Yoeli 3

Yoeli 3

Mungu atayahukumu mataifa

1“Wakati huo na siku hizo

nitakapoirekebisha hali ya Yuda na Yerusalemu,

2nitayakusanya mataifa yote,

niyapeleke katika bonde liitwalo,

‘Mwenyezi-Mungu Ahukumu.

Huko nitayahukumu mataifa hayo,

kwa mambo yaliyowatendea watu wangu Israeli,

hao walio mali yangu mimi mwenyewe.

Maana waliwatawanya miongoni mwa mataifa,

waligawa nchi yangu

3na kugawana watu wangu kwa kura.[#3:3 Wakazi wa Yuda walipochukuliwa uhamishoni kule Babuloni mnamo mwaka 586 K.K. waliowateka walipiga kura kuchagua wafungwa (taz Oba 11).]

Waliwauza wavulana ili kulipia malaya,

na wasichana ili kulipia divai.

4“Mnataka kunifanya nini enyi Tiro na Sidoni na maeneo yote ya Filistia? Je, mna kisasi nami mnachotaka kulipiza? Kama mnalipiza kisasi, mimi nitawalipizeni mara moja![#3:4 Hii ilikuwa miji ya Foinike maarufu sana kwenye pwani ya Mediteranea.]

5Mmechukua fedha na dhahabu yangu, na kuvibeba vitu vyangu vya thamani hadi kwenye mahekalu yenu.

6Mmewapeleka watu wa Yuda na Yerusalemu mbali na nchi yao, mkawauza kwa Wagiriki.[#3:6 mshairi Mgiriki aitwaye Homeri anashuhudia pia kwamba Wagiriki walifanya biashara ya utumwa (taz pia Eze 27:13).]

7Sasa, nitawarudisha watu wangu kutoka huko mlikowauza. Nitawalipizeni kisasi kwa yote mliyowatendea.

8Watoto wenu wa kiume na wa kike nitawafanya wauzwe kwa watu wa Yuda, nao watawauzia Washeba, watu wa taifa la mbali kabisa. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.[#3:8 Hawa waliishi kwenye eneo la kusini mwa Arabia.]

9“Watangazieni watu wa mataifa jambo hili:[#3:9 Mwisho wa nyakati unaelezwa mara nyingine kama wa vita vikubwa ambavyo Mwenyezi-Mungu ataibuka mshindi dhidi ya nguvu za uovu na haki itatawala (rejea Eze 39:1-10).]

Jitayarisheni kwa vita,

waiteni mashujaa wenu;

askari wote na wakusanyike,

waende mbele.

10Majembe yenu yafueni yawe mapanga,

miundu yenu ya kupogolea iwe mikuki.

Hata aliye dhaifu na aseme:

‘Mimi pia ni shujaa’.

11Njoni haraka, enyi mataifa yote jirani,

kusanyikeni huko bondeni.”

Ee Mwenyezi-Mungu!

Teremsha askari wako dhidi yao!

12“Haya mataifa na yajiweke tayari;

yaje kwenye bonde liitwalo:

‘Mwenyezi-Mungu Ahukumu’.

Huko, mimi Mwenyezi-Mungu,

nitaketi kuyahukumu mataifa yote ya jirani.

13Haya! Chukueni mundu wa kuvuna,

kwani sasa ni wakati wa mavuno.

Ingieni! Wapondeni kama zabibu

ambazo zimejaza shinikizo.

Uovu wao umepita kiasi

kama mapipa yanayofurika.”

14Wanafika makundi kwa makundi

kwenye bonde la Hukumu,

maana siku ya Mwenyezi-Mungu imekaribia.

15Jua na mwezi vinatiwa giza,

na nyota zimeacha kuangaza.

Mungu atawabariki watu wake

16Mwenyezi-Mungu ananguruma huko Siyoni;

sauti yake inavuma kutoka Yerusalemu;

mbingu na dunia vinatetemeka.

Lakini Mwenyezi-Mungu ni kimbilio la watu wake,

ni ngome ya usalama kwa Waisraeli.

17“Hapo, ewe Israeli,

utajua kwamba mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako,

nakaa Siyoni, mlima wangu mtakatifu,

Yerusalemu utakuwa mji mtakatifu;

na wageni hawatapita tena humo.

18“Wakati huo, milima itatiririka divai mpya,

na vilima vitatiririka maziwa.

Vijito vyote vya Yuda vitajaa maji;

chemchemi itatokea nyumbani mwa Mwenyezi-Mungu,

na kulinywesha bonde la Shitimu.

19“Misri itakuwa mahame,

Edomu itakuwa jangwa tupu,

kwa sababu waliwashambulia watu wa Yuda

wakawaua watu wasio na hatia.

20Bali Yuda itakaliwa milele,

na Yerusalemu kizazi hata kizazi.

21Nitawaadhibu waliomwaga damu ya watu wa Yuda

wala sitawaachia wenye hatia.

Mimi, Mwenyezi-Mungu nakaa Siyoni.”

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania