The chat will start when you send the first message.
1Enyi Wagalatia, mmekuwa wajinga kweli! Ni nani aliyewaroga? Habari juu ya kusulubiwa kwake Yesu Kristo ilielezwa waziwazi mbele ya macho yenu.[#3:1—5:15 Hii ni sehemu ya katikati ya barua hii na ina shabaha ya kuonesha kwamba Mungu alikamilisha katika Kristo ile ahadi aliyompa Abrahamu na wazawa wake; kutokana na hayo sheria haina tena nafasi yake kuu. Mkristo hayuko tena katika utawala wa sheria na ameitwa kuishi katika uhuru ule unaopatikana katika kuungana na Kristo.]
2Napenda kujua tu kitu kimoja kutoka kwenu: Je, mlipokea Roho wa Mungu kwa sababu ya kutimiza matakwa ya sheria ama kwa sababu ya kuisikia na kuiamini Injili?[#3:2 Aya ya pili mpaka ya tano ni maswali ambayo majibu yake ni dhahiri; yanatumika hapa kuweka katika ngazi ya juu kabisa umuhimu wa kuamini Habari Njema ya Yesu katika shughuli yote ya wokovu; sheria haina nafasi yake katika jambo hilo. Mfululizo huo unatayarisha pia mfano ambao Paulo ataueleza kuanzia aya ya sita.]
3Je, nyinyi ni wajinga kiasi hicho? Nyinyi mlianza yote kwa msaada wa Roho, je, mnataka sasa kumaliza kwa nguvu zenu wenyewe?
4Je, mambo yale yote yaliyowapata nyinyi yamekuwa bure tu? Haiwezekani!
5Je, Mungu huwajalia Roho na kutenda miujiza kati yenu ati kwa sababu mnatimiza yanayotakiwa na sheria, ama kwa sababu mnasikia Injili na kuiamini?
6Chukueni kwa mfano habari za Abrahamu: yeye alimwamini Mungu, naye Mungu akamkubali kuwa mwadilifu.[#3:6 Gal Mwa 15:6; Rom 4:3. Itakumbukwa kwamba wazo hilo muhimu la kuwafanya watu kuwa waadilifu linaendelezwa kwa kirefu katika Rom 4.]
7Sasa basi, jueni kwamba watu wenye kumwamini ndio walio watoto halisi wa Abrahamu.
8Maandiko Matakatifu yalionesha kabla kwamba Mungu atawafanya watu wa mataifa kuwa waadilifu kwa njia ya imani. Hivyo Maandiko Matakatifu yalitangulia kumtangazia Abrahamu Habari Njema: “Katika wewe mataifa yote yatabarikiwa.”
9Basi, wale walio na imani wanabarikiwa pamoja na Abrahamu aliyeamini.
10Lakini wote wanaotegemea tu kutimiza yanayotakiwa na sheria, wako chini ya laana. Maana, Maandiko Matakatifu yasema: “Yeyote asiyeshika na kutimiza yote yaliyoandikwa katika kitabu cha sheria, yuko chini ya laana.”
11Ni dhahiri kwamba sheria haiwezi kumfanya mtu kuwa mwadilifu; maana Maandiko yasema: “Mwadilifu kwa imani ataishi.”[#3:11 Hab 2:4; taz Rom 1:17 maelezo.]
12Lakini sheria haitegemei imani, ila Maandiko yasema: “Mwenye kutimiza yanayotakiwa na sheria ataishi.”
13Kristo alitukomboa kutoka katika laana ya sheria kwa kujitwalia laana hiyo kwa ajili yetu; maana Maandiko yanasema: “Yeyote aliyetundikwa msalabani amelaaniwa.”[#3:13 Kitenzi cha Kigiriki chenye maana ya “kukomboa” hapa kinamaanisha pia kulipwa kitu au bei ili kumwondoa mtu kutoka hali fulani (kwa kawaida hali isiyofaa). Lakini hapa wazo linalotokeza zaidi ni lile la kupata uhuru kwa kifo cha Yesu Kristo. Taz Rom 3:25 maelezo.; #3:13 Kumb 21:23. Paulo anatumia maneno hayo moja kwa moja kuhusu kifo cha Yesu msalabani ambapo alichukua nafasi yetu ya kubeba ile laana na kwa kufanya hivyo tukapata uhuru wetu.]
14Jambo hili lilifanyika kusudi ile baraka aliyopewa Abrahamu iwashukie watu wa mataifa mengine kwa njia ya Kristo, na ili kwa imani, tumpokee yule Roho ambaye Mungu alituahidia.
15Ndugu, nitawapeni mfano kutoka maisha yetu ya kila siku. Fikirini juu ya mkataba kati ya watu wawili. Mkataba ukisha fanyika na kutiwa sahihi hapana mtu anayeuweka kando au kuuongezea kitu.
16Basi, Abrahamu alipewa ahadi, yeye pamoja na mzawa wake. Maandiko hayasemi: “Na wazawa wake,” yaani wengi, bali yasema, “Na mzawa wake,” yaani mmoja, naye ndiye Kristo.[#3:16 Mwa 12:7. Matumizi ya neno “mzawa” katika Mwanzo (mmoja) ingawa linachukua maana ya jamii, yanampa Paulo fursa ya kuendeleza hoja yake kwa mtindo wa kawaida uliofahamika kwa waalimu wa Kiyahudi na kuona kwamba hapo katika Mwa 12:7, huyo mmoja ni Kristo.]
17Ninachotaka kusema ni hiki: Mungu alifanya agano lake, akalithibitisha; sheria ambayo ilitokea miaka 430 baadaye, haiwezi kulitangua hilo agano wala kuibatilisha hiyo ahadi.[#3:17 Yaani, tangu wakati wa Abrahamu mpaka wakati Mose alipowaongoza Waisraeli kutoka Misri. Taz Kut 12:40.]
18Maana, kama zawadi ya Mungu inategemea sheria, basi, haiwezi kutegemea tena ahadi ya Mungu. Kumbe, lakini Mungu alimkirimia Abrahamu kwa sababu aliahidi.
19Ya nini basi, sheria? Iliongezwa hapo ili kuonesha uhalifu ni kitu gani, mpaka atakapokuja yule mzawa wa Abrahamu aliyepewa ile ahadi. Sheria ililetwa na malaika kwa mkono wa mpatanishi.[#3:19 Taz Mate 7:53 maelezo.]
20Ama hakika, mpatanishi hahitajiwi ikiwa jambo lenyewe lamhusu mtu mmoja; na Mungu ni mmoja.
21Je, sheria inapingana na ahadi za Mungu? Hata kidogo! Maana, kama kungalitolewa sheria ambayo ingeweza kuwapa watu uhai, basi, tungeweza kufanywa waadilifu kwa njia ya sheria.
22Lakini sivyo; Maandiko Matakatifu yamekwisha sema kwamba ulimwengu wote upo chini ya utawala wa dhambi; na hivyo, wenye kuamini watimiziwe ile ahadi aliyotoa Mungu, kwa kumwamini Yesu Kristo.
23Kabla ya kujaliwa imani, sheria ilitufanya wafungwa, tukingojea imani hiyo ifunuliwe.
24Basi, hiyo sheria ilikuwa kama mlezi wetu mpaka alipokuja Kristo, ili kwa njia ya imani tufanywe waadilifu mbele yake Mungu.[#3:24 Paulo hatumii neno “mlezi” hapa kwa maana ya kufunza na kuongoza, bali kwa maana ya kwamba mlezi ni mtu wa kupita tu mpaka hali fulani ifikiwe.]
25Lakini kwa vile ile imani imekwisha fika, sisi hatuko tena chini ya mlezi.
26Kwa njia ya imani, nyinyi nyote mmekuwa watoto wa Mungu kwa kuungana na Kristo.
27Nyinyi nyote mliobatizwa mkaungana na Kristo ni kama vile mmemvaa Kristo.[#3:27 Rom 13:12-14; rejea Efe 4:22-25; Kol 3:8-12.]
28Hivyo, hakuna tena tofauti kati ya Myahudi na Mgiriki, mtumwa na mtu huru, mwanamume na mwanamke. Nyote ni kitu kimoja kwa kuungana na Kristo Yesu.[#3:28 Rom 10:12; 1Kor 12:13; Kol 3:11. Kwa kuungana na Kristo, tofauti zote kati ya kati ya mataifa, kabila, jamii na jinsia zinaondolewa.]
29Ikiwa nyinyi ni wa Kristo, basi ni wazawa wa Abrahamu, na mtapokea yale aliyoahidi Mungu.