Amosi 1

Amosi 1

1Maneno ya Amosi, mmoja wa wachungaji wa Tekoa: yale aliyoyaona kuhusu Israeli miaka miwili kabla ya tetemeko la ardhi, wakati Uzia alikuwa mfalme wa Yuda, na Yeroboamu mwana wa Yehoashi alikuwa mfalme wa Israeli.

2Alisema:

“Bwana ananguruma toka Sayuni,

pia ananguruma kutoka Yerusalemu;

malisho ya wachungaji yanakauka,

kilele cha Karmeli kinanyauka.”

Hukumu kwa majirani wa Israeli

3Hili ndilo asemalo Bwana :

“Kwa dhambi tatu za Dameski,

hata kwa dhambi nne, sitaizuia ghadhabu yangu.

Kwa sababu aliipura Gileadi

kwa vyombo vya chuma vyenye meno.

4Nitatuma moto juu ya nyumba ya Hazaeli

ambao utateketeza ngome za Ben-Hadadi.

5Nitalivunja lango la Dameski;

nitamwangamiza mfalme aliye katika Bonde la Aveni,

na yeye ambaye anaishika fimbo ya utawala katika Beth-Edeni.

Watu wote wa Aramu wataenda uhamishoni huko Kiri,”

asema Bwana .

6Hili ndilo asemalo Bwana :

“Kwa dhambi tatu za Gaza,

hata kwa dhambi nne, sitaizuia ghadhabu yangu.

Kwa sababu walichukua mateka jumuiya nzima

na kuwauza kwa Edomu,

7nitatuma moto juu ya kuta za Gaza

ambao utateketeza ngome zake.

8Nitamwangamiza mfalme wa Ashdodi

na yeye aishikaye fimbo ya utawala katika Ashkeloni.

Nitaugeuza mkono wangu dhidi ya Ekroni,

hadi Mfilisti wa mwisho atakapokufa,”

asema Bwana Mwenyezi.

9Hili ndilo asemalo Bwana :

“Kwa dhambi tatu za Tiro,

hata kwa dhambi nne, sitaizuia ghadhabu yangu.

Kwa sababu ameuza jumuiya nzima ya mateka kwa Edomu,

na kutokujali mapatano ya undugu,

10Nitatuma moto kwenye kuta za Tiro

ambao utateketeza ngome zake.”

11Hili ndilo asemalo Bwana :

“Kwa dhambi tatu za Edomu,

hata kwa dhambi nne, sitaizuia ghadhabu yangu.

Kwa sababu alimfuatia ndugu yake kwa upanga,

alikataa kuonesha huruma yoyote,

kwa sababu hasira yake kali iliendelea kupanda wakati wote

na ghadhabu iliwaka bila kuzuiliwa.

12Nitatuma moto juu ya Temani

ambao utateketeza ngome za Bosra.”

13Hili ndilo asemalo Bwana :

“Kwa dhambi tatu za Amoni,

hata kwa dhambi nne, sitaizuia ghadhabu yangu.

Kwa sababu aliwatumbua wanawake wajawazito wa Gileadi

ili kuongeza mipaka yake.

14Nitatuma moto kwenye kuta za Raba

ambao utateketeza ngome zake

katikati ya kelele za vita katika siku ya mapigano,

katikati ya upepo mkali katika siku ya dhoruba.

15Mfalme wake ataenda uhamishoni,

yeye pamoja na maafisa wake,”

asema Bwana .

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.