The chat will start when you send the first message.
1Kando ya mito ya Babuloni, tulikaa,
tukawa tunalia tulipokumbuka Siyoni.
2Katika miti ya nchi ile,
tulitundika zeze zetu.
3Waliotuteka walitutaka tuwaimbie;
watesi wetu walitutaka tuwafurahishe:
“Tuimbieni mojawapo ya nyimbo za Siyoni!”
4Twawezaje kuimba wimbo wa Mwenyezi-Mungu
katika nchi ya kigeni?
5Ee Yerusalemu, kama nikikusahau,
mkono wangu wa kulia na ukauke!
6Ulimi wangu na uwe mzito,
kama nisipokukumbuka wewe, ee Yerusalemu;
naam, nisipokuthamini kuliko furaha yangu kubwa!
7Ee Mwenyezi-Mungu, usisahau waliyotenda Waedomu,
siku ile Yerusalemu ilipotekwa;
kumbuka waliyosema:
“Bomoeni mji wa Yerusalemu!
Ngoeni hata na misingi yake!”
8Ee Babuloni, utaangamizwa![#Taz Ufu 18:6]
Heri yule atakayekulipiza mabaya uliyotutenda!
9Heri yule atakayewatwaa watoto wako
na kuwapondaponda mwambani!