Hesabu 21

Hesabu 21

Ushindi huko Horma

1Mfalme mmoja Mkanaani wa Aradi aliyeishi huko Negebu alipopata habari kwamba Waisraeli walikuwa wanakuja kwa njia ya Atharimu, alikwenda kuwashambulia, akawateka baadhi yao.[#21:1-3: Hapa unatajwa ushindi wa kwanza wa Waisraeli dhidi ya Wakanaani baada ya kushindwa kwao kule Horma (Hes 14:39-45).]

2Hapo, Waisraeli wakamwekea Mwenyezi-Mungu nadhiri wakisema: “Kama utawatia watu hawa mikononi mwetu, basi tutaiangamiza kabisa miji yao.”[#21:2 Maneno haya yanagusia desturi iliyokuwa kawaida miongoni mwa watu wa Mashariki ya Kati ya Kale ambayo kwa Kiebrania iliitwa “kherem”. Desturi hiyo ilihusu kuweka wakfu au kutenga vitu fulani kwa ajili ya mungu. Kwa kawaida vitu hivyo viliteketezwa na hivyo kuvifanya visiweze kutumiwa na mtu. Taz Kumb 7:23-26; 13:12-16; 20:10-18.]

3Mwenyezi-Mungu akalisikia ombi lao, akawapa ushindi juu ya Wakanaani. Waisraeli wakawaangamiza kabisa Wakanaani pamoja na miji yao. Kwa hiyo mahali hapo pakaitwa Horma.[#21:3 Jina hili la Kiebrania linafanana kimatamshi na neno “kherem” na hapa lina maana ya “maangamizi”.]

Nyoka wa shaba

4Waisraeli walifunga safari kutoka Mlima Hori wakapitia njia inayoelekea bahari ya Shamu ili waizunguke nchi ya Edomu. Lakini njiani watu walikufa moyo.

5Basi, wakaanza kumnung'unikia Mungu na Mose, wakisema, “Kwa nini mmetutoa Misri tuje tukafie humu jangwani? Humu hamna chakula wala maji; nasi tumechoshwa na chakula hiki duni.”

6Hapo Mwenyezi-Mungu akapeleka nyoka wenye sumu miongoni mwa watu, wakawauma hata Waisraeli wengi wakafa.[#21:6 Neno linalotafsiriwa hapa kama “nyoka wenye sumu” linatokana na neno lenye maana ya “moto” na kwa sababu hiyo wengi wanafikiri nyoka hao walisababisha maumivu makali kama ya kuchomwa na moto.]

7Basi, watu wakamwendea Mose, wakamwambia, “Tumetenda dhambi kwa kumnung'unikia Mwenyezi-Mungu na wewe pia. Mwombe Mwenyezi-Mungu atuondolee nyoka hawa.” Kwa hiyo, Mose akawaombea watu.

8Ndipo Naye Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Tengeneza nyoka wa shaba, umtundike juu ya mlingoti. Mtu yeyote atakayeumwa na nyoka, akimtazama nyoka huyo wa shaba, atapona.”[#21:8 Baadhi ya watu wa kale waliamini kwamba nyoka ni kiumbe hatari mno na aliweza tu kupunguzwa nguvu zake kwa kutengeneza sanamu yake. Sanamu ya nyoka wa shaba ilifanyiwa ibada huko Palestina mpaka wakati ilipoteketezwa na mfalme Hezekia (2Fal 18:4). Taz pia Yoh 3:13-14.]

9Basi, Mose akatengeneza nyoka wa shaba, akamtundika juu ya mlingoti. Kila mtu aliyeumwa na nyoka alipomtazama nyoka huyo wa shaba, alipona.

Safari hadi bonde la Wamoabu.

10Waisraeli waliendelea na safari yao, wakapiga kambi huko Obothi.

11Kutoka huko walisafiri mpaka Iye-abarimu, katika jangwa upande wa mashariki, mwa Moabu.

12Kutoka huko walisafiri wakapiga kambi yao katika bonde la Zeredi.

13Kutoka huko walisafiri, wakapiga kambi kaskazini ya mto Arnoni, ambao hutiririka kutoka katika nchi ya Waamori na kupitia jangwani. Mto Arnoni ulikuwa mpaka kati ya Wamoabu na Waamori.

14Kwa sababu hiyo, imeandikwa katika kitabu cha vita vya Mwenyezi-Mungu:[#21:14 Kitabu hiki ambacho kinatajwa hapa tu katika Biblia, huenda kilikuwa mkusanyo wa tenzi au nyimbo za vita mithili ya kitabu kile kinachotajwa katika Yos 10:1 kama “kitabu cha Yashari” (taz Yos 10:13 maelezo).]

“Mji wa Wahebu nchini Sufa,

na mabonde ya Arnoni,

15na mteremko wa mabonde

unaofika hadi mji wa Ari,

na kuelekea mpakani mwa Moabu!”

16Kutoka huko Waisraeli walisafiri mpaka Beeri; yaani kisima ambapo Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose, “Wakusanyeni watu pamoja, nami nitawapa maji.”

17Hapo Waisraeli waliimba wimbo huu:

“Bubujika maji ee kisima! — Kiimbieni!

18Kisima kilichochimbwa na wakuu

kilichochimbwa sana na wenye cheo,

kwa fimbo zao za enzi na bakora.”

Kutoka jangwani walisafiri mpaka Matana,

19kutoka Matana mpaka Nahalieli, kutoka Nahalieli mpaka Bamothi,

20na kutoka Bamothi mpaka kwenye bonde linaloingia nchi ya Moabu, kwenye kilele cha Mlima Pisga, kielekeacho chini jangwani.

Waisraeli wanawashinda wafalme Sihoni na Ogu

(Kumb 2:26—3:1)

21Waisraeli walimpelekea mfalme Sihoni wa Waamori, ujumbe huu:[#21:21 Eneola Waamori lilikuwa upande wa mashariki wa mto Yordani, kaskazini ya nchi ya Waamoni. Huyo mfalme Sihoni anaitwa pia “mfalme wa Heshboni” (Hes 21:25; Kumb 1:4; Yos 12:2).]

22“Turuhusu tupite katika nchi yako; hatutakwenda pembeni na kuingia mashambani au katika mashamba ya mizabibu, wala hatutakunywa maji ya visima vyenu; tutapita moja kwa moja katika barabara kuu ya mfalme mpaka tumeondoka nchini mwako.”

23Lakini Sihoni hakuwaruhusu watu wa Israeli wapite katika nchi yake. Aliwakusanya watu wake, akaenda Yahasa Jangwani kuwashambulia Waisraeli.

24Lakini Waisraeli walimuua, wakaitwaa nchi yake tangu mto Arnoni hadi mto Yaboki, yaani hadi mpaka wa nchi ya Waamoni ambao ulikuwa unalindwa sana.[#21:24 Waamoni na Waamori walitokana na babu mmoja na mataifa hayo mawili yalikuwa maadui wa Waisraeli (taz Amu 10:11-18; 1Sam 14:47-48; 2Fal 3:21-27).]

25Waisraeli waliiteka miji hii yote nao wakaishi katika miji ya Waamori katika Heshboni na vitongoji vyake.

26Heshboni ulikuwa mji wa Sihoni mfalme wa Waamori, ambaye hapo awali alikuwa amepigana na mfalme wa Moabu na kuiteka nchi yake yote mpaka mto Arnoni.

27Ndiyo maana washairi wetu huimba:

“Njoni Heshboni na kujenga.

Mji wa Sihoni na ujengwe na kuimarishwa.

28Maana moto ulitoka Heshboni,

miali ya moto ilitoka mjini kwa Sihoni,

uliuteketeza mji wa Ari wa Moabu,

ukaiangamiza milima ya mto Arnoni.

29Ole wenu watu wa Moabu!

Mmeangamizwa, enyi watu wa mungu Kemoshi!

Umewafanya watoto wenu wa kiume kuwa wakimbizi,

binti zako umewaacha wachukuliwe mateka

mpaka kwa Sihoni, mfalme wa Amori.

30Lakini sasa wazawa wao wameangamizwa,

kutoka Heshboni mpaka Diboni,

kutoka Nashimu mpaka Nofa, karibu na Medeba.”

31Basi, Waisraeli wakakaa katika nchi ya Waamori.

32Kisha Mose alituma watu wapeleleze mji wa Yazeri; wakauteka pamoja na vitongoji vyake, wakawafukuza Waamori waliokaa humo.

33Waisraeli waligeuka wakafuata njia iendayo Bashani. Mfalme Ogu wa Bashani akatoka na jeshi lake kuwashambulia huko Edrei.

34Lakini Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Usimwogope, maana nimemtia mikononi mwako pamoja na watu wake wote na nchi yake yote. Utamtendea kama ulivyomtendea Sihoni, mfalme wa Waamori, aliyekuwa anakaa Heshboni.”

35Basi, Waisraeli wakamuua Ogu, wanawe na watu wake wote, bila kumwacha hata mtu mmoja, kisha wakaitwaa nchi yake.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania