Mhubiri 6

Mhubiri 6

1Nimeona jambo moja ovu hapa duniani, linalowakandamiza watu:

2Mungu humjalia mtu utajiri, mali na heshima, asitindikiwe kitu chochote anachotamani, lakini hampi uwezo wa kuvifurahia vitu hivyo; badala yake, mgeni fulani atavifaidi. Hilo nalo ni bure kabisa; ni jambo la mateso makali.[#6:2 Taz 2:18-23; 5:13-17. Hatuambiwi ni namna gani huyo tajiri anazuiwa kufurahia mali yake. Wazo ni kwamba ingalikuwa afadhali kwake kutokuwa na utajiri huo. Mwandishi anaiona hali hiyo kama isiyo nzuri; lakini, bila shaka anasema hivyo kuonesha tena kwamba binadamu hawezi kuelewa njia au mipango ya Mungu.]

3Mtu akiweza kuzaa watoto 100, na akaishi maisha marefu, lakini kama mtu huyo hafurahii maisha yake, wala hafanyiwi mazishi basi nasema mtoto aliyezaliwa amekufa ni afadhali kuliko mtu huyo.

4Mtoto mfu hafaidiki chochote kwa kuzaliwa; yeye hutokomea gizani, akasahaulika.[#6:3-5 Katika utamaduni wa Waisraeli kama vile na tamaduni za makabila na mataifa mengi kupata watoto ilichukuliwa kuwa zawadi kubwa kutoka kwa Mungu. Lakini hiyo nayo si kitu kama mtu asipopata mazishi yanayostahili (2Fal 9:33-37; Isa 14:19; Yer 16:4-7; 22:18-19). Kama kawaida yake, mwandishi anaingiza hapa picha ya mtoto aliyezaliwa mfu ili kulinganisha na maisha ya mtu aliye na mali na hakuyafurahia na hakupata kuzikwa kwa heshima ifaayo. Afadhali mtoto aliyezaliwa mfu kuliko huyo tajiri.]

5Zaidi ya hayo, mtoto wa namna hiyo hakupata kuuona mwanga wa jua wala kutambua chochote. Hata hivyo, huyo mtoto angalau hupata pumziko ambapo yule mtu hapati.

6Ingawa mtu huyo ataishi miaka elfu mbili, lakini hafurahii maisha, basi ni kama huyo mtoto wote wawili huenda mahali pamoja.

7Kazi yote ya mtu ni kwa ajili ya kupata chakula, lakini tamaa yake ya kula haitoshelezwi kamwe.

8Je, mtu mwenye hekima anayo nafuu zaidi kuliko mpumbavu? Na mtu maskini hupata faida gani akijua namna ya kuyakabili maisha?

9Hayo nayo ni bure kabisa; ni sawa na kufukuza upepo. Afadhali kuridhika na ulicho nacho kuliko kuhangaika kwa kutamani kitu kingine.

10Kila kitu kinachotukia kilikwisha pangwa hapo awali; hali ya binadamu inajulikana, na tunajua kwamba mnyonge hawezi kubishana na mtu mwenye nguvu zaidi.[#6:10 Wazo la hapo awali ni 1:9-10 (taz 1:8-11 maelezo); 3:3-15.]

11Maneno mengi hayana faida, hayamwinui binadamu.

12Nani ajuaye yamfaayo mtu katika maisha haya mafupi yasiyo na faida, maisha ambayo hupita kama kivuli? Nani duniani ajuaye yatakayompata mtu baada ya kufa?

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania