2 Nyakati 28

2 Nyakati 28

Ahazi mfalme wa Yuda

(2Fal 16:1‑6)

1Ahazi alikuwa na umri wa miaka ishirini alipoanza kutawala. Akatawala huko Yerusalemu kwa miaka kumi na sita. Tofauti na Daudi baba yake, hakufanya yaliyo mema machoni pa Bwana .

2Akaenenda katika njia za wafalme wa Israeli, na pia akasubu sanamu kwa ajili ya kuabudu Mabaali.

3Akatoa sadaka za kuteketezwa katika Bonde la Ben-Hinomu, na kuwatoa kafara watoto wake kwa kuwateketeza kwa moto, akifuata njia za machukizo za yale mataifa Bwana aliyoyafukuza humo mbele ya Waisraeli.

4Akatoa sadaka na kufukiza uvumba katika mahali pa juu pa kuabudia, juu ya vilima, na chini ya kila mti uliotanda.

5Kwa hiyo Bwana Mungu wake akamtia mikononi mwa mfalme wa Aramu. Waaramu wakamshinda, wakachukua watu wake wengi mateka na kuwaleta Dameski.

Tena alitiwa mikononi mwa mfalme wa Israeli, ambaye aliwaua watu wake wengi.

6Kwa siku moja Peka mwana wa Remalia aliwaua askari elfu mia moja na ishirini katika Yuda, kwa kuwa Yuda walikuwa wamemwacha Bwana , Mungu wa baba zao.

7Zikri, askari shujaa Mwefraimu, akamuua Maaseya mwana wa mfalme, Azrikamu mkuu wa jumba la kifalme na Elkana aliyekuwa wa pili kwa mfalme.

8Waisraeli wakawachukua mateka kutoka ndugu zao, watu wapatao elfu mia mbili, wakiwa wanawake, pamoja na watoto wa kiume na wa kike. Wakachukua pia kiasi kikubwa cha nyara, ambazo walirudi nazo Samaria.

9Lakini huko kulikuwa na nabii wa Bwana aliyeitwa Odedi; akaondoka ili kukutana na jeshi liliporejea Samaria. Akawaambia, “Kwa kuwa Bwana , Mungu wa baba zenu, aliwakasirikia Yuda, aliwatia mikononi mwenu. Lakini mmewachinja kwa hasira ambayo imefika hadi mbinguni.

10Nanyi sasa mnakusudia kuwafanya wanaume na wanawake wa Yuda na Yerusalemu watumwa wenu. Lakini ninyi je, hamna pia hatia ya dhambi mliyotenda dhidi ya Bwana Mungu wenu?

11Basi nisikilizeni! Mkawarudishe mateka mliowachukua kutoka kwa ndugu zenu, kwa kuwa hasira kali ya Bwana iko juu yenu.”

12Ndipo baadhi ya viongozi katika Efraimu, yaani Azaria mwana wa Yehohanani, Berekia mwana wa Meshilemothi, Yehizkia mwana wa Shalumu na Amasa mwana wa Hadlai, wakawapinga wale waliokuwa wakitoka vitani.

13Wakamwambia, “Hamna ruhusa kuwaleta hao wafungwa hapa, ama sivyo tutakuwa na hatia mbele za Bwana . Je, mnataka kuongezea dhambi yetu na hatia yetu? Kwa sababu hatia yetu tayari ni kubwa, nayo hasira kali ya Bwana iko juu ya Israeli.”

14Hivyo wale askari wakawaacha wale mateka pamoja na nyara mbele ya hao maafisa na kusanyiko lote.

15Kisha watu waliotajwa kwa majina wakawachukua wale mateka, na kutoka zile nyara wakachukua mavazi, wakawavika wale wafungwa wote waliokuwa uchi. Wakawapatia nguo na viatu, chakula na cha kunywa, wakawapa matibabu, wote waliokuwa dhaifu miongoni mwao wakawapandisha juu ya punda, wakawaleta ndugu zao Yeriko, ndio Mji wa Mitende, kisha wakarudi Samaria.

Waashuru wakataa kusaidia Yuda

(2Fal 16:7‑9)

16Wakati ule, Mfalme Ahazi akatuma wajumbe kwa mfalme wa Ashuru kuomba msaada.

17Waedomu walikuwa wamekuja tena na kuwashambulia Yuda na kuchukua mateka.

18Pia Wafilisti walikuwa wameshambulia miji iliyokuwa chini ya vilima na katika miji ya Negebu ya Yuda. Wakatwaa Beth-Shemeshi, Aiyaloni, Gederothi, Soko pamoja na vijiji vyake, Timna pamoja na vijiji vyake, Gimzo pia pamoja na vijiji vyake, wakaishi humo.

19Bwana aliishusha Yuda kwa sababu ya Ahazi mfalme wa Israeli, kwa kuwa alikuwa ameongeza uovu katika Yuda na kumkosea Bwana mno.

20Hivyo Tiglath-Pileseri mfalme wa Ashuru akaja kumtesa badala ya kumsaidia.

21Ahazi akachukua baadhi ya vitu kutoka Hekalu la Bwana , jumba la kifalme na kutoka kwa wakuu wake na kumpa mfalme wa Ashuru kama ushuru, lakini hilo halikumsaidia.

22Katika wakati wake wa mateso Mfalme Ahazi akazidi kukosa uaminifu kwa Bwana .

23Akatoa sadaka kwa miungu ya Dameski, waliokuwa wamemshinda, kwa kuwa aliwaza, “Kwa kuwa miungu ya mfalme wa Aramu imewasaidia wao, nitaitolea dhabihu ili inisaidie.” Lakini haya ndio yaliyokuwa maangamizi yake na Waisraeli wote.

24Ahazi akakusanya vyombo vya nyumba ya Mungu na kuvivunja vipande vipande. Akafunga milango ya Hekalu la Bwana na kusimamisha madhabahu katika kila njia panda ya barabara za Yerusalemu.

25Katika kila mji wa Yuda akajenga mahali pa juu pa kuabudia ili kuitolea miungu mingine sadaka za kuteketezwa na kuchochea hasira ya Bwana , Mungu wa baba zake.

26Matukio mengine ya utawala wake na njia zake nyingine zote, kuanzia mwanzo hadi mwisho, zimeandikwa katika kitabu cha wafalme wa Yuda na Israeli.

27Ahazi akalala na baba zake na akazikwa katika Mji wa Yerusalemu, lakini hawakumleta kwenye makaburi ya wafalme wa Israeli. Naye Hezekia mwanawe akawa mfalme baada yake.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.