1 Samweli 3

1 Samweli 3

Bwana amwita Samweli

1Kijana Samweli alihudumu mbele za Bwana chini ya Eli. Katika siku zile neno la Mungu lilikuwa adimu, hapakuwa na maono mengi.

2Usiku mmoja Eli, ambaye macho yake yalikuwa yamefifia sana kiasi kwamba aliona kwa shida sana, alikuwa amelala mahali pake pa kawaida.

3Taa ya Mungu bado ilikuwa haijazimika, na Samweli alikuwa amelala hekaluni mwa Bwana , ambapo Sanduku la Mungu lilikuwa.[#3:3 Hekaluni maana yake ndani ya Maskani ya .]

4Kisha Bwana akamwita Samweli.

Samweli akajibu, “Mimi hapa.”

5Naye akakimbia kwa Eli na kumwambia, “Mimi hapa, kwa kuwa umeniita.”

Lakini Eli akasema, “Sikukuita; rudi ukalale.” Hivyo akaenda kulala.

6Bwana akaita tena, “Samweli!” Naye Samweli akaamka, kwenda kwa Eli na kusema, “Mimi hapa, kwa kuwa umeniita.”

Eli akasema, “Mwanangu, sikukuita, rudi ukalale.”

7Wakati huu Samweli alikuwa bado hajamjua Bwana . Neno la Bwana lilikuwa bado halijafunuliwa kwake.

8Bwana akamwita Samweli mara ya tatu, naye Samweli akaamka kwenda kwa Eli na kusema, “Mimi hapa, kwa kuwa umeniita.”

Ndipo Eli akatambua kuwa Bwana alikuwa akimwita kijana.

9Hivyo Eli akamwambia Samweli, “Nenda ukalale; akikuita, sema, ‘Nena Bwana , kwa kuwa mtumishi wako anasikiliza.’ ” Hivyo Samweli akaenda na kulala mahali pake.

10Bwana akaja, akasimama pale, akiita kama hapo awali, “Samweli! Samweli!”

Kisha Samweli akasema, “Nena Bwana , kwa kuwa mtumishi wako anasikiliza.”

11Naye Bwana akamwambia Samweli: “Tazama, nipo karibu kufanya kitu katika Israeli ambacho kitafanya masikio ya kila mmoja atakayesikia yawashe.

12Wakati huo nitatimiza dhidi ya Eli kila kitu nilichonena dhidi ya jamaa yake, kuanzia mwanzo hadi mwisho.

13Kwa kuwa nilimwambia kwamba ningehukumu jamaa yake milele kwa sababu ya dhambi aliyoijua, wanawe kumkufuru Mungu, naye akashindwa kuwazuia.

14Kwa hiyo, nikaapa kuhusu nyumba ya Eli, ‘Hatia ya nyumba ya Eli kamwe haitaweza kufidiwa kwa dhabihu au sadaka.’ ”

15Samweli akalala hadi asubuhi, kisha akafungua milango ya nyumba ya Bwana . Aliogopa kumwambia Eli yale maono,

16lakini Eli akamwita na kumwambia, “Samweli mwanangu.”

Samweli akamjibu, “Mimi hapa.”

17Eli akamuuliza, “Ni nini alichokuambia? Usinifiche. Bwana na akuadhibu vikali zaidi kama utanificha chochote alichokuambia.”

18Kwa hiyo Samweli akamwambia kila kitu bila kumficha chochote. Ndipo Eli akasema, “Yeye ni Bwana ; na afanye lile lililo jema machoni pake!”

19Bwana alikuwa pamoja na Samweli alipokuwa akikua, na hakuacha neno lolote la Samweli lianguke chini.

20Nao Israeli wote kuanzia Dani hadi Beer-Sheba wakatambua kuwa Samweli amethibitishwa kuwa nabii wa Bwana .

21Bwana akaendelea kutokea huko Shilo, na huko alijidhihirisha kwa Samweli kupitia neno lake.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.