Waamuzi 10

Waamuzi 10

Tola

1Baada ya kifo cha Abimeleki, Tola mwana wa Pua mwana wa Dodo, wa kabila la Isakari, akatokea kuwakomboa Waisraeli. Tola aliishi Shamiri katika nchi ya milima ya Efraimu.[#10:1-5 Aya hizi zina orodha ya kwanza ya watu ambao wanajulikana kama “waamuzi wadogo”. Katika 12:8-12 tunapewa orodha nyingine. Hatujui mengi juu ya watu hao ila tu kwamba walikuwa waamuzi (taz aya 1 ambapo Tola anasemwa kuwa alitokea kuwakomboa Waisraeli).; #10:1 Huyu alikuwa wa kabila la Isakari (Hes 26:23-25). Haisemwi zaidi jinsi alivyowakomboa Waisraeli.]

2Alikuwa mwamuzi wa Israeli kwa miaka ishirini na mitatu, kisha akafariki na kuzikwa huko Shamiri.

Yairi

3Baada ya Tola, alitokea Yairi wa Gileadi, akawa mwamuzi wa Waisraeli kwa miaka ishirini na miwili.[#10:3-4 Yairi alikuwa na watoto wa kiume thelathini, kila mmoja na punda wake; hiyo aghalabu ilikuwa ishara ya kwamba jamaa hiyo ilikuwa tajiri. Eneo la Gileadi lilikuwa mashariki ya mto Yordani.]

4Yairi alikuwa na watoto wa kiume thelathini ambao walipanda punda thelathini na walikuwa na miji thelathini katika nchi ya Gileadi, ambayo mpaka leo inaitwa Hawoth-yairi.[#10:4 Maana yake ni “vijiji vya Yairi”. Taz Kumb 3:14.]

5Yairi alifariki na kuzikwa huko Kamoni.

Yeftha

6Waisraeli walitenda tena uovu mbele ya Mwenyezi-Mungu wakatumikia Mabaali, Maashtarothi, na miungu ya Shamu, ya Sidoni, ya Moabu, ya Amoni na ya Wafilisti. Walimwacha Mwenyezi-Mungu na wala hawakumwabudu tena.[#10:6 Amu 2:11-13; 3:7,12; 4:1; 6:1. Baali na Ashtarte ilikuwa miungu mikuu ya Wakanaani; hata mataifa ya jirani nayo yalikuwa na miungu ya namna hiyohiyo, ya kike na ya kiume.]

7Hasira ya Mwenyezi-Mungu ikawaka dhidi ya Israeli, naye akawatia mikononi mwa Wafilisti na Waamoni.

8Kwa miaka kumi na minane hao waliwatesa na kuwakandamiza Waisraeli walioishi huko Gileadi katika eneo la Waamori mashariki ya mto Yordani.

9Waamoni nao walivuka mto Yordani kupigana na makabila ya Yuda, Benyamini na Efraimu. Nao Waisraeli wakapata taabu sana.

10Basi wakamlilia Mwenyezi-Mungu, wakisema, “Tumetenda dhambi dhidi yako, maana tumekuacha wewe Mungu wetu, tukatumikia Mabaali.”

11Naye Mwenyezi-Mungu akawaambia, “Je, mimi sikuwakomboa kutoka kwa Wamisri, Waamoni, Waamori, Wafilisti?

12Wasidoni, Waamaleki na Wamidiani waliwakandamiza nanyi mkanililia, nami nikawakomboa mikononi mwao.

13Hata hivyo nyinyi mmeniacha, mkatumikia miungu mingine. Kwa hiyo sitawakomboeni tena.

14Nendeni mkaililie hiyo miungu mliyoichagua. Iacheni hiyo iwakomboe katika taabu zenu!”

15Lakini Waisraeli wakamwambia Mwenyezi-Mungu, “Tumetenda dhambi. Tufanye upendavyo, lakini tunakuomba utuokoe leo.”

16Kisha wakaitupilia mbali miungu ya kigeni, wakamtumikia tena Mwenyezi-Mungu. Mwenyezi-Mungu hakuweza kuvumilia zaidi kuona taabu za Waisraeli.[#10:10-15 Waisraeli wanamwambia Mungu kwamba wamemkosea lakini Mungu hakubali (aya 11-14). Ni pale tu walipoondoa vinyago vya hiyo miungu miongoni mwao ndipo anapokubali kuwasaida tena (aya 16).]

17Waamoni wakajikusanya wakapiga kambi yao huko Gileadi. Waisraeli nao wakakusanyika na kupiga kambi yao huko Mizpa.[#10:17 Katika Amu 10-12 Mispa ni jina la mji katika nchi ya Gileadi, mashariki ya mto Yordani na ni tofauti na Mispa katika sura 20—21 ambao uko katika eneo la Benyamini.]

18Waisraeli na viongozi wao wakaulizana, “Ni nani atakayeanza kupigana na Waamoni? Atakayefanya hivyo ndiye atakayekuwa kiongozi wa wakazi wote wa Gileadi.”

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania