Hesabu 20

Hesabu 20

Maji ya Meriba

(Kut 17:1-7)

1Jumuiya nzima ya Waisraeli ilifika katika jangwa la Sinai mnamo mwezi wa kwanza, wakapiga kambi yao huko Kadeshi. Wakiwa huko, Miriamu alifariki, akazikwa.[#20:1 Eneo hili labda lilikuwa kaskazini-mashariki mwa jangwa la Parani.]

2Mahali hapo walipopiga kambi hapakuwa na maji. Kwa hiyo watu jumuiya yote, wakakusanyika kinyume cha Mose na Aroni.[#20:2 Simulizi hili linataja manung'uniko au malalamiko kadhaa ya Waisraeli kule jangwani (taz Hes 11:1 maelezo).]

3Waliwalalamikia wote wakisema, “Afadhali tungekufa pamoja na ndugu zetu mbele ya hema la Mwenyezi-Mungu!

4Kwa nini mlituleta sisi jumuiya ya Mwenyezi-Mungu huku jangwani? Je, mlituleta ili tufe pamoja na mifugo yetu?

5Na, kwa nini mlitutoa Misri na kutuleta mahali hapa pabaya hivi? Hapa si mahali pa nafaka, tini, zabibu wala makomamanga. Hata maji ya kunywa hakuna!”

6Hapo, Mose na Aroni waliondoka kwenye umati wa watu, wakaenda kusimama kwenye mlango wa hema la mkutano, wakasujudu. Basi, utukufu wa Mwenyezi-Mungu ukawatokea,

7naye Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose,

8“Twaa ile fimbo yako, kisha wewe na Aroni ndugu yako, muikusanye jumuiya yote ya watu. Halafu, mbele ya macho yao, uuambie mwamba ulio mbele ya macho yao utoe maji yake. Naam, utaufanya mwamba utoe maji, ili jumuiya nzima ya watu na mifugo yao waweze kunywa.”

9Mose akaenda kuichukua ile fimbo mbele ya Mwenyezi-Mungu kama alivyoamriwa.

10Kisha Mose na Aroni wakaikusanya jumuiya yote ya watu mbele ya mwamba, naye Mose akawaambia, “Sikilizeni sasa, enyi waasi: je, tuwatoleeni maji kutoka mwamba huu?”

11Kisha Mose akainua mkono wake, akaupiga ule mwamba mara mbili kwa fimbo yake. Maji yakabubujika kwa wingi, watu wakanywa pamoja na mifugo yao.

12Lakini Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose na Aroni, “Kwa kuwa nyinyi hamkuniamini mimi, wala kunistahi mbele ya macho ya Waisraeli, basi kwa sababu hiyo hamtaiingiza jumuiya hii katika ile nchi niliyowapa.”[#20:12 Ingawa hapa si dhahiri kosa hilo lilikuwaje, mahali pengine katika Biblia kosa la Mose na Aroni linatajwa kuwa ni kukosa kumtii Mungu (Hes 20:24; 27:14).]

13Hayo ni maji ya Meriba, mahali ambapo Waisraeli walimnung'unikia Mwenyezi-Mungu, naye alijionesha kwa utakatifu kati yao.[#20:13 Kiebrania jina hili lina maana ya “kunung'unika”. Taz pia Zab 95:8.]

Mfalme wa Edomu anawazuia Waisraeli kupita

14Mose alipeleka wajumbe kutoka Kadeshi kwa mfalme wa Edomu akamwambia: “Ndugu yako, Israeli, asema hivi: Wewe wazijua taabu zote tulizozipata.[#20:14 Hii ni ripoti ya jumla; jina la mfalme mhusika halitajwi popote katika Biblia. Taz pia Amu 11:16-18; Kumb 23:7; Oba 1:10,12. Waedomu walikuwa wazawa wa Esau (Mwa 25:24-26; 36:1). Eneo la Edomu lilikuwa kusini mwa Bahari ya Chumvi, kati ya jangwa la Sini na nchi ya Moabu.]

15Jinsi babu zetu walivyokwenda Misri, ambako tuliishi kwa muda mrefu na jinsi Wamisri walivyowatesa babu zetu, wakatutesa na sisi pia.

16Tulimlilia Mwenyezi-Mungu, naye akakisikia kilio chetu, akatuletea malaika aliyetuondoa Misri. Sasa tuko hapa Kadeshi, mji unaopakana na nchi yako.[#20:16 Taz Kut 23:20-33 maelezo.]

17Tafadhali uturuhusu tupite nchini mwako. Hatutakanyaga mashamba yenu, wala yale ya mizabibu; wala hatutakunywa maji ya visima vyenu. Tutaifuata barabara kuu ya mfalme na kwenda moja kwa moja bila kugeuka kulia au kushoto, mpaka tutakapotoka katika nchi yako.”[#20:17 Hiyo ilikuwa barabara muhimu sana kwa biashara; ilianza kwenye Ghuba ya Akaba, ikapitia upande wa mashariki mwa Mto Yordani kupitia nchi za Edomu, Moabu na Amoni. Taz Hes 21:22; Kumb 2:27.]

18Lakini mfalme wa Edomu akamjibu, “La! hutapita katika nchi yangu, kama ukipita nitatoka na kukushambulia kwa upanga.”

19Waisraeli wakamwambia, “Sisi tutafuata njia kuu; kama sisi na mifugo yetu tukinywa maji yenu, tutalipa. Tunachoomba tafadhali turuhusu tu, tupite kwa miguu wala hatutaki neno lolote lingine.”

20Lakini mfalme wa Edomu akasisitiza: “Hatutawaruhusu.” Mara, Waedomu wenye nguvu wakatoka kupigana nao.

21Basi, Waedomu wakakataa kuwapa ruhusa Waisraeli kupita katika mipaka yao. Waisraeli wakageuka na kushika njia nyingine.

Kifo cha Aroni

22Waisraeli wote walisafiri kutoka Kadeshi, wakafika kwenye Mlima Hori.[#20:22-23 Mlima huu ambao ni tofauti na ule unaotajwa katika Hes 34:7-8 haujulikani ulipo.]

23Basi, Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose na Aroni huko kwenye Mlima Hori, mpakani mwa nchi ya Edomu,

24“Aroni atakufa; hataingia katika nchi ambayo nimewapa watu wa Israeli kwa sababu nyinyi wawili mliiasi amri yangu kule Meriba[#20:24 Kuhusu uasi huo wa Mose na Aroni taz aya 20:12 maelezo.]

25Mchukue Aroni na Eleazari mwanawe, uwalete juu ya Mlima Hori.[#20:25-28 Mwanawe Aroni ambaye alichukua mahali pake kama kuhani au mtambikaji. Taz maelezo ya aya 13. Taz pia Mwa 25:8; Hes 27:13; Isa 57:1-2; Ebr 12:23.]

26Kisha, mvue Aroni mavazi yake rasmi, umvalishe mwanawe Eleazari. Aroni atakufa akiwa huko mlimani.”

27Mose alifanya kama alivyoamriwa na Mwenyezi-Mungu. Wote watatu walipanda mlimani mbele ya jumuiya yote ya watu.

28Kisha Mose alimvua Aroni mavazi yake rasmi, akamvalisha mwanawe, Eleazari. Naye Aroni akafa palepale mlimani. Kisha Mose na Eleazari wakateremka chini.

29Jumuiya yote ya watu ilipopata habari kwamba Aroni amefariki, ikafanya matanga ya siku thelathini.[#20:29 Kwa desturi matanga yalifanyika kwa siku saba (Mwa 50:10; 1Sam 31:13) lakini hapa yalifanywa kwa siku hizo thelathini.]

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania