Zaburi 30

Zaburi 30

Sala ya shukrani

1Ee Mwenyezi-Mungu, nakutukuza maana umeniokoa,

wala hukuwaacha maadui zangu wanisimange.

2Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu,

nilikulilia msaada, nawe ukaniponya.

3Ee Mwenyezi-Mungu, umeniokoa kutoka kuzimu;

umenipa tena uhai,

umenitoa miongoni mwa waendao kuzimu.

4Mwimbieni Mwenyezi-Mungu sifa, enyi waaminifu wake;

kumbukeni utakatifu wake na kumshukuru.

5Hasira yake hudumu kitambo kidogo,

wema wake hudumu milele.

Kilio chaweza kuwapo hata usiku,

lakini asubuhi huja furaha.

6Mimi nilipofanikiwa, nilisema:

“Kamwe sitashindwa!”

7Kwa wema wako, ee Mwenyezi-Mungu,

umeniimarisha kama mlima mkubwa.

Lakini ukajificha mbali nami,

nami nikafadhaika.

8Nilikulilia wewe, ee Mwenyezi-Mungu;

naam niliomba dua kwako ee Mwenyezi-Mungu:

9“Je, utapata faida gani nikifa

na kushuka hadi kwa wafu?

Je, mavumbi ya wafu yanaweza kukusifu?

Je, yanaweza kusimulia uaminifu wako?

10Usikie, ee Mwenyezi-Mungu, unihurumie;

ee Mwenyezi-Mungu, unisaidie!”

11Wewe umegeuza maombolezo langu kuwa ngoma ya furaha;

umeniondolea huzuni yangu, ukanizungushia furaha.

12Mimi nitakusifu wala sitakaa kimya.

Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu nitakushukuru milele.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania