, malaika mkuu, aliye mlinzi wa watu wako, atatokea. Ndipo kutakuwa na wakati wa taabu sana kuliko nyakati nyingine zote tangu mataifa yalipoanza kuwako duniani. Lakini, wakati huo, kila mmoja wa watu wako ambaye jina lake limeandikwa katika kitabu cha uhai, ataokolewa.[#Taz Mat 24:21; Marko 13:19; Ufu 7:14; 12:7]

2Wengi wa wale ambao wamekwisha kufa, watafufuka; wengine watapata uhai wa milele, na wengine watapata uhai na kudharauliwa milele.[#Taz Isa 26:19; Mat 25:46; Yoh 5:29]

3Wale wenye hekima watangaa kama anga angavu, na wale waliowaongoza wengine kutenda mema, watangaa kama nyota milele.

4Ila sasa, Danieli, weka siri mambo hayo; kifunge kitabu na kukitia mhuri mpaka wakati wa mwisho utakapofika. Wengi watakimbilia huko na huko, na maarifa yataongezeka.’”[#Taz Ufu 22:10]

5“Kisha, mimi Danieli nikatazama, nikaona watu wawili wamesimama penye kingo za mto; mmoja upande huu na mwingine upande wa pili.

6Nikamwuliza yule aliyesimama upande wa juu wa mto, amevaa mavazi ya kitani, mambo haya ya kutisha yatadumu mpaka lini ndipo yaishe?

7Yule mtu aliyesimama upande wa juu wa mto, amevaa mavazi ya kitani, akainua mikono yake yote miwili kuelekea mbinguni. Kisha nikamsikia akiapa kwa jina la yule aishiye milele: ‘Itakuwa muda wa nyakati tatu na nusu. Wakati mateso ya watu watakatifu yatakapokomeshwa, mambo haya yote yatakuwa yametimia.’[#Taz Ufu 10:5; 12:14]

8Nilisikia lakini sikuelewa. Ndipo, nikamwuliza, ‘Bwana wangu, mwisho wa mambo haya yote utakuwaje?’

9Akanijibu, ‘Danieli, sasa nenda zako, kwani maneno haya ni siri na yamefungwa kwa kutiwa mhuri mpaka wakati wa mwisho.

10Watu wengi wataondolewa uchafu, watatakaswa na kusafishwa. Lakini watu waovu wataendelea kutenda uovu. Hakuna hata mmoja wa hao waovu atakayeelewa; wenye hekima ndio watakaoelewa.[#Taz Ufu 22:11]

11“ ‘Tangu wakati wa kukomeshwa kwa sadaka za kuteketezwa kila siku, yaani kutoka wakati ule chukizo haribifu litakaposimamishwa itakuwa muda wa siku 1,290.[#Taz Dan 9:27; 11:31; Mat 24:15; Marko 13:14]

12Heri yao watakaostahimili mpaka siku zile 1,335 zitakapotimia.

13“ ‘Lakini wewe, ee Danieli, jiendee, ukapumzike kaburini, na wakati huo utakapotimia, utafufuka na kupata tuzo lako.’”

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania