Hesabu 13

Hesabu 13

Wapelelezi

(Kumb 1:19-33)

1Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose,

2“Tuma watu waende wakaipeleleze nchi ya Kanaani ambayo ninawapa wana wa Israeli. Utatuma mtu mmoja kutoka katika kila kabila, na mtu huyo lazima awe kiongozi katika kabila lake.”

3Basi, kwa mujibu wa agizo la Mwenyezi-Mungu, Mose akatuma watu kutoka jangwa la Parani. Watu wote waliotumwa walikuwa viongozi wa makabila mbalimbali ya wana wa Israeli.

4Ifuatayo ndiyo orodha ya majina ya watu hao:

Kabila la Reubeni, Shamua mwana wa Zakuri.

5Kabila la Simeoni, Shafati mwana wa Hori.

6Kabila la Yuda, Kalebu mwana wa Yefune.

7Kabila la Isakari, Igali mwana wa Yosefu.

8Kabila la Efraimu, Hoshea mwana wa Nuni.

9Kabila la Benyamini, Palti mwana wa Rafu.

10Kabila la Zebuluni, Gadieli mwana wa Sodi.

11Kabila la Yosefu (yaani kabila la Manase), Gadi mwana wa Susi.

12Kabila la Dani, Amieli mwana wa Gemali.

13Kabila la Asheri, Sethuri mwana wa Mikaeli.

14Kabila la Naftali, Nabi mwana wa Wofsi.

15Kabila la Gadi, Geueli mwana wa Maki.

16Haya ndiyo majina ya watu ambao Mose aliwatuma kwenda kuipeleleza nchi ya Kanaani. Mose alimpa Hoshea mwana wa Nuni jina jipya, akamwita Yoshua.[#13:16 Majina hayo mawili ni mitindo miwili ya kuandika jina lile lile ambalo lina maana ya “Mwenyezi-Mungu (Yahweh) aokoa”. Kwa kuandika jina hilo hilo Kigiriki tunapata pia jina Yesu (taz Mat 1:21 maelezo).]

17Alipowatuma kwenda kuipeleleza nchi ya Kanaani, Mose aliwaambia: “Nendeni juu kule Negebu, hadi kwenye nchi ya milima,[#13:17-22 Aya hizi zinaeleza kinaganaga safari ya hao wapelelezi. Kutoka Kadeshi (13:26) wanasafiri katika jangwa la Negebu (taz Mwa 12:9 maelezo), mpaka kufika Hebroni (aya 22) ambao ni mji kwenye nyanda za juu zilizojulikana kama nchi ya Yuda au Yudea (taz Mwa 13:18 maelezo). Kutoka huko walielekea sehemu ya kaskazini ya nchi ya Kanaani (aya 21).]

18mkaipeleleze nchi ilivyo. Chunguzeni pia kama watu wanaoishi humo ni wenye nguvu au dhaifu, wengi au wachache.

19Pelelezeni kama nchi hiyo ni nzuri au mbaya, na kama miji wanamoishi ni kambi au ni nyumba zilizozungukwa na ngome.

20Chunguzeni pia kama nchi yenyewe ni tajiri au maskini, ina miti au haina. Muwe na mioyo ya ujasiri na mnaporudi chukueni baadhi ya matunda ya nchi hiyo.” Hayo yalikuwa majira ya zabibu zianzapo kuiva.

21Basi, watu hao wakaenda na kuipeleleza nchi toka jangwa la Sini hadi Rehobu, karibu na njia ya kuingilia Hamathi.

22Walikwenda hadi Negebu wakapita mpaka mji wa Hebroni. Humo waliwakuta Waahimani, Washeshai na Watalmai, wazawa wa Anaki. (Mji wa Hebroni ulikuwa umejengwa miaka saba kabla ya mji wa Soani ulioko nchini Misri).[#13:22 Hao walikuwa watu warefu na hodari wa vita (taz aya 32-33).]

23Walipofika katika Bonde la Eshkoli, watu hao walikata shada la mzabibu lililokuwa na matunda mengi nalo lilibebwa na watu wawili juu ya mti. Walichukua pia makomamanga kadhaa na tini.[#13:23 Maana yake ni “shada la zabibu.”]

24Mahali hapo paliitwa Bonde la Eshkoli kwa sababu ya shada ambalo watu hao wa Israeli walikata kutoka mahali hapo.

25Baada ya kuipeleleza nchi kwa muda wa siku arubaini, watu hao walirudi.

26Waliwaendea Mose, Aroni na jumuiya ya Waisraeli huko Kadeshi, katika jangwa la Parani, wakatoa taarifa ya mambo waliyoyaona na kuwaonesha matunda ya nchi.[#13:26 Mji huo unaitwa pia “Kadesh-barnea” na ulikuwa mji jangwani ambapo kulikuwa na maji na miti (Hes 34:3-4; Yos 15:1,3).]

27Walimwambia Mose, “Tuliifikia nchi uliyotutuma tuipeleleze; hiyo ni nchi inayotiririka maziwa na asali, na hili ni tunda lake.[#13:27 Msemo ambao unatumika mara kwa mara katika vitabu vya kwanza vya Biblia kueleza hali ya rutuba ya nchi ya Kanaani (taz Kut 3:8 maelezo).]

28Lakini wenyeji wake ni wenye nguvu sana, na miji yao ni imara na mikubwa sana. Zaidi ya hayo, huko tuliona wazawa wa Anaki.

29Waamaleki wanakaa katika eneo la Negebu; Wahiti, Wayebusi na Waamori wanakaa katika eneo la milima, na Wakanaani wanakaa karibu na bahari ya Mediteranea na karibu na kingo za mto Yordani.”[#13:29 Waamaleki walikuwa watu waliohamahama ambao waliishi eneo la kusini na mashariki ya Bahari ya Chumvi. Walikuwa maadui wa Waisraeli (Kut 17:8-14). Nao Wahiti walikuwa watu wenye nguvu ambao walikuwa wazawa wa Hethi mjukuu wake Hamu (Mwa 10:6-20). Hao walimiliki nchi ya Kanaani tangu wakati wa Abrahamu hadi karne ya 12 K.K. Wayebusi nao walitawala Yerusalemu mpaka wakati Daudi alipowafukuza humo (2Sam 5:6-9). Waamori waliishi katika nyanda za juu za nchi ya Kanaani wakati Waisraeli walipoivamia (Yos 2:10). Wakanaani walikuwa wazawa wa Hamu, mwanawe Noa (Mwa 10:6-20); waliishi katika maeneo karibu na mto Yordani na kando ya Bahari ya Mediteranea kaskazini ya Yerusalemu.]

30Lakini Kalebu aliwanyamazisha watu mbele ya Mose, akasema, “Twende mara moja tukaimiliki nchi hiyo. Kwa kuwa tunao uwezo sana wa kushinda.”

31Lakini watu walioandamana naye kuipeleleza nchi wakasema, “Hatutaweza kupigana na watu hao; wao wana nguvu kuliko sisi.”

32Kwa hiyo wakaeneza mambo ya uongo kati ya wana wa Israeli kuhusu nchi waliyoipeleleza, wakisema, “Nchi hiyo inawaua watu wake. Pia watu wote tuliowaona huko ni wakubwa sana.

33Tuliona majitu huko, wazawa wa Anaki. Sisi tulijiona kuwa kama panzi mbele yao, na ndivyo walivyotuona sisi.”[#13:33 Neno au jina linalotafsiriwa hapa kama “majitu” Kiebrania ni “nefilim”. Hapa wanaitwa wazawa wa Anaki lakini katika Mwa 6:1-4 wanasemekana kuwa ni wazawa wa akina mama wa kibinadamu na kina baba wa kimbingu.]

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania