Mathayo 7

Mathayo 7

Kuhusu kuwahukumu wengine

(Luka 6:37-38,41-42)

1“Msiwahukumu wengine, msije nanyi mkahukumiwa na Mungu;

2kwa maana jinsi mnavyowahukumu wengine, ndivyo nanyi mtakavyohukumiwa; na kipimo kilekile mnachotumia kwa wengine ndicho Mungu atakachotumia kwenu.

3Kwa nini wakiona kibanzi kilicho jichoni mwa ndugu yako, na papo hapo huioni boriti iliyoko jichoni mwako?[#7:3 Namna ya makusudi ya kusema kwa upeo; taz maelezo ya Mat 5:29-30.]

4Au, wawezaje kumwambia ndugu yako, ‘Ndugu, ngoja nikuondoe kibanzi jichoni mwako,’ wakati wewe mwenyewe unayo boriti jichoni mwako?

5Mnafiki wewe! Ondoa kwanza boriti iliyomo jichoni mwako na hapo ndipo utaona sawasawa kiasi cha kuweza kuondoa kibanzi kilichomo jichoni mwa ndugu yako.

6“Msiwape mbwa vitu vitakatifu wasije wakageuka na kuwararua nyinyi; wala msiwatupie nguruwe lulu zenu wasije wakazikanyaga.[#7:6 Haidhihiriki ni vitu gani hivyo vitakatifu: Tambiko kwa Mungu, mafundisho ya dini au Habari Njema.; #7:6 Maneno yanayotumika kwa maana ya watu wasiotaka kuthamini ubora wa vitu vizuri vya kiroho. Kwa Wayahudi, mbwa na nguruwe walikuwa wanyama najisi.]

Omba, tafuta, bisha mlango

(Luka 11:9-13)

7“Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtapata; bisheni mlango, nanyi mtafunguliwa.[#7:7 Sala kama njia ya kuwasiliana na Mungu. Taz pia Marko 11:24; Luka 11:9-13; Yer 29:13-14; Yoh 14:13; 16:23; ling pia Isa 55:6.]

8Maana, yeyote aombaye hupewa, atafutaye hupata, na abishaye mlango hufunguliwa.

9Je, kuna yeyote miongoni mwenu ambaye mtoto wake akimwomba mkate, atampa jiwe?

10Au je, akimwomba samaki, atampa nyoka?

11Kama basi nyinyi, ingawa ni waovu, mwajua kuwapa watoto wenu vitu vizuri, hakika Baba yenu wa mbinguni atafanya zaidi: atawapa mema wale wanaomwomba.

12“Yote mnayotaka watu wawatendee nyinyi, watendeeni wao vivyo hivyo. Hii ndiyo maana ya sheria ya Mose na mafundisho ya manabii.[#7:12 Taz pia Luka 6:31. Msemo huu ambao pengine wajulikana kama “sheria ya dhahabu” ulijulikana tangu zamani hata kwa watu wasio Wayahudi. Ilikaririwa pengine katika muundo wake wa kinyume: “usimtendee mwenzako … kama usivyopenda kutendewa naye”. Yesu lakini anatilia mkazo hali ya kutenda siyo kutotenda kama msimamo wa kitendo chema.; #7:12 Taz 5:17.]

Mlango mwembamba

(Luka 13:24)

13“Ingieni kwa kupitia mlango mwembamba. Kwa maana njia inayoongoza kwenye maangamizi ni pana, na mlango wa kuingilia humo ni mpana; waendao njia hiyo ni wengi.

14Lakini njia inayoongoza kwenye uhai ni nyembamba, na mlango wa kuingilia humo ni mwembamba; ni watu wachache tu wanaoweza kuigundua njia hiyo.[#7:14 Msemo wenyewe labda wahusu magumu yaliyotajwa katika aya zilizotangulia, au jambo la haraka la kumfuata Yesu pamoja na magumu na mateso yanayoambatana na hali hiyo.]

Mti hujulikana kwa matunda yake

(Luka 6:43-44)

15“Jihadharini na manabii wa uongo. Wao huja kwenu wakionekana kama kondoo kwa nje, lakini kwa ndani ni mbwamwitu wakali.

16Mtawatambua kwa matendo yao. Je, watu huchuma zabibu katika miti ya miiba, au tini katika mbigili? La![#7:16 Linatafsiri neno la Kigiriki “Karpos” (tunda). Mara nyingi mfano wa mti na matunda hutumiwa katika maandishi ya hekima kuelezea hali ya mtu. Taz pia Yak 3:12.]

17Basi, mti mzuri huzaa matunda mazuri, na mti mbaya huzaa matunda mabaya.

18Mti mzuri hauwezi kuzaa matunda mabaya, wala mti mbaya hauwezi kuzaa matunda mazuri.

19Kila mti usiozaa matunda mazuri utakatwa na kutupwa motoni.

20Kwa hiyo, mtawatambua kwa matendo yao.

Siwajui nyinyi

(Luka 13:25-27)

21“Si kila aniambiaye, ‘Bwana, Bwana’, ataingia katika ufalme wa mbinguni; ila ni yule tu anayetimiza matakwa ya Baba yangu aliye mbinguni.

22Wengi wataniambia siku ile ya hukumu: ‘Bwana, Bwana! Kwa jina lako tulitangaza ujumbe wako, na kwa jina lako tuliwatoa pepo na kufanya miujiza mingi’.

23Hapo nitawaambia: ‘Sikuwajua nyinyi kamwe; ondokeni mbele yangu, enyi watenda maovu.’[#7:23 Msemo huu ni sawa na “nyinyi si wangu” (rejea 1Kor 8:3; 2Tim 2:19). “Ondokeni … enyi watenda maovu” (taz Zab 6:8).]

Wajenzi wawili

(Luka 6:47-49)

24“Kwa hiyo, kila mtu anayeyasikia maneno yangu na kuyazingatia, anafanana na mtu mwenye busara, aliyejenga nyumba yake juu ya mwamba.

25Mvua ikanyesha, mito ikafurika, pepo kali zikavuma na kuipiga nyumba hiyo. Lakini haikuanguka kwa sababu ilikuwa imejengwa juu ya mwamba.

26“Lakini yeyote anayesikia maneno yangu haya bila kuyazingatia, anafanana na mtu mpumbavu aliyejenga nyumba yake juu ya mchanga.

27Mvua ikanyesha, mito ikafurika, pepo kali zikavuma na kuipiga nyumba hiyo, nayo ikaanguka; tena anguko hilo lilikuwa kubwa.”

Mamlaka ya Yesu

28Yesu alipomaliza kusema maneno hayo, umati wa watu ukashangazwa na mafundisho yake.[#7:28 Msemo huo na maneno mengine yanayofanana nao unatumika kutia alama mwisho wa kila moja ya sehemu tano za masimulizi yaliyopangwa na mwandishi Mathayo.]

29Hakuwa kama waalimu wao wa sheria, bali alifundisha kwa mamlaka.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania