The chat will start when you send the first message.
1Mwenyezi-Mungu akujibu uwapo taabuni;
jina la Mungu wa Yakobo likulinde.
2Akupelekee msaada kutoka hekaluni mwake;
akutegemeze kutoka mlima Siyoni.
3Azikumbuke sadaka zako zote;
azikubali tambiko zako za kuteketezwa.
4Akujalie unayotamani moyoni mwako,
aifanikishe mipango yako yote.
5Tutashangilia kwa ajili ya ushindi wako;
tutatweka bendera kulitukuza jina la Mungu wetu.
Mwenyezi-Mungu akutimizie maombi yako yote!
6Najua Mwenyezi-Mungu atamsaidia mfalme aliyemteua,
atamjibu kutoka patakatifu pake mbinguni;
kwa mkono wake wa kulia atamjalia ushindi mkubwa.
7Wengine hujigamba kwa magari ya vita;
wengine hujigamba kwa farasi wao.
Lakini sisi twajivunia Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu.
8Hao watajikwaa na kuanguka;
lakini sisi tutainuka na kusimama imara.
9Umjalie mfalme ushindi, ee Mwenyezi-Mungu;
utujibu wakati tunapokuomba.