Mhubiri 7

Mhubiri 7

Mawaidha kuhusu maisha

1Sifa njema ni bora kuliko marashi ya thamani.[#7:1 Kuwa na jina au sifa nzuri ni jambo lililothaminiwa sana katika maandishi ya hekima (Meth 10:7; 22:1) na pia katika tamaduni mbalimbali za makabila ya Afrika. Uhusiano wa sehemu ya pili ya msemo huo: “Siku ya kufa ni bora kuliko siku ya kuzaliwa” na hiyo sehemu ya kwanza si dhahiri. Hata hivyo inaonekana kwamba mwandishi alitaka kuonesha kwamba sifa njema ya mtu inaeonekana jinsi anavyomalizia maisha yake. Picha hiyo inaendelezwa katika aya inayofuata.]

Siku ya kufa ni bora kuliko siku ya kuzaliwa.

2Afadhali kwenda kwenye matanga,

kuliko kwenda kwenye karamu,

kwa sababu walio hai yawapasa kukumbuka kwamba kifo chatungojea sisi sote.

3Huzuni ni afadhali kuliko kicheko

maana, huzuni ya uso ni faida ya moyo.

4Moyo wa mwenye hekima huthamini matanga,

lakini moyo wa mpumbavu hupenda raha.

5Afadhali kusikia maonyo ya wenye hekima

kuliko kusikiliza nyimbo za wapumbavu.

6Maana, kicheko cha mpumbavu

ni kama mlio wa miiba motoni.

Hayo nayo ni bure kabisa.

7Mwenye hekima akimdhulumu mtu;

hujifanya mwenyewe kuwa mpumbavu

kupokea rushwa hupotosha akili.

8Mwisho wa jambo ni afadhali kuliko mwanzo wake;

mvumilivu rohoni ni bora kuliko mwenye majivuno.

9Usiwe mwepesi wa hasira,

maana, hasira hukaa ndani ya wapumbavu.

10Usiulize, “Kwa nini nyakati za kale zilikuwa bora kuliko za sasa?”

Huulizi hivyo kwa kutumia hekima.

11Hekima ni ya thamani kubwa kama urithi;[#7:11-12 Kuhusu thamani ya hekima taz Meth 16:16.]

ni muhimu kwa wale wote walio hai.

12Kulindwa na hekima ni kama kulindwa na fedha.

Faida ya maarifa ni kwamba hekima hulinda maisha ya mtu aliye nayo.

13Tafakarini vema kazi yake Mungu;

ni nani awezaye kunyosha alichopinda Mungu?

14Katika siku za fanaka uwe na furaha; katika siku za maafa utafakari jambo hili: fanaka, pia maafa, Mungu amefanya hiyo ya kwanza iambatane na ya pili ili binadamu asiweze kujua yatakayotukia baada yake.

15Katika maisha yangu duni, nimeona kila kitu; mtu mwadilifu hufa ingawa ni mwadilifu, ambapo mtu mwovu huendelea kuishi maisha marefu ingawa ni mwovu.

16Basi, usiwe mwadilifu sana, wala usiwe mwenye hekima mno! Ya nini kujiangamiza wewe mwenyewe?[#7:16 Mawaidha yanayosemewa hapa kwa msomaji si dhahiri, na fafanuzi tofauti zimetolewa na wataalamu wa mambo ya Biblia. Mwandishi labda anajaribu kusema kwamba mtu hapaswi kujaribu kuwa mwema mno au mwenye hekima mno maana hakuna binadamu duniani anayetenda yaliyo sawa daima (7:20). Au, huenda mwandishi anaonya juu ya kujisingizia kuwa mwema mno kuliko alivyo kikweli maana hiyo inaweza kuleta uharibifu (Meth 16:18).]

17Lakini pia, usiwe mwovu sana wala usiwe mpumbavu! Ya nini kufa kabla ya wakati wako?

18Inakupasa ushike la kwanza na la pili pia; maana anayemtii Mungu atajengwa kwayo.

19Hekima humfanya mwenye busara kuwa na nguvu zaidi kuliko watawala kumi mjini.

20Hakika, hakuna mtu mwadilifu duniani atendaye mema daima bila kutenda dhambi.

21Usitie maanani maneno yote wasemayo wanadamu, usije ukamsikia mtumishi wako akikutukana.

22Wewe mwenyewe wajua moyoni kwamba umeapiza wengine mara nyingi.

Kuomba hekima

23Nimeyapima hayo yote kwa hekima; nikajisemea: “Nataka kuwa mwenye hekima!” Lakini hekima iko mbali sana nami.

24Jinsi gani binadamu ataweza kugundua maana ya maisha; jambo hilo ni zito na gumu mno kwetu!

25Hata hivyo, nilipania kujua na kuchunguza na kutafuta hekima na maana ya mambo yaliyoko, na pia kujua uovu ni upuuzi, na upumbavu ni wazimu.

26Jambo moja nililogundua lililo baya zaidi kuliko kifo, ni mwanamke ambaye moyo wake ni mtego na wavu, na mikono yake ni kama minyororo. Lakini anayempendeza Mungu humkwepa mwanamke huyo, lakini mwenye dhambi hunaswa naye.[#7:26 Huyu ni mwanamke ambaye hujaribu kuwashawishi wanaume kuzini naye (Meth 2:16-19; 5:7-18; 9:13-18; 23:27-28). Lakini huyo “mwanamke … mtego” yamkini pia ni mfano wa chochote kile ambacho huwaongoza watu waache kuwa waaminifu kwa Mungu. Katika maandishi ya hekima, kwa upande mmoja “Hekima” na kwa upande mwingine “Upumbavu”, huelezwa pia kwa picha ya “mwanamke” (Meth 3:16-18; 9:1-6).]

27Haya, nakuambia mimi Mhubiri, ndio niliyogundua nilipofanya uchunguzi wangu kidogokidogo.

28Nilipania kugundua mambo hayo tena na tena, lakini sikufaulu. Kati ya wanaume elfu moja, nilifaulu kumwona mwanamume mmoja, anayestahili heshima, lakini kati ya wanawake wote kama hao sikumwona hata mmoja anayestahili heshima.

29Tazama, nimegundua jambo hili moja: kwamba Mungu aliwaumba wanadamu wanyofu, lakini wao wenyewe wamejitafutia matatizo.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania