Mhubiri 11

Mhubiri 11

Afanyavyo mwenye busara

1Jishughulishe na biashara

hata kama kwa kubahatisha;

yawezekana baadaye

ukapata chochote kile.

2Wagawie watu saba hata wanane sehemu yako,[#11:1-2 Tafsiri ya aya ya 1 ni ya makala ya Kiebrania iliyo ngumu na ambayo neno kwa neno ni : “Tupa chakula chako usoni pa maji … utakiona baada ya siku nyingi”. Wengi wamechukua maneno hayo kuwa na maana ya kuwasaidia maskini (Kumb 15:10; Gal 6:9,10). Lakini huenda kuna uhusiano wa namna hii ya kusema na Isa 18:2 ambapo yahusu kufanya biashara.]

maana, hujui balaa litakalofika duniani.

3Mawingu yakijaa maji, mvua hunyesha;

mti ukiangukia kusini au kaskazini,

hapo uangukiapo ndipo ulalapo.

4Anayengoja upepo hatapanda mbegu,

anayesubiri mawingu yatoweke, hatavuna kitu.

5Usivyojua jinsi uhai unavyoingia katika mifupa ya mtoto tumboni mwa mamake, kadhalika huwezi kuelewa matendo ya Mungu, ambayo hufanya kila kitu.

6Panda mbegu asubuhi na jioni usiache kupanda, maana, hujui zipi zitaota; za asubuhi, za jioni, au zote zitakuwa nzuri.

7Mwanga wafaa, na kuliona jua kwapendeza macho.

8Mtu akiishi miaka mingi, na aifurahie miaka hiyo yote; lakini akumbuke kuwa siku za giza zitakuwa nyingi, na kwamba yote yatakayofuata ni bure.[#11:7-8 Mwandishi anakiri kwamba katika maisha kuna uzuri (aya 7); na kwamba kuna siku za giza (kwa maana ya siku mbaya au kifo) zitakuwa nyingi. Ulinganisho baina ya giza na mwanga ni wazo kawaida katika Biblia na wazo hilo lilijitokeza tangu 2:13-14.]

Mawaidha kwa vijana

9Ewe kijana, furahia ujana wako, moyo wako, uchangamke wakati ungali kijana. Fuata mapenzi ya moyo wako na upeo wa macho yako. Lakini kumbuka kwamba Mungu atakuhukumu kadiri ya hayo yote.[#11:9 Sehemu ya kwanza ya aya hii inaonekana kwa jumla kwamba ni mtazamo wa kawaida wa huyo mwanafalsafa (taz 2:24-26; 3:12,13,22; 5:18-20; 9:7). Lakini mtazamo huo hauna lengo la kuhimiza maisha ya hovyo au ya kipumbavu (5:1-7). Ndio maana sehemu ya pili (hata kama wengine wanafikiri ilijumlishiwa hapo baadaye) inammwonya binadamu juu ya athari za kuishi bila kumtii Mungu (taz pia 12:14).]

10Ondoa mahangaiko moyoni mwako, jikinge, usipate maumivu mwilini kwa sababu ujana na mwisho wa maisha ni bure kabisa.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania