The chat will start when you send the first message.
1Mbona, ewe jitu, wajivunia ubaya wako
dhidi ya wenye kumcha Mungu?
2Kila wakati unawaza maangamizi;
ulimi wako ni kama wembe mkali!
Unafikiria tu kutenda mabaya.
3Wewe wapenda uovu kuliko wema,
wapenda uongo kuliko ukweli.
4Ewe mdanganyifu mkuu,
wapenda mambo ya kuangamiza wengine.
5Kwa hivyo Mungu atakuangamiza milele,
atakunyakua na kukuondoa nyumbani mwako;
atakungoa katika nchi ya walio hai.
6Waadilifu wataona hayo na kuogopa,
kisha watakucheka na kusema:
7“Tazameni yaliyompata mtu huyu!
Yeye hakutaka Mungu awe kimbilio lake;
bali alitegemea wingi wa mali yake,
na kutafuta humo usalama wake!”
8Lakini mimi ni kama mzeituni mbichi,
unaostawi katika nyumba ya Mungu.
Nazitegemea fadhili zake milele na milele.
9Ee Mungu, nitakushukuru daima,
kwa ajili ya mambo uliyofanya.
Nitatangaza kwamba wewe ni mwema,
mbele ya watu wako waaminifu.