1 Samueli 22

1 Samueli 22

Shauli anawaua makuhani

1Daudi aliondoka huko akakimbilia kwenye pango karibu na mji wa Adulamu. Kaka zake na ndugu zake wengine waliposikia kwamba alikuwa hapo, wote walikwenda kuungana naye.[#22:1 Taz Zab 57 (Maneno yanayotangulia Zaburi yenyewe au “kichwa cha Zaburi” katika Kiebrania; Zab 142 (Maneno yanayotangulia Zaburi yenyewe au “kichwa cha Zaburi” katika Kiebrania).; #22:1 Mahali yapata kilomita 32 kusini-magharibi ya Gibea na kilomita 17 Kusini-Mashariki ya Gathi.]

2Watu wote waliokandamizwa au waliokuwa na madeni, au wale ambao hawakuridhika walijumuika na Daudi. Jumla yao ilikuwa watu kama 400, naye akawa kiongozi wao.

3Kutoka huko, Daudi alikwenda mpaka huko Mizpa nchini Moabu. Akamwambia mfalme wa Moabu, “Nakuomba, baba yangu na mama yangu wakae hapa kwako mpaka nijue Mungu atanifanyia nini.”[#22:3 Haifahamiki dhahiri mahali hapo palikuwa wapi. Tunajua Moabu lilikuwa eneo mashariki ya Bahari ya Chumvi. Wamoabu walikuwa maadui wa Waisraeli (Amu 10:11-18; 1Sam 14:47-48). Lakini huenda Daudi alifikiri mfalme wa Wamoabu angemuunga mkono kwa vile naye alikuwa na uhasama na Shauli. Katika Rut 4:13-17 Daudi ana uhusiano wa damu na Wamoabu kupitia kwa Ruthu ambaye alikuwa Mmoabu.]

4Basi, Daudi aliwaacha wazazi wake wakae na mfalme wa Moabu; nao wakakaa kwake muda wote ambao Daudi alikuwa ngomeni.

5Kisha nabii Gadi akamwambia Daudi, “Usikae hapa ngomeni, ondoka mara moja uende katika nchi ya Yuda.” Basi, Daudi akaondoka, akaenda kwenye msitu wa Herethi.[#22:5 Anatajwa kwa mara ya kwanza hapa; Mungu atamtumia nyakati nyingine kumwongoza Daudi (2Sam 24:11-19; 2Nya 29:25). Katika 1 Nya 29:29 inasemwa kwamba yeye Gadi pamoja na Samueli na Nathani aliandika historia ya utawala wa Daudi.]

6Siku moja, Shauli alikuwa Gibea, amekaa chini ya mkwaju, mlimani, huku akiwa na mkuki wake mkononi na watumishi wake walikuwa wamesimama kandokando yake. Basi akaambiwa kwamba Daudi na watu wake wameonekana.[#22:6 Watawala na wafalme wa kale mara kwa mara wanasemekana kuketi chini ya mti fulani wakati wa kuamua mambo ya watu au kutoa ilani maalumu.]

7Naye Shauli akawaambia watumishi wake, “Sasa nyinyi watu wa kabila la Benyamini nisikilizeni, je, mnadhani huyu Daudi mwana wa Yese atampa kila mmoja wenu mashamba na mashamba ya mizabibu? Au je, mnadhani atamfamya kila mmoja wenu kamanda wa maelfu au kamanda wa mamia ya majeshi?[#22:7 Shauli alikuwa pia Mbenyamini (taz 9-12; 10:21) hali Daudi alikuwa wa kabila la Yuda (taz 16:1; 2Sam 2:4 maelezo). Maneno ya Shauli hapa yanadhihirisha kwamba yeye aliwapendelea watu wa kabila lake mwenyewe kwa kuwapa mashamba.; #22:7 Yaani, Daudi. Huenda Shauli hapa anaacha kutaja jina la Daudi kwa madharau.]

8Kwa nini nyinyi nyote mmekula njama dhidi yangu? Hakuna hata mmoja wenu anayeniambia habari hii, wakati mwanangu afanyapo mapatano na mtoto wa Yese. Tena, kwa nini hakuna hata mmoja kati yenu anayesikitika au kunieleza kuwa mwanangu mwenyewe anamchochea mtumishi wangu dhidi yangu akinivizia kama ilivyo leo hii?”

9Ndipo Doegi, Mwedomu, ambaye alikuwa amesimama karibu na watumishi wa Shauli akasema, “Nilimwona mwana wa Yese akija Nobu kwa kuhani Ahimeleki mwana wa Ahitubu.

10Ahimeleki alimwombea Daudi kwa Mwenyezi-Mungu, akampa chakula na upanga wa yule Mfilisti Goliathi.”[#22:9-10 Taz Zab 52 (kichwa cha Zaburi hiyo Kiebrania).]

11Mfalme Shauli akaagiza kuhani Ahimeleki mwana wa Ahitubu, pamoja na watu wote wa jamaa ya baba yake ambao walikuwa makuhani huko Nobu waitwe. Wote wakamwendea mfalme Shauli.

12Shauli akasema, “Sasa sikiliza wewe mwana wa Ahitubu.” Ahimeleki akamjibu, “Naam, bwana.”

13Shauli akamwambia, “Kwa nini wewe na Daudi mwana wa Yese, mmekula njama dhidi yangu? Kwa nini ulimpatia mikate na upanga, halafu ukamwombea kwa Mungu? Kwa sababu hiyo, leo ameniasi na ananivizia.”

14Ahimeleki akamjibu, “Kati ya watumishi wako, Daudi ndiye ofisa wa kuaminika kuliko wote. Yeye ni mkwe wako wewe mfalme mwenyewe, kapteni wa kikosi chako cha ulinzi na anaheshimika kuliko wote nyumbani mwako.

15Leo, sio mara ya kwanza kumwomba Mungu shauri kwa ajili yake. Mfalme, usinishuku mimi wala mtu yeyote katika jamaa ya baba yangu juu ya njama hizo. Mimi mtumishi wako, sijui lolote, liwe kubwa au dogo juu ya jambo hilo.”

16Lakini mfalme Shauli akamwambia, “Ahimeleki, hakika utauawa, wewe na jamaa yote ya baba yako.”

17Shauli akawaambia walinzi waliokuwa wamesimama kandokando yake, “Geukeni na kuwaua makuhani wa Mwenyezi-Mungu, maana wao wanapatana na Daudi; walijua kuwa ametukimbia wala hawakuniarifu.” Lakini walinzi hao hawakuinua mikono yao ili kuwaua makuhani wa Mwenyezi-Mungu.

18Kwa hiyo, mfalme Shauli akamwambia Doegi, “Wewe geuka ukawaue makuhani.” Doegi, Mwedomu, akaenda na kuwaua makuhani wote. Siku hiyo, Doegi aliua makuhani themanini na watano ambao huvaa vizibao vya kikuhani vya kitani.[#22:17-18 Watu wa Shauli walikataa amri yake ya kuwaua makuhani kwani walimtii Mungu zaidi kuliko Shauli. Doegi lakini hakuwa Mwisraeli na alikuwa mwaminifu kwa Shauli tu; kwa hiyo hakuwa na woga wowote ule kutii amri ya Shauli ya kuwaua hao makuhani.]

19Kisha aliwaua kwa makali ya upanga wakazi wote wa Nobu, mji wa makuhani, wanaume na wanawake, watoto wadogo na wanyonyao, ng'ombe, punda na kondoo.

20Lakini Abiathari, mmoja wa watoto wa kiume wa Ahimeleki, mwana wa Ahitubu, aliponyoka akakimbilia kwa Daudi.[#22:20 Huyu alipata kuwa kuhani wakati Daudi alipokuwa mfalme (1Sam 23:6; 2Sam 20:25), lakini baadaye aliondolewa na Solomoni (1Fal 2:26-27).]

21Abiathari alimweleza Daudi kuwa Shauli amewaua makuhani wa Mwenyezi-Mungu.

22Naye Daudi akamwambia Abiathari, “Nilijua wazi siku ile nilipomwona Doegi Mwedomu, kuwa atamwambia Shauli. Hivyo, mimi nimesababisha vifo vya watu wa jamaa ya baba yako.[#22:22 Hapa Daudi anakiri makosa yake na hivyo kuonesha kile ambacho chaweza kusemwa kuwa ni tabia ya pekee ya unyenyekevu.]

23Wewe, kaa pamoja nami, wala usiogope. Maana, anayetafuta kuyaangamiza maisha yangu anatafuta hata yako pia. Ukiwa pamoja nami, uko salama kabisa.”

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania