Isaya 27

Isaya 27

1Siku hiyo, Mwenyezi-Mungu atautwaa upanga wake mkubwa, mkali na imara, na kuliadhibu dude Lewiyathani joka lirukalo na danganyifu; Mwenyezi-Mungu ataliua joka liishilo baharini.[#27:1 Taz Yobu 41:1; Zab 74:14; 104:26; #27:1 Joka la kutisha katika hadithi za kale, hapa latumiwa kutajia mataifa yaliyokandamiza Israeli.]

2Siku hiyo, Mwenyezi-Mungu atasema hivi:

“Imbeni utenzi wa shamba langu zuri la mizabibu!

3Mimi, Mwenyezi-Mungu, ni mkulima wake;

nalimwagilia maji kila wakati,

ninalilinda usiku na mchana,

lisije likaharibiwa na mtu yeyote.

4Silikasirikii tena shamba hili;

kama miiba na mbigili ingelilivamia,

mimi ningepambana nayo na kuichoma moto.

5Maadui za watu wangu wakitaka ulinzi wangu,

basi, na wafanye amani nami;

naam, wafanye amani nami.”

6Itakuja siku wazawa wa Yakobo watashika mizizi;

naam, watu wa Israeli watachanua na kuchipua,

na kuijaza dunia yote kwa matunda.

7Mungu hakuwaadhibu Waisraeli vikali

kama alivyowaadhibu maadui wake;

Waisraeli waliopotea vitani,

ni wachache kuliko wale wa maadui zake.

8Aliwaadhibu watu wake kwa kuwapeleka uhamishoni.

Wakati wa upepo mkali wa mashariki,

aliwaondoa kwa kipigo kikali.

9Hivi ndivyo uovu wa wazawa wa Yakobo utakavyoondolewa,

hivi ndivyo dhambi yake itakavyofutwa kabisa:

Ataziharibu madhabahu za miungu;

mawe yake yatasagwasagwa kama chokaa;

Ashera, wala madhabahu za kufukizia ubani hazitabaki.

10Mji ule wa ngome sasa umekuwa mtupu,

umeachwa na kuhamwa kama jangwa,

humo ndama wanalisha na kupumzika.

11Matawi ya miti yamekauka na kuvunjika;

kina mama huyaokota wakawashia moto.

Watu hawa hawajaelewa kitu,

kwa hiyo Mungu, Muumba wao, hatawahurumia,

yeye aliyewafanya, hatawafadhili.

12Siku hiyo, kutoka mto Eufrate hadi mpakani mwa Misri, Mwenyezi-Mungu ataipura nafaka yake, nanyi Waisraeli mtakusanywa mmojammoja.

13Siku hiyo, tarumbeta kubwa itapigwa na watu wote wa Israeli waliopotea nchini Ashuru au waliotawanywa nchini Misri watarudi na kumwabudu Mwenyezi-Mungu juu ya mlima mtakatifu huko Yerusalemu.

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania