2 Samueli 1

2 Samueli 1

Daudi anahabarishwa juu ya kifo cha Shauli

1Baada ya kifo cha Shauli, Daudi alirudi baada ya kuwashinda Waamaleki, akakaa Siklagi kwa muda wa siku mbili.[#1:1-27 Kwa sura hii ya kwanza tunafikia mwisho wa sehemu kubwa ambayo ilianza katika 1Sam 16. Kwamba sehemu hiyo yenye umoja imeendelea mpaka sura hii ya kwanza ya kitabu cha pili ni mojawapo ya sababu zinaoonesha kwamba vitabu hivi viwili vya Samueli hapo awali vilikuwa kitabu kimoja. Kitabu cha kwanza kilitilia mkazo mambo ya Shauli; hiki cha pili kinazingatia hasa mambo ya Daudi ambaye ndiye mhusika mkuu katika kitabu hiki.; #1:1 Mtindo huu wa namna ya kusema unaonesha mara nyingi kwamba habari zinazosimuliwa zinaendeleza habari au mambo yaliyotajwa katika sehemu au kitabu kilichotangulia (Yos 1:1; Amu 1:1). Hapa, yamkini panaonesha pia kwamba vitabu viwili vya Samueli hapo awali vilikuwa kitabu kimoja.; #1:1 Rejea 1Sam 30. Taz Kut 17:8 maelezo.; #1:1 Taz 1Sam 27:6.]

2Siku iliyofuata, mtu mmoja kutoka kambi ya Shauli, mavazi yake yakiwa yamechanwa kwa huzuni na akiwa na mavumbi kichwani alimwendea Daudi. Alipomfikia Daudi, alijitupa chini mbele yake akamsujudia.[#1:2 Rejea Yos 7:6; 1Sam 4:12.]

3Daudi akamwambia, “Unatoka wapi?” Naye akamwambia, “Nimetoroka kutoka kambi ya Waisraeli.”

4Daudi akamwambia, “Niambie mambo yalivyokuwa huko.” Yule mtu akamjibu, “Watu wetu wameyakimbia mapigano na wengi wetu wameuawa. Zaidi ya hayo, Shauli na mwanawe Yonathani pia wameuawa.”

5Daudi akamwuliza yule kijana, “Unajuaje kuwa Shauli na Yonathani mwanawe wamekufa?”

6Yule kijana akamjibu, “Kwa bahati, nilikuwapo mlimani Gilboa. Nilimwona Shauli ameegemea mkuki wake na magari ya wapandafarasi ya adui zake yalikuwa yanamsonga sana.[#1:6-10 Habari hii juu ya kifo cha Shauli ina mengine ya ziada ambayo hayamo katika lile simulizi la 1Sam 31:3-5 (rejea 1 Nya 10:6-10). Katika sehemu hiyo ya 1 Samueli tunaambiwa kwamba Shauli alijiua mwenyewe. Yamkini huyo Mmaleki, kwa kutia chumvi kidogo, alitazamia kupata tuzo kutoka kwa Daudi lakini haikuwa hivyo kama aya zinazofuata zinavyosimulia.]

7Shauli alipotazama nyuma, aliniona, akaniita. Nilipoitika,

8yeye aliniuliza mimi ni nani, nami nikamwambia kuwa mimi ni Mmaleki.[#1:8 Waamaleki walikuwa adui wa Waisraeli tangu zamani (rejea Kut 17:8-14; Kumb 25:17-19; 1Sam 15:2) naye Daudi mwenyewe hapo kabla alikwisha pigana nao (1Sam 30:1-5).]

9Hapo, akaniambia, ‘Karibia uniue maana nimejeruhiwa vibaya na maumivu ni makali. Lakini bado ningali hai’.

10Hivyo, nilikwenda karibu naye na kumuua, kwa sababu nilikuwa na uhakika kuwa akianguka chini, hataweza kuishi zaidi. Lakini taji iliyokuwa kichwani pake na kikuku kilichokuwa mkononi mwake, vyote nimekuletea wewe, bwana wangu.”

11Daudi akayashika mavazi yake na kuyararua kwa huzuni. Hata watu waliokuwa pamoja na Daudi wakafanya vivyo hivyo.

12Wakaomboleza, wakalia na kufunga mpaka jioni kwa ajili ya Shauli, Yonathani mwanawe, na nchi ya Waisraeli, watu wa Mwenyezi-Mungu, kwa kuwa wengi wao waliuawa vitani.[#1:12 Jambo la kufunga au kuacha kula chakula (tofauti na tamaduni za makabila mengine katika Afrika) lilikuwa la kawaida wakati wa kilio huko Mashariki ya Kati ya Kale (rejea 1Sam 31:13; Yoeli 2:12).]

13Daudi akamwuliza yule kijana aliyempasha habari, “Unatoka wapi?” Yeye akajibu, “Mimi ni Mmaleki, lakini ninaishi katika nchi yako kama mgeni.”

14Daudi akamwuliza, “Ilikuwaje wewe hukuogopa kuunyosha mkono wako na kumuua mtu aliyeteuliwa na Mwenyezi-Mungu kwa kupakwa mafuta?”[#1:14 Tafsiri ya maneno mawili katika Kiebrania ambayo neno kwa neno ni “Mpakwa wa Mwenyezi-Mungu”. Kutokana na kupakwa mafuta ya zeituni (taz Zab 2:2 maelezo), mfalme aliwekwa wakfu na kuwa mtu aliyetengwa kwa ajili ya Mungu (na hivyo mtakatifu). Taz pia 1Sam 24:6-7; 26:9 ambapo hata Daudi mwenyewe anamtambua Shauli kuwa hivyo.]

15Kisha, Daudi akamwita mmoja wa vijana wake akamwambia, “Muue mtu huyu!” Yule kijana alimpiga yule Mmaleki, naye akafa.

16Daudi akasema, “Uwajibike wewe mwenyewe kwa kifo chako, maana umejishuhudia wewe mwenyewe kwa mdomo wako ukisema, ‘Nimemuua mtu aliyeteuliwa na Mwenyezi-Mungu kwa kupakwa mafuta.’”

Daudi aomboleza kifo cha Shauli na Yonathani

17Daudi aliimba ombolezo lifuatalo kwa ajili ya Shauli na mwanawe Yonathani.

18Daudi alisema watu wa Yuda wafundishwe ombolezo hilo, nalo limeandikwa katika kitabu cha Yashari. Daudi aliimba,[#1:18 Kiebrania ni neno lenye maana ya “upinde”. Wengine wamejaribu kufafanua maana ya neno hili kuwa kwamba Daudi alikuwa anadokezea watu wafundishwe kuwa mafundi wa kurusha mishale.; #1:18 Au “Kitabu cha Waadilifu” au, “Kitabu cha Wanyofu”. Wengine wanafikiri kitabu hicho kilikuwa mkusanyo wa tenzi za kale za vita (Yos 10:13 maelezo).]

19“Walio fahari yako, ee Israeli,[#1:19 Yamkini yahusu Shauli na Yonathani.]

wameuawa milimani pako.

Jinsi gani mashujaa walivyoanguka!

20Jambo hilo msiuambie mji wa Gathi

wala katika mitaa ya Ashkeloni.

La sivyo, wanawake Wafilisti watashangilia,

binti za wasiotahiriwa, watafurahi.

21“Enyi milima ya Gilboa,

msiwe na umande au mvua juu yenu.

Wala mashamba yenu daima yasitoe chochote.

Maana huko ngao za shujaa zilitiwa najisi,

ngao ya Shauli haikupakwa mafuta.

22“Upinde wa Yonathani kamwe haukurudi nyuma,

upanga wa Shauli kamwe haukurudi bure,

daima ziliua wengi.

Naam, ziliua mashujaa.

23“Shauli na Yonathani,

watu wa ajabu na wakupendeza.

Maishani na kifoni hawakutengana.

Walikuwa wepesi kuliko tai,

naam, wenye nguvu kuliko simba.

24“Wanawake wa Israeli, mlilieni Shauli!

Aliwavika mavazi mekundu ya fahari,

aliyatarizi mavazi yenu kwa dhahabu.

25“Jinsi gani mashujaa walivyoanguka!

Wamekufa wakiwa katika mapambano.

“Yonathani analala,

akiwa ameuawa milimani.

26Nasikitika kwa ajili yako, ndugu yangu Yonathani.

Umekuwa kwangu daima mtu wa kupendeza,

pendo lako kwangu limekuwa la ajabu,

la ajabu kuliko la mwanamke.

27“Jinsi gani mashujaa wameanguka,

na silaha zao zimeachwa, hazina kazi.”

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania