The chat will start when you send the first message.
1Watu walianza kumlalamikia Mwenyezi-Mungu juu ya taabu zao. Mwenyezi-Mungu aliposikia, alishikwa na hasira, akawapelekea moto. Moto huo uliwaka kati yao na kuchoma upande mmoja wa kambi.[#11:1 Tafsiri nyingine: “Watu walianza kumnung'unikia Mwenyezi Mungu”. Jambo la Waisraeli kumlalamikia Mwenyezi-Mungu ni wazo linalotajwa katika kitabu cha Kutoka na mara nyingi katika kitabu hiki cha Hesabu (taz Kut 14:11-12 maelezo). Kutokana na malalamiko hayo mwandishi anatilia mkazo maombi ya Mose kwa Mwenyezi-Mungu kumsihi awe na huruma kwao.; #11:1 Taz 9:15-16 maelezo. Hapo matukio ya moto, moshi na wingu viliashiria kuweko kwake Mungu. Lakini hapa, kama vile pia mahali pengine katika Biblia, moto ni ishara ya hukumu ya adhabu kutoka kwa Mungu.]
2Watu wakamlilia Mose, naye akamwomba Mwenyezi-Mungu na moto huo ukazimika.
3Kwa hiyo, mahali hapo pakaitwa Tabera, kwa sababu hapo moto wa Mwenyezi-Mungu uliwaka kati ya watu.[#11:3 Jina hili ni kama neno la Kiebrania lenye maana “kuchoma.”]
4Miongoni mwa Waisraeli kulikuwa na kundi fulani lililoandamana nao ambalo lilikuwa na hamu kubwa. Waisraeli kwa mara nyingine walilia, wakisema. “Laiti kama tungeweza kupata nyama ya kula![#11:4 Habari hii ni ya pekee, lakini ni muhimu sana kihistoria. Yaani watu waliotoka Misri walikuwa kweli Waisraeli, lakini kulikuwa pia watu wengine ambao hawakuwa Waisraeli (taz Kut 12:38). Inaonekana kwamba kunung'unika kwao juu ya kukosa chakula cha Wamisri kuliwafanya pia nao Waisraeli wanung'unike.]
5Tunakumbuka, samaki tuliokula kule Misri bila malipo, matango, matikiti, mboga, vitunguu na vitunguu saumu!
6Lakini sasa nguvu zimetuishia na hakuna chakula kingine isipokuwa hii mana tu!”[#11:6 Mungu aliwapatia Waisraeli chakula hiki cha pekee kila siku isipokuwa siku ya Sabato. Kuhusu maana ya neno hilo la Kiebrania taz Kut 16:14-16 maelezo.]
7Mana ilikuwa kama punje za mtama, rangi yake ilikuwa kama ya bedoza.
8Watu walizungukazunguka na kuikusanya, kisha waliisaga kwa mawe ya kusagia au waliitwanga kwa vinu, halafu waliitokosa vyunguni na kutengeneza maandazi. Ladha yake ilikuwa kama ya maandazi yaliyokaangwa kwa mafuta.
9(Umande ulipoanguka kambini wakati wa usiku, mana pia ilianguka pamoja na huo umande).
10Mose alisikia watu wakilia katika familia zote, kila mtu penye lango la hema lake. Basi, hasira ya Mwenyezi-Mungu iliwaka sana; naye Mose alichukizwa.
11Ndipo Mose alipomwambia, Mwenyezi-Mungu “Kwa nini unanitendea vibaya mimi mtumishi wako? Mbona hupendezwi nami, kwa nini umenitwika mzigo wa kuwatunza watu wote hawa?
12Je, ni mimi niliyewazaa, hata ukaniambia niwabebe kifuani pangu kama mlezi abebavyo mtoto mchanga, na kuwapeleka mpaka nchi uliyoapa kuwapa babu zao?
13Nitapata wapi nyama ya kuwalisha watu hawa wote? Maana wanalia mbele yangu wakisema: ‘Tupe nyama tule!’
14Siwezi kuwatunza watu wote hawa peke yangu; hilo ni jukumu kubwa mno kwangu!
15Ikiwa hivi ndivyo utakavyonitenda, afadhali uniue mara moja! Kama ninapata kibali mbele yako, usiniache niikabili taabu yangu.”
16Basi, Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Wakusanyeni wazee sabini wa Israeli, ambao wewe unajua wanaheshimiwa na kukubaliwa na watu kuwa viongozi, uwalete kwenye hema la mkutano, wasimame karibu nawe.[#11:16 Idadi sabini (saba mara kumi), katika Biblia mara nyingine ni idadi inayoashiria ukamilifu kama vile saba katika siku saba za kuumbwa ulimwengu. Vilevile ni namba muhimu ya kimfano. Hao wazee yamkini walikuwa watu waliokuwa na umri mkubwa katika jumuiya na hivyo walipata kuongoza koo za makabila yao. Taz Kut 18:13-25.]
17Nitashuka huko na kuzungumza nawe; nitachukua sehemu ya roho niliyokupa, niwape watu hao. Nao watabeba jukumu la kuwatunza watu hawa pamoja nawe, usije ukaubeba mzigo huo peke yako.
18Sasa waambie watu hivi: Jitakaseni kwa ajili ya kesho; mtakula nyama. Mwenyezi-Mungu amesikia mkilia na kusema kuwa hakuna wa kuwapeni nyama, na kwamba hali yenu ilikuwa nzuri zaidi mlipokuwa Misri. Sasa Mwenyezi-Mungu atawapeni nyama, nanyi sharti muile.[#11:18 Waisraeli walitakiwa kujiweka katika hali inayofaa kidini: kutawadha, kufua nguo zao na kuepa kujamiiana, wawe tayari kupokea zawadi ya Mungu. Taz Kut 19:10-15.]
19Mtakula nyama si kwa muda wa siku moja tu, au mbili, au tano, au kumi au ishirini,
20bali kwa muda wa mwezi mzima! Mtaila hadi iwatoke puani, mpaka muikinai. Yote hayo ni kwa sababu mmemkataa Mwenyezi-Mungu aliye hapahapa miongoni mwenu, na kulia mbele yake mkisema, ‘Kwa nini tulitoka Misri?’”
21Lakini Mose alimwambia Mwenyezi-Mungu, “Idadi ya watu ninaowaongoza hapa ni 600,000 waendao kwa miguu, nawe wasema, ‘Nitawapa nyama ya kuwatosha mwezi mzima!’[#11:21 Watu hao ni idadi ya watu ambao wangeweza kuwa askari wa Waisraeli (taz Kut 12:37; Hes 1:20-46).]
22Je, panaweza kuchinjwa kondoo na ng'ombe wa kuwatosheleza? Je, samaki wote baharini wavuliwe kwa ajili yao?”
23Mwenyezi-Mungu akamjibu Mose, “Je, uwezo wangu umepungua? Utaona basi kama neno langu litakuwa la kweli kwako au la.”
24Basi, Mose akaenda na kuwajulisha watu yale aliyosema Mwenyezi-Mungu. Kisha, akakusanya wazee sabini kutoka miongoni mwa wazee viongozi nao akawaweka kandokando kuizunguka hema.
25Hapo, Mwenyezi-Mungu akashuka katika wingu na kuzungumza naye. Halafu akatwaa sehemu ya roho aliyokuwa amempa Mose, akawapa kila mmoja wa wale wazee sabini. Walipoingiwa na roho hiyo, wazee hao walianza kutoa unabii, lakini hawakurudia kufanya hivyo.[#11:25 Hapa “roho” ni nguvu ya pekee ya Mungu, nguvu ambayo alimpa Mose apate kuwaongoza Waisraeli. Mwandishi anasema kwamba sehemu ya nguvu hiyo aliwapa pia hao wazee nao wakaanza kutabiri au kutoa unabii. Mungu aliwashirikisha hao wazee kipaji kile kile alichokuwa amempa Mose. Lakini, tunaambiwa, kipaji hicho hakikuwa cha kudumu. Taz pia kama mfano wa tukio hilo 1Sam 10:5-6; 19:20-24.]
26Wazee wawili kati ya wale sabini waliochaguliwa, Eldadi na Medadi, walikuwa wamebaki kambini wenzao walipokwenda kwenye hema. Roho iliwajia humohumo kambini, wakaanza kutoa unabii mahali walipokuwa.
27Kijana mmoja alitoka mbio na kumwambia Mose, “Eldadi na Medadi wanatoa unabii kambini.”
28Hapo, Yoshua, mwana wa Nuni, ambaye alikuwa msaidizi wa Mose tangu ujana wake, akamwambia Mose, “Bwana wangu, wakataze!”
29Lakini Mose akamjibu, “Je, unaona wivu kwa ajili yangu? Laiti Mwenyezi-Mungu angewapa watu wake wote roho yake nao wakawa manabii!”
30Kisha Mose alirudi kambini pamoja na wale wazee sabini wa Israeli.
31Baadaye Mwenyezi-Mungu akavumisha upepo kwa ghafla, ukaleta kware kutoka baharini na kuwafanya watue kando ya kambi, mwendo wa siku moja hivi kila upande kuizunguka kambi, wakarundikana chini karibu kimo cha mita moja hivi.[#11:31 Yamkini ni bahari ambamo kuna ghuba ya Akaba.]
32Basi, siku hiyo yote, kutwa kucha, na siku iliyofuata watu walishughulika kukusanya kware; hakuna mtu aliyekusanya chini ya kilo 1,000. Wakawaanika kila mahali kandokando ya kambi ili wawakaushe.
33Kulipokuwa bado kuna nyama kwa wingi na kabla watu hawajawamaliza kuila, Mwenyezi-Mungu aliwakasirikia watu, akawapiga watu kwa pigo kubwa sana.[#11:33 Watu walitakiwa kuokota tu kiasi cha kutosha kwa siku, jambo ambalo lingewafanya wawe na imani na Mungu mwenye kuwajalia mahitaji ya siku kwa siku; lakini wakaona afadhali wajiwekee kwa siku zilizofuata.]
34Kwa hiyo mahali hapo palipewa jina Kibroth-hataava; kwa sababu huko ndiko walikowazika watu waliokuwa walafi.[#11:34 Maana yake “makaburi ya watu wenye tamaa” au “makaburi ya walafi”. Taz pia Kumb 9:22.]
35Kutoka hapo Kibroth-hataava watu walisafiri mpaka Haserothi, wakapiga kambi yao na kukaa huko.[#11:35 Yafikiriwa kuwa ni mahali pajulikanapo siku hizi kwa jina “Ain el-Huderah”, yapata kilomita arubaini kaskazini-mashariki ya mlima Sinai (taz pia 12:16; 33:17-18; Kumb 1:1).]