The chat will start when you send the first message.
1Hapo zamani, Mungu alisema na babu zetu mara nyingi kwa namna nyingi kwa njia ya manabii,
2lakini siku hizi za mwisho, amesema nasi kwa njia ya Mwanae. Yeye ndiye ambaye kwa njia yake Mungu aliumba ulimwengu, akamteua avimiliki vitu vyote.
3Yeye ni mngao wa utukufu wa Mungu, na mfano kamili wa hali ya Mungu mwenyewe, akiutegemeza ulimwengu kwa neno lake lenye nguvu. Baada ya kuwatakasa binadamu dhambi zao, ameketi huko juu mbinguni, upande wa kulia wa Mungu Mkuu.
4Mwana ni mkuu kuliko malaika, kama vile jina alilopewa na Mungu ni kuu kuliko jina lao.
5Maana Mungu hakumwambia kamwe hata mmoja wa malaika wake:[#Taz Zab 2:7]
“Wewe ni Mwanangu;
mimi leo nimekuwa Baba yako.”
Wala hakusema juu ya malaika yeyote:
“Mimi nitakuwa Baba yake,
naye atakuwa Mwanangu.”
6Lakini Mungu alipokuwa anamtuma Mwanae, mzaliwa wa kwanza, ulimwenguni alisema:
“Malaika wote wa Mungu na wamwabudu.”
7Lakini kuhusu malaika, alisema:[#Taz Zab 104:4]
“Amewafanya malaika wake kuwa upepo,
na wahudumu wake ndimi za moto.”
8Lakini kuhusu Mwana, Mungu alisema:[#Taz Zab 45:6-7]
“Kiti chako cha enzi, ee Mungu, chadumu milele na milele!
Wewe wawatawala watu wako kwa haki.
9Wewe wapenda uadilifu na kuchukia uovu.
Ndiyo maana Mungu, Mungu wako, amekuweka wakfu
na kukumiminia furaha kubwa kuliko wenzako.”
10Na tena:[#Taz Zab 102:25-27]
“Bwana, wewe uliumba dunia hapo mwanzo,
mbingu ni kazi ya mikono yako.
11Hizo zitatoweka, lakini wewe wabaki daima,
zote zitachakaa kama vazi.
12Utazikunjakunja kama koti,
nazo zitabadilishwa kama vazi.
Lakini wewe ni yuleyule daima,
na maisha yako hayatakoma.”
13Mungu hakumwambia kamwe hata mmoja wa malaika wake:[#Taz Zab 110:1]
“Keti upande wangu wa kulia,
mpaka niwaweke adui zako chini ya miguu yako.”
14Malaika ni nini ila roho wanaomtumikia Mungu na ambao hutumwa kuwasaidia wale watakaopokea wokovu?